PADRI Ambrose Mkenda. |
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud Mohamed, alitoa tamko hilo jana jijini Dar es Salaam baada ya kutoka kumtembelea Paroko wa Kanisa Katoliki wa Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye, mjini Zanzibar, Padri Ambrose Mkenda, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Aboud akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), alisema katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza mfululizo wa mashambulizi dhidi ya viongozi wa dini hatua ambayo inailazimu serikali kufanya uchunguzi kubaini kama ni hujuma au la.
Mbali na Padri Mkenda, pia kiongozi mwingine wa dini aliyefanyiwa unyama ni Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, ambaye alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana
“Tutahakikisha tunafanya uchunguzi tujue kiini cha tatizo ni nini, kama ni hujuma tutajua, kama kuna kundi la watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi tutajua,” alisema Mohamed.
Alisema wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea na uchunguzi, wananchi wasiwe na wasiwasi kwani serikali itahakikisha wahalifu wote popote walipo wanasakwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Afisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Ismail, alisema hali ya Padri Mkenda, inaendelea vizuri na anaendelea kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo.
Waandishi wa habari wakiwa katika wodi aliyolazwa padri huyo, walifanikiwa kuzungumza na kujibu kwa kifupi kuwa anaendelea vizuri hivyo hakusimulia mkasa huo kutokana na maumivu.
Padri Mkenda alipigwa risasi Desemba 25, mwaka huu saa 1:30 usiku nyumbani kwake na watu wawili wasiojukana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa.
Juzi, Mkurugenzi wa Shule ya Francis Maria Libaman Tomondo, Padre Arbogast Mushi, alisema Padri Mkenda alipigwa risasi kupitia kioo cha mbele cha gari lake aina ya Toyota Rav4 wakati akirejea nyumbani kwake.
Baada ya kutokwa na damu nyingi, alipelekwa katika Hospitali ya Alrahama na baadaye Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambako alifanyiwa upasuaji mdogo eneo la taya na baadye kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Matukio ya viongozi wa dini kuhujumiwa yametanguliwa na matukio ya kuchomwa moto baa 12 na makanisa 25 katika maeneo tofauti visiwani Zanzibar.
Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar, Askofu Augustino Shao, juzi alisema tukio hilo limewashtua sana wananchi na waumini wa dini ya Kikristo wana imani kuwa vyombo vya usalama vitafanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwakamata waliohusika.
Askofu Shao alisema Padri Mkenda ambaye ni Mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendaye kupigwa risasi hakumaanishi kuwa waliofanya hivyo walitaka kupora fedha kwa sababu hana tabia ya kutembea na fedha za Kanisa hata siku moja.
Alisema kabla ya tukio hilo, vilisambazwa vipeperushi vya vitisho na watu wasiojulika vikiwa na ujumbe: “Viongozi wa Uamsho waachiwe huru na serikali mara moja kabla ya kufanyika sikukuu ya Krismasi, vinginevyo kutatokea tukio kubwa Zanzibar.”
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh, alisema Jeshi la Polisi limeonyesha udhaifu wa kusimamia ulinzi dhidi ya raia na mali zao.
Askofu Hafidh alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo, vilisambazwa vipeperushi vya kutishia amani, lakini hakuna hatua za tahadhari zilizochukuliwa kabla ya Padri Mkenda kupigwa risasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, juzi alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika waliofanya uhalifu huo kwa madhumuni gani kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sisi tunahesabu kuwa kitendo hiki ni kitendo cha kihalifu na tunawatafuta wahalifu waliofanya kitendo hiki kwa hiyo bado ni mapema kusema kimefanywa na nani kwa kuwa uchunguzi wetu unaendelea na hadi sasa hakuna mtu tuliyemshika kuhusiana na tukio hili,” alisema Kamanda Aziz.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment