ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 9, 2012

Ufisadi wazidi ‘kuitafuna’ serikalini

Waziri John Magufuli

*Watendaji wabadili umiliki na kujilimbikizia magari kiholela
Wakati taifa likiwa katika mchakato wa kulinda mali za umma, vita dhidi ya ufisadi inazidi kupoteza nguvu, kutokana wenye dhamana za uongozi, kujitwalia mali kinyume cha sheria.

Moja ya maeneo yaliyokumbwa na kashfa hiyo, ni magari ya umma, ambayo watendaji kadhaa serikalini wamebainika kuyabadili namba na kujimilikisha.

Tayari Wizara ya Ujenzi inayoongozwa na Waziri John Magufuli, imeweka wazi ukweli wa kushamiri kwa ufisadi huo, ikieleza kuwepo idadi kubwa ya watumishi na watendaji wanaotuhumiwa.

Baada ya jitihada za muda mrefu za NIPASHE Jumapili kumtafuta Magufuli bila mafanikio, Msemaji wa wizara hiyo, Martin Ntemu, anathibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo viovu.Awali, NIPASHE Jumapili ilielezwa kuwa kugundulika kwa ufisadi dhidi ya magari ya umma, kulitokana na hatua ya Magufuli, kuanzisha operesheni maalum ya kusaka magari ya umma yenye namba binafsi, yasajiliwe kwa namba za serikali.

Ntemu alisema tangu operesheni ya Magufuli ianze, magari mengi na pikipiki yalibainika kuchukuliwa na kumilikiwa kinyemela.

“Imebainika kuwepo magari mengi na pikipiki ambazo ni mali ya umma, lakini zimebadilishwa namba na sasa zipo mikononi mwa watu binafsi, tena kinyume na sheria na utaratibu,” alisema.

Alisema wakati zoezi la kuyabadilisha namba magari hayo linaanza, Magufuli alitoa muda wa siku 18 kwa kazi hiyo kukamilika, lakini ilionekana muda huo hautoshi.

Alisema hali hiyo ilitokana na kugundulika kuwepo mali nyingi za umma hasa magari ya pikipiki katika halmashauri za wilaya na mikoa, zilizobadilishwa na kumilikiwa na watu binafsi hususani watendaji na watumishi wengine.

"Waziri (Magufuli) alitoa dira ya zoezi zima, lakini operesheni ilipoanza ilibainika tatizo ni kubwa sana kwani watu wengi wanamiliki magari na pikipiki za serikali kinyume cha sheria na taratibu,” alisema.

Kwa mujibu wa Ntemu, tatizo ya kujimilikisha magari na pikipiki za umma lilibainika kuwa kubwa, kiasi cha kuifanya serikali iongeze muda ili kulifikia eneo kubwa zaidi.

Miongoni mwa magari yanayodaiwa kuhujumiwa ni yaliyotumika katika miradi ya maendeleo na ustawi wa jamii, yakitolewa na wahisani wa nje ya nchi.

Serikali imekuwa ikishirikiana na wahisani wanaofadhili miradi hiyo kwa fedha, utaalamu na vifaa kama magari na pikipiki, lakini inapofikia ukomo wao (wahisani), watendaji na watumishi wamekuwa wakiihujumu kwa kujimilikisha.

“Hata kama magari, pikipiki na vifaa vingine vinaachwa na wahisani, inakuwa mali ya umma na haipaswi kujimilikisha kwa mtu binafsi,” alisema.

Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili ulibaini kuwepo uhujumu wa mali hizo hususani katika miradi ya maji, mazingira, afya na kilimo.

"Watu wengine walijua magari hayo waliyofadhiliwa hayapo chini ya serikali baada ya miradi kumalizika, lakini ni mali ya umma na lazima yarudishwe serikalini," alisema Ntemu.

Wakati karipio hilo likitolewa, taarifa za ndani zimelifikia NIPASHE Jumapili zikieleza kuwepo watendaji waliojimilikisha magari na pikipiki, wameanza kuyarejesha.

Hata hivyo, hakuna takwimu halisi zilizopatikana kuhusu idadi ya magari na pikipiki zinazodaiwa ‘kuporwa’, ingawa Ntemu alisema taarifa kamili itatolewa na Magufuli hivi karibuni.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Oktoba 20 mwaka huu, Magufuli alitangaza kuanzisha zoezi rasmi la kurejesha usajili wa magari yote.

Alisema mpaka ifikapo Novemba 15, mwaka huu magari ya umma yenye namba za kiraia, yangerejeshewa namba stahiki za magari ya umma.

Magufuli alisema magari hayo na pikipiki yatakuwa na aina ya namba za usajili zitakazotumika kama ST, PT, MT,JW, DFP, CW, SM na SU.

Hadi sasa serikali imesajili vyombo vya moto, 123,431 yakiwemo magari, pikipiki, bajaj na mitambo ya umma.

CHANZO:NIPASHE

No comments: