ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 9, 2012

Tujivunie nini miaka 51 ya Uhuru?

LEO nchi yetu imetimiza miaka 51 tangu ilipopata Uhuru mwaka 1961. Miaka yapata 20 iliyopita, siku kama ya leo ilikuwa ikiadhimishwa kwa sherehe mbalimbali nchini kote.
Ni siku iliyokuwa na bashasha na nderemo kwa wananchi kuimba na kucheza kwa hisia kubwa, ikiwa ni kumbukumbu ya siku aliyoondoka mkoloni na kuwaacha wazalendo wakijipanga kuendesha mambo yao wenyewe.

Pamoja na matatizo mengi ya kiuchumi yaliyokuwapo wakati huo, wananchi walikuwa na matumaini makubwa kwamba ipo siku matatizo hayo yangemalizika. Hii ilikuwa sawa kabisa kwa sababu wakati huo wananchi walikuwa na imani kubwa na viongozi wao ambao hakika waliweka mbele masilahi ya wananchi.

Hoja hapa siyo kwamba siku kama ya leo haisherehekewi. La hasha. Mwaka jana, kwa mfano ziliandaliwa sherehe kubwa nchi nzima ikiwa ni kumbukumbu ya Miaka 50 ya Uhuru zilizotumia zaidi ya Sh60 bilioni. Kama tutakavyoshuhudia baadaye leo, zitakuwapo pia sherehe mbalimbali kama gwaride, burudani, michezo na ngoma na zitatumika fedha nyingi pia. Hata hivyo, hoja ni kwamba sherehe za miaka ya hivi karibuni zimekosa hamasa na msisimko kutokana na wananchi wengi kupoteza matumaini ya kupata maisha bora kinyume na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Matumaini ya maisha bora kwa wananchi yamepotea kutokana na kusalitiwa na viongozi. Viongozi walipolitosa Azimio la Arusha walikuwa pia wameutosa uzalendo na kukumbatia ufisadi ambao kama tulivyoshuhudia, ndiyo hasa umeporomosha uchumi wetu na kuwaacha wananchi katika lindi la umaskini wa kutisha. Sera za ubinafsishaji uliohusisha pia nguzo kuu nyingi za uchumi uliua asilimia kubwa ya viwanda vyetu vilivyokuwa vikitoa ajira kwa wananchi.

Hayo ndiyo matokeo ya viongozi kukosa uzalendo. Wananchi wanaposikia kashfa za ufisadi wa viongozi kila kukicha, utoroshaji wa mali asili, mabilioni ya Uswisi, kashfa za Kagoda, Epa, Meremeta, Kiwira, Richmond, Dowans na nyingine nyingi, wanakosa matumaini ya maisha bora kwa kuwa hawaoni juhudi za dhati zikifanyika kuwawajibisha wahusika ambao wanajulikana kwa mamlaka zote za nchi.

Ndiyo maana wananchi wengi, hasa maelfu kwa maelfu ya vijana walio vijiweni kwa kukosa ajira wanauliza kwamba wajivunie nini katika kusherehekea kumbukumbu ya miaka 51 ya Uhuru wetu. Hivyo pia ndivyo wanavyosema maelfu ya wakulima, wafanyakazi, wafugaji na makundi mengine mengi nchini ambayo hayaoni nini hasa cha kusherehekea kutokana na uduni wa maisha yao.

Sherehe hizo za kila mwaka hazitakuwa na maana iwapo viongozi hawatairudisha nchi yetu katika misingi ya utu, haki, usawa, umoja, uzalendo, upendo na mshikamano. Pasipo kutumia rasilimali za nchi kuinua hali za wananchi wote, viongozi wetu watambue kwamba sherehe kama za leo zitakuwa hazina maana yoyote.

No comments: