MMILIKI wa Kampuni ya McDonald inayodaiwa kupewa mkataba wa zabuni ya kufanya ukarabati wa miundombinu ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kinyemela ameanika sababu za yeye kutajwa na Mbunge wa Ubungo John Mnyika kuwa mmoja wa mafisadi unaolihujumu shirika hilo.
Katika maelezo yake aliyoyatoa jana, mmiliki huyo, Donald Mwakamele alisema kuwa hatua hiyo ni baada ya yeye kukataa kutoa rushwa kwa mmoja wa viongozi wa shirika hilo.
Katika maelezo yake aliyoyatoa jana, mmiliki huyo, Donald Mwakamele alisema kuwa hatua hiyo ni baada ya yeye kukataa kutoa rushwa kwa mmoja wa viongozi wa shirika hilo.
Hivi karibuni Mnyika, alitaja hadharani majina ya watu 16 ambao amewahusisha na ufisadi ndani ya shirika hilo la umma.
Mnyika aliwataja wafanyakazi watatu wa Tanesco akieleza kuwa walihusika katika kutoa mapendekezo yaliyowezesha kampuni hiyo pamoja na nyingine kupewa mkataba wa zabuni kinyemela, ambao alidai ndiyo wanaoshirikiana kuihujumu Tanesco na kuliingizia taifa hasara.
Akizunguzia tuhuma hizo, Mwakamele alisema ugomvi wote huo unatokana na kiongozi mmoja kutoka Kitengo cha Transimition (usambazaji umeme), aliyekuwa akitaka rushwa ya Sh100 milioni ili kuweza kutumia vikombe vilivyoagizwa na kampuni moja (jina tunalo), lakini mmiliki huyo alikataa hivyo kuwa mwanzo wa mgogoro huo.
“Huyu kiongozi hata mimi amenisumbua sana, baada ya kupewa zabuni ya mkataba wa kukarabati miundombinu ya Tanesco bila kuzima umeme Mkoa wa Arusha alinifuata mara kadhaa nimpatie rushwa,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo walianza kuwaandama yeye pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando kwani waliamini ndiye anayemsaidia kupata zabuni na hata kufikia hatua ya kusema kuwa hata Chuo cha McDonald cha Morogoro kinachotoa kozi za kufanya ukarabati wa nguzo bila kuzima umeme anachokimiliki kihalali ni mali ya Mhando.
“Si hivyo tu, walihakikisha wananinyang’anya ile kazi ya Arusha, lakini siku nikiwa na wageni kutoka mataifa 26 ya Afrika waliokuja kutembelea chuo kwa ajili ya kujifunza namna ya kukarabati nguzo bila kuzima umeme, walizima umeme mji mzima wa Morogoro na kwamba wameapa hii teknolojia ninayofanya isiwepo nchini, na ndiyo maana wanahangaika kunichafua,” alisisitiza Mwakamele.
Mwakamele alienda mbali zaidi na kumshangaa Mnyika kuwa hajui anachokitetea na kwamba hajui alikuwa na masilahi ya shilingi ngapi katika mgawo huo wa Sh100 milioni ambazo wenzake walikuwa wanazihitaji.
“Natoa Sh20 milioni kwa Mnyika kama ataweza kudhibitisha tuhuma dhidi yangu nitampatia, huu ni mpango wa baadhi ya viongozi ambao mbunge huyo haujui ameingia kichwa kichwa.”
Mnyika alitaja majina ya aliodai kuwa ni mafisadi akisema hiyo ni awamu ya kwanza ambapo wamo baadhi ya waliokuwa watendaji wa shirika hilo ambao wamesimamishwa kupisha uchunguzi unaofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alipoulizwa wiki iliyopita kuhusu uchunguzi huo, CAG, Ludovick Utouh alisema uchunguzi huo umeshakamilika na kilichokuwa kikisubiriwa ni kuikabidhi ripoti hiyo kwa Bodi ya Tanesco.
Mnyika aliwataja vigogo wengine watatu wa Tanesco na kueleza kuwa walifanya uzembe na kushindwa kusimamia sheria ya ununuzi wa umma na kupendekeza kampuni mbili kupewa zabuni, licha ya kuwa hazikutimiza masharti kwa sababu ya mgongano wa masilahi.
Aliwataja watumishi wawili ambao walishindwa kutoa taarifa za ukiukaji wa vigezo vya utoaji wa zabuni namba PA/001/09/HQ/W/014 na kufanya kampuni moja kati ya hizo mbili kupewa zabuni na kusema kuwa watendaji hao walichangia kufanya kampuni hiyo kupewa zabuni pamoja na kwamba haikuwa na fedha na kuiwezesha kupewa malipo ya asilimia za ziada kinyume na mkataba.
Akapendekeza watendaji hao kuchuliliwa hatua za kinishamu. Mnyika aliwataja watumishi wengine sita wa Tanesco ambao kwa pamoja walifanya uamuzi uliosababisha kutolewa kwa mkataba namba PA/001/HQ/W/14 wa Machi 11,2010 kwa kampuni hiyo bila kuzingatia uwezo wa kitaalamu, kifedha na hivyo kukiuka sheria ya ununuzi wa umma.
Mnyika alipendekeza wachukuliwe hatua za kisheria ili kuepusha Tanesco kuingia mikataba kuliongezea shirika mzigo wa gharama na kusababisha ongezeko la bei ya umeme.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment