ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 22, 2012

Tisa kutoa ushahidi kesi ya Lulu

Msanii Elizabeth Michael a.k.a'Lulu
 
Mashahidi tisa upande wa mashitaka akiwemo aliyekuwa daktari wa marehemu Steven Kanumba, wanatarajia kutoa ushahidi wao katika Mahakama Kuu wakati kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili msanii Elizabeth Michael 'Lulu' itakapoanza.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Agustina Mmbando, aliyasema hayo jana mahakamani hapo, wakati upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, uliposoma maelezo ya mashahidi hao.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo alibadilishiwa shitaka la kuua na kusomewa jipya la kuua bila kukusudia.
Wakili Kimaro aliieleza mahakama hiyo kuwa mara baada ya kesi hiyo kuanza kwenye Mahakama Kuu, moja ya vielelezo vitakavyotolewa na upande wa mashitaka ni nyaraka yenye ramani iliyochorwa April 7, mwaka huu eneo la tukio hilo.

Alisema ramani hiyo iliyochorwa nyumbani kwa marehemu Kanumba inaonyesha mwili wake pamoja na vyumba vya nyumba aliyokuwa akiishi.

Kadhalika alisema vielelezo vingine ni ripoti ya uchunguzi wa daktari inayoonyesha sababu za kifo cha Kanumba.

Aliongeza kuwa maelezo ya awali ya mshtakiwa Lulu aliyoyatoa katika kituo cha Polisi Oysterbay, yatatumika kama ushahidi Mahakama Kuu.

Aliwataka mashahidi wengine kuwa ni mdogo wa marehemu, Seki Bosco, mama mwenye nyumba aliyokuwa akiishi marehemu, Sofia Kasimu na daktari wa marehemu, Paplas Kagaige.

Wengine ni Daktari Magreth mkazi wa Tabata Kimanga ambaye alisimamia uchunguzi wa awali wa mwili wa marehemu uliofanyika Muhimbili chini ya jopo la madaktari.

Mshtakiwa huyo amerudishwa rumande hadi hapo kesi hiyo itakapopelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.

Elizabert alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za mauaji ya Kanumba yaliyotolea Aprili 7, mwaka huu.

Jana asubuhi maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam baadhi ya watu walieneza uvumi kuwa mshtakiwa huyo ameachiwa kwa dhamana.

CHANZO: NIPASHE

No comments: