ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 19, 2012

Watu 40 mbaroni kwa kuvamia kituo cha polisi

Na Jacqueline Massano
Jeshi la Polisi Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, linawashikilia watu 40 waliovamia kituo cha Polisi cha wilaya hiyo na kutaka kukichoma moto kwa lengo la kushinikiza waganga wa jadi, maarufu kama ‘lambalamba’ waachiwe huru.

Kundi la wananchi kutoka kata ya Mazae wilayani humo walikivamia kituo cha Polisi, Jumamosi na kufanya vurugu hali iliyolilazimu jeshi la olisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na kufanikiwa kuwatia mbaroni watu 40.

Wananchi hao walifikia hatua hiyo baada ya jeshi kuweka mtego na kuwakamata waganga hao wa jadi waliokuwa wakijiandaa kupita katika nyumba za wananchi katika kata ya Mazae kwa lengo la kutoa uchawi.

Wananchi hao wamesema walichanga kiasi cha Sh. 5,000 kila kaya ili lambalamba hao waweze kupita nyumba hadi nyumba kwaa jili ya kutoa uchawi.

Kwa mujibu wa mkuu wa Polisi Wilaya ya Mpwapwa, Jeremiah Shiva ni kwamba baada ya kutawanywa kwa mabomu ya machozi wananchi walikwenda kuvamia gari ya diwani wa kata yao, William Madanya na kuivunja vioo.

Wananchi hao walikuwa wakimuhusisha Diwani huyo kuwa ndiye aliyetoa taarifa polisi ili Waganga hao wa jadi wakamatwe.

Wananchi hao pia wanadaiwa kuchoma moto shule ya Sekondari ya Madanya new Vission iliyopo wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye, alisema wananchi hao walijipanga kwa ajili ya kutaka kuvamia kituo hicho lakini hawakufanikiwa.
“Walikuja kwa hamasa kubwa ya kutaka kuvunja, lakini azma yao haikufanikiwa kwani walitawanywa na polisi ila kuna wale ambao walijifanya ni wabishi…lakini walikamatwa,” alisema.

Mbali na hilo, alisema kutokana na hali hiyo serikali itawachukuliwa hatua kali wale wote wanaowaita waganga wa jadi wanaofika wilayani humo kwa lengo la kutoa uchawi katika nyumba za watu.

“Ila wale wote ambao wamekatwa walitarajiwa kufikishwa mahakamani juzi na tutaendelea na oparesheni ya kuwakamata wale wote ambao wanafanya udanganyifu kwa wananchi,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kukusanyika na kutaka kuvamia kituo hicho, lakini jaribio lao lilishindikana kutokana na polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.

”Ni kweli wamekamatwa na jana (juzi), wamefikishwa mahakamani...na hili litakuwa fundisho kwa wale wengine wote ambao wataendelea na suala hili la lambalamba,” alisema.

No comments: