ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 22, 2012

Panga la Mwakyembe lafyeka vigogo 16 Bandari

Dk. Harrison Mwakyembe
 
Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe, amewasimamisha kazi vigogo 16 wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhilifu wa mali zinazowakabili.

Aidha ametangaza kiama kwa walipata ajira kwa kutumia majina ya wajomba bila kuwa na sifa kuwa waanze kujiondoa wenyewe kabla ya kutimuliwa.

Alitangaza maamuzi hayo jana yaliyofikiwa na Bodi mpya ya Mamlaka ya Bandari baada ya kupitia ripoti ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali bandarini hapo.

Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uhandisi, mhandisi Bakari Kilo, Mkurugenzi wa Mipango, Florence Nkya, Mkurugenzi wa teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama), Ayoub Kamti, Mkurugenzi wa Mfumo wa Menejementi, Dk Maimuna Mrisho , Meneja wa Uhandisi, Mhandisi Raymond Swai, Meneja Ununuzi na Ugavi, Bahebe Machibya na Meneja Ununuzi, Theophil Kimaro.


Wengine ni Afisa Mhandisi Mkuu, Mhandisi Mary Mhayaya, Meneja wa Tehama, Macelina Mhando, Fotunatus Sandaria kitengo cha ulinzi, Fadhil Ngorongoro kutoka kitengo cha majini, Mohamed Abdallah ambaye alikuwa ni derena, Owen Rwebangila cheo chake hakikupatikana na Kilimba ambaye yupo idara ya ulinzi.

Dk. Mwakyembe alisema bodi yake imeridhia kuwasimamisha kazi vigogo hao kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

Alisema baada ya kamati ya kuchunguza tuhuma za bandari kukamilisha kazi yake, bodi yake iliipitia ripoti hiyo na kubaini mambo mbalimbali.

Alisema idadi ya vigogo waliosimamishwa kazi mpaka ni 23 na kwamba zoezi la kuwasimamisha watumishi wengine litaendelea.

Dk. Mwakyembe alisema wamegundua kuwepo kwa mgongano wa maslahi baina ya viongozi kwa kufungua kampuni zao binafsi kwa kuhudumia shughuli za bandari kinyume na sheria na kuitafuna bandari.

Alisema katika uchunguzi wao walibaini kuwa kampuni hizo hazijasajiliwa "Hizi kampuni hazijasajiliwa na Brela jambo ambalo limeishtua bodi ni kwamba kampuni hizo ni za wakubwa tayari wameandikiwa barua wajieleze ni kwanini wasichukuliwe hatua kali," alisema Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe alisema pia imebainika kuwepo kwa tatizo utoaji wa ajira bila kufuata sheria. "Watu wanapeana ajira kwa kuwa anamkubwa wake hapa bandari."

"Kuajiriwa bandarini ni kazi bila kuwa na mjomba hupati ajira hili shirika baadaye litakuwa ni la ukoo nasema kuwa aliyeingia bila kuwa na sifa ajiondoe mwenye kwani anaweza kuambulia fedha lakini akisubiri nimuondoe ataambulia patupu," alisema Dk Mwakyembe.

Alisema mambo mengine yaliyoonywa na bodi hiyo ni kukithiri kwa vitendo vya wizi na kusema kuwa suala hilo linafanywa na mtandao mkubwa na kwamba wamejipanga kuuvunja mtandao huo.

Alisema wakati alipoingia bandari ilivunja rekodi kwa vitendo vya wizi, ukiritimba pamoja na ucheleweshaji wa mizigo kwa wateja.

Dk Mwakyembe alisema kwa kipindi cha mwaka jana makontena 30 yameyeyuka jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na hatua zinatakiwa kuchukuliwa ili tatizo hilo liweze kumalizika.

Alisema hivi karibuni alipokutana na Rais wa Demokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, alimjulisha kuwa serikali yake ipo katika mchakato wa kuacha kuitumia bandari ya Dar es Salaam kutokana na kukithiri kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo vitendo vya wizi.

Alisema ilipofika septemba mwaka huu mapato yaliongezeka na kufikia bilioni 38 kwa mwezi, Oktoba yalifikia bilioni 40 na mwezi Novemba natarajia yatakuwa yamepanda.

Alisema haiwezekani bandari ya Mombasa kukusanya kiasi cha sh bilioni 300 kwa mwezi halafu kwa bandari ya Dar es Salaam ambayo inatetegemewa kwa kiasi kikubwa kukusanya mapato ya sh bilioni 28.

Dk. Mwakyembe alisema tatizo lililopo ni kuwepo kwa mtandao wa wizi" unajua nilikuwa nikisikia miujiza ya twiga kuingia kwenye ndege nilikuwa najiuliza hivi anaingiaje sasa ni hivi inakuweje kontena linakuwepo na kuyeyuka kama kibiriti," alihoji

No comments: