Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, amesema katika kushughulikia madai hayo, Serikali ya Tanzania imeanza rasmi mchakato wa kubaini maeneo halisi zilikofichwa fedha hizo.
Dk. Mgimwa aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kufungua mafunzo ya ujasiriamali.Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum mkoani Iringa (CCM), Ritha Kabati kupitia mradi wa Decision Foundation.
Katika mahojiano yake na waandishi wa habari, Dk. Mgimwa ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga, alisema ni ukweli usiopingika kwamba utoroshwaji wa mabilioni hayo ya fedha kwenda nje ya nchi unachangia uchumi wa taifa kudumaa.
Aidha, alisema mtu yeyote aliyehamisha fedha hizo kiharamu na kuwekeza nje ya nchi, atashughulikiwa kuanzia sasa kwa kuwa taratibu na uchunguzi zimeanza.
Waziri Mgimwa alisema lengo la uchunguzi huo ni kutambua fedha hizo zilipelekwa ughaibuni kwa makusudi gani, ni Shilingi ngapi pamoja na kuhakikisha serikali inawatambua kwa majina yao.
“Tumeanza kufanya mawasiliano na nchi ambazo zinatajwa kuhusika katika uhifadhi wa mabilioni hayo kwa hiyo serikali imeanza uchunguzi ikitaka kufahamu kiwango cha fedha kilichotoroshwa ili kutambua serikali imepata hasara kiasi gani na hatimaye wahusika wa tuhuma hizo kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Aliongeza: “Yeyote aliyewekeza fedha hizo nje ya nchi atashughulikiwa, kwa sababu hali hii inasababisha matatizo kwa taifa na wananchi kutokana na kuhamisha fedha kiharamu."
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment