ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 21, 2012

NAMNA BORA YA KUACHANA NA MPENZI WAKO-2

KUUKIMBIA ukweli ni sawa na kukikimbia kivuli chako mwenyewe. Siku zote ukweli umekuwa silaha ya kwanza katika maisha ya binadamu yeyote mwenye mafanikio. Uongo hauna maana, ingawa upo wenye faida kwa muda na manufaa fulani.
Mada hii inagusa maisha yetu ya kila siku, tena wengi yanawakuta, lakini kwa hakika inaumiza na kuna ambao wapo tayari kuikimbia, ndiyo kule niliposema kukimbia kivuli chako mwenyewe!
Rafiki zangu, hebu vuta picha, uko kwenye uhusiano na mpenzi wako, mwaka sasa unakatika. Dalili zote zinaonyesha kwamba anakupenda kwa dhati ya moyo wake, lakini wewe ukijiangalia kwa ndani, ukisikiliza sauti ya ndani ya moyo wako, inakuambia kwamba huyo siye yule wako, utafanyaje?
Uendelee kujilazimisha na kupoteza muda wa mwenzako au utafute mbinu za kujiondoa? Kisaikolojia ni vyema ukatafuta mbinu za kujiondoa, ingawa sasa inategemea utatumia mbinu gani na mwenzako yupo katika hali gani.
Nilitangulia kusema wiki iliyopita kwamba, lazima ujiulize ni kwa nini unataka kumuacha mpenzi wako. Zipo sababu ndani ya makundi mawili tu; hujihisi kumpenda au umegundua siye kwa sababu ya tabia zake mbaya.
Ikiwa sababu ni hii ya pili, ni rahisi tu KUMWEKEA USHAHIDI MEZANI NA KUACHANA NAYE. Kama ni ile ya kwanza, mbinu unazotakiwa kuzitumia ni hizi ninazozifafanua katika mada hii. Yupo msomaji mmoja ambaye anaogopa ukweli, alinitumia meseji wiki iliyopita. Alilaumu sana mada hii.
Huyu hapa: “Kaka Shaluwa nakuheshimu sana na ninafuatilia sana mada zako gazetini. Kiukweli zimenibadilisha sana na nimewashawishi marafiki zangu wengi wawe wasomaji wako, lakini sasa naanza kuingiwa wasiwasi na wewe.
“Hii mada unapotosha jamii. Yaani unawafundisha watu waachane? Hapo napingana na wewe kabisa ingawa kwa muda mrefu umekuwa mwalimu wangu. Jirekebishe Shaluwa.”
Naomba nifiche jina lake, lakini naamini akisoma mada hii kwa makini atabaki na funzo kubwa sana maishani mwake. Marafiki zangu, nilisema wiki iliyopita kwamba, kipengele cha kwanza ni kupunguza mawasiliano, sasa tuendelee na dondoo nyingine...

PUNGUZA MAHABA
Mahaba ni kati ya nakshi za uhusiano, kupoteza au kupunguza mahaba humaanisha kwamba kuna jambo jipya limetokea. Sasa punguza mahaba. Kwa mfano, akikutumia meseji na kukuita kimapenzi dear, sweetie nk, wewe mjibu kwa kumwita jina lake.
Ikiwezekana mwite jina lake kamili, mathalani mpenzi wako anaitwa Joseph na umekuwa na kawaida ya kumwita Joe, mwite Josefu – ile ya Kiswahili kabisa, atagundua kuna tofauti. Majina mengine ni kama Margareth – Maggie - Magreti, Erdward – Edo - Edwadi, Abdallah – Dulla – Abdala n.k.
Mwenye macho haambiwi tazama, kwa dalili hizi ambazo utazionyesha hata mnapowasiliana kwa njia ya simu au katika mazungumzo ya mara kwa mara, atagundua kwamba kuna tatizo. Ama amechokwa au anatafutiwa sababu.
Zaidi ya yote atahisi umebadilika na huendani naye kitabia, hivyo atapendekeza muachane, jambo ambalo kwako ni sherehe.

BADILI RATIBA
Ili uweze kufikia lengo lako, ikiwa hatua za awali hazijazaa matunda, sasa badilisha ratiba zako. Kama mlikuwa na kawaida ya kuonana labda kila wikiendi, sasa mwambie una mambo mengi.
Mnaweza kukubaliana kukutana, lakini ghafla unakataa na kusema kuna mambo yameingiliana hivyo hamuwezi kuonana tena. Mabadiliko ya ratiba zako, tena ya ghafla ikiwezekana yawe na maudhi yatamgongea alamu kichwani mwake, kwamba WEWE SIYE TENA!
Cha kufurahisha sasa, yeye ndiye atakayechukua uamuzi wa kuachana na wewe. Hapo utabaki salama, ukisubiri aliye sahihi kwako. Mada bado haijaisha, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Chanzo:Global Publishers

No comments: