ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 28, 2012

NAMNA BORA YA KUACHANA NA MPENZI WAKO-3


UKITAKA kuwa mjanja, usikimbie tatizo. Siku zote kujua tatizo ni mwanzo wa kuelekea kwenye mafanikio. Rafiki zangu, leo namalizia mada yetu iliyodumu hapa kwa wiki tatu; namna bora ya kuachana na mpenzi wako.
Nilishatangulia kusema huko nyuma wakati naanza mada hii, kwamba kuachana si jambo zuri sana, lakini kuna wakati kwa sababu mbalimbali unajikuta unahitaji sana kuachana na mpenzi wako.
Hata hivyo, pamoja na sababu hizo, unagundua kwamba mwenzako ana pendo zito na hana mpango wa kukuacha. Hapo wengi ndipo wanapochanganyikiwa. Je, ni sahihi ujilazimishe kuwa naye huku moyoni humpendi au uachane naye ili uepukane na matatizo yasiyo ya lazima huko mbele?
Jibu ni rahisi sana; kuachana naye. Yes! Hapo sasa ndipo kwenye mada yenyewe...kama una sababu zinazoeleweka weka mezani, ikiwa huna, vipengele vifuatavyo vinakwenda kukuachanisha naye mara moja na utabaki ukiwa mwenye amani naye akiendelea na maisha yake.
Twende sasa...

KATAA MITOKO
Kwa kawaida outing hunogesha penzi. Kama mlikuwa na kawaida ya kutoka pamoja, badilisha ratiba kwa visingizio visivyo na maana. Akitaka mtoke, mtafutie sababu.
Jambo kubwa na muhimu kwako kuzingatia hapa ni kwamba, sababu zenyewe ziwe hazina msingi, kiasi kwamba hata yeye agundue kwamba hutaki tu kutoka naye. Hata kama akiwa na hisia hasi si mbaya sana maana ndiyo lengo lililopo moyoni mwako – akuache!

MSHUSHE THAMANI
Kusifia ni jambo ambalo hustawisha penzi. Bila shaka mara kwa mara umekuwa ukifanya hivyo kwa mpenzi wako. Wakati mwingine, hata kama ni kwa mambo ya uongo, wengi hupenda tu kuwasifia wenzi wao.
Badilisha utaratibu. Sasa mshushe thamani. Unaweza kumwambia: ”Dah! hujapendeza kabisa...siku hizi huwezi kufanya uchaguzi mzuri wa mavazi.”
Kwa kauli hii lazima kuna kitu kitagonga kichwani mwake. Atajua labda una mtu mwingine anakudanganya au umemchoka tu na pengine una dharau. Hayo ni mawazo yake, tena akiwaza hivyo ni vizuri zaidi kwa sababu ni rahisi kutamka: “Kama vipi tuachane bwana..” sasa hapo kuna nini tena zaidi ya kushangilia?

MLAUMU KILA MARA
Chuki na hasira si vitu vinavyokubalika kwa wapenzi. Mara nyingi wenzi huwa na sura zenye bashasha. Wanaoneshana mapenzi na wanajaliana kwa kila hali. Hili ndilo linalotarajiwa na wengi.
Sasa wewe ukumbuke kwamba, uko kwenye kipindi cha matarajio ya kuachana naye. Usijali, kwako lawama ndiyo mtaji mzuri. Hata kama akifanya kosa dogo tu, ambalo kwa kawaida mngeweza kulisuluhisha vizuri tu, wewe unamshushia lawama.
Kuna mambo mengine yatakuwa madogo zaidi kiasi cha kumchanganya na kumshangaza, hilo lisikupe hofu, kwa sababu unaijua nia yako.

SASA ACHANA NAYE!
Kwa vipengele vyote hivyo, lazima atagundua kitu. Jambo la kufurahisha ni kwamba, anaweza kugundua kwamba wewe siye na wala si kwamba unafanya makusudi. Hapo ni rahisi zaidi kwake kujitoa.
Wapo wengine ving’ang’anizi, hawajui kukataliwa. Mkifikia hatua hiyo na bado anaendelea kuonesha uvumilivu, huna haja ya kujitesa zaidi, mwambie ukweli – kwamba ulikosea awali na sasa unahitaji kumwacha huru na maisha yake.
Rafiki zangu ni jambo jema kabisa. Kuna sababu gani ya kuendelea kuwa na mtu ambaye moyoni unajua wazi kuwa huna mapenzi naye? Uamuzi upo mikononi mwako!
Ahsanteni sana kwa kunisoma, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine kali, USIKOSE!

www.globalpublishers.info

No comments: