Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu
SIKU moja baada ya kuchapishwa kwa habari kwamba Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu anamiliki kampuni inayojishughulisha na masuala ya kitalii ya Nitoke Safaris, kiongozi huyo amejitokeza na kuweka bayana umiliki wake huo.
Akizungumza kwa simu kutoka Mwanza jana, Nyalandu alisema kampuni hiyo iliyoanzishwa Aprili, 2009 ikiwa ni mali ya familia ilisitisha kazi zake tangu Mei mwaka huu baada ya kula kiapo cha kuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo.
“Baada ya kuapishwa Mei mwaka huu tulifikia makubaliano mimi na familia yangu kwamba kampuni hii isitishe shughuli kwa kuhofia mgongano wa kimasilahi,” alisema Nyalandu na kuongeza:
“Tangu wakati huo hakuna kazi iliyowahi kufanyika katika kampuni hiyo, hata aliyekuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni hiyo ambaye pia alikuwa akisimamia Jarida la Tutoke (Tutoke Magazine), Gloria Mshana alilazimika kutafuta ajira sehemu nyingine.”
“Kufuatia uteuzi wangu wa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na kwa kuzingatia uwezekano wa kuwapo mwingiliano wa kimasilahi, niliamua kusitisha shughuli zote za kibiashara za Nitoke Safaris Ltd na Tutoke Magazine, baada ya kuapishwa… Jarida la Tutoke lilichapisha toleo lake la kwanza Septemba 2009 na toleo lake la mwisho lilichapishwa Novemba 2011.”
“Nilichukua hatua hii ili nipate fursa na uwezo wa kusimamia sekta ya utalii nchini kwa haki na umakini kwa wadau wetu wote wanaojishirikisha na biashara ya utalii nchini. Kuhusu ofisi, waziri huyo alisema kampuni hiyo ilishahama katika Jengo la PPF Complex Suit, namba 24 Barabara ya Mzingo tangu mwaka 2011 na kuhamia katika eneo la Kijenge kabla ya kuzifunga miezi saba iliyopita.
Juzi, gazeti hili liliandika baada ya kufanya uchunguzi na kubaini kuwa Nyalandu anamiliki kampuni hiyo na mkewe Faraja, huku kumbukumbu za Wakala wa Usajili wa Kampuni na Leseni (Brela), zikionyesha kila mmoja ana asilimia 30 ya hisa.
Kampuni hiyo ilisajiliwa Aprili 24, 2009 na kupewa nambari 70735, wakati huo Nyalandu akiwa Mbunge wa Singida Kaskazini, wadhifa alioupata kuanzia mwaka 2000. Alipoulizwa kuhusu madai hayo juzi, Waziri Nyalandu alisema tayari alishajitoa na kufafanua kwamba kama ambavyo haipendezi yeye kumiliki kampuni ya utalii akiwa waziri wa wizara hiyo, haitapendeza pia waziri wa habari kumiliki gazeti.
“Huwezi kuwa Waziri wa Utalii na ukafanya biashara ya utalii, katika kampuni hiyo mimi nilishatoka kitambo,” alisema bila kufafanua zaidi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment