Monday, December 24, 2012

Usafiri wa mikoani balaa tupu


*Tayari Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra), imeyakamata mabasi 11 madogo ya kusafirisha abiria yakifanya hivyo. Hata hivyo wenye mabasi hayo wametozwa faini ya Sh250,000 kwa kila gari moja.
WINGI wa watu wanaosafiri kutoka jijini Dar es Salaam, kwenda mikoani, umetoa mwanya kwa baadhi ya wamiliki wa mabasi katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo, kupandisha nauli.

Mwananchi ilifika UBT majira ya asubuhi na kukuta umati mkubwa wa watu wakiwa wanahangaika kutafuta usafiri wa kuelekea mikoani, tayari kwa kuungana na ndugu zao katika kusherehekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Wingi huo wa watu usiowiana na idadi ya mabasi katika kituo hicho, pia umewalazimisha watu wenye daladala kutumia mabasi yao, kusafirisha abiria isivyo halali.


Tayari Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra), imeyakamata mabasi 11 madogo ya kusafirisha abiria yakifanya hivyo. Hata hivyo wenye mabasi hayo wametozwa faini ya Sh250,000 kwa kila gari moja.Upungufu mabasi umewaathiri zaidi abiria wanaokwenda katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Morogoro, Tanga na Dodoma.
Nauli ya kwenda Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro hasa Moshi, jana ilifikia Sh45,000 kutoka Sh25,000 ya awali wakati Tanga ikiwa imefika Sh17,000 kutoka Sh13,500.
Abiria mmoja aliyekuwa anasubiri usafiri wa kuelekea Moshi, Salia Mkoi, alisema usafiri katika Kituo cha Ubungo ulikuwa mgumu kuliko wakati mwingine huko nyuma.

“Nimefika hapa tangu saa 11.30 alfajiri lakini mpaka sasa (saa 4.00asubuhi) sijapata usafiri na licha ya kwamba baadhi ya magari yamepandisha nauli hadi kufikia Sh45,000 lakini bado hayapatikani,” alisema Mkoi. Abel Frank aliyekuwa anasubiri usafiri wa kuelekea Tanga ,alisema hali si shwari kwani kila mkoa usafiri ni mgumu.

Frank alisema wamiliki wa mabasi wanatakiwa kujizatiti kwa kuongeza huduma za mabasi hususan wakati huu wa sikukuu.

“Mwisho wa mwaka usafiri unakuwa mgumu kila mwaka ,Sumatra na wamiliki wa mabasi wanatakiwa kujipanga ili kutowanyima fursa abiria kusafiri na kwenda kula sikukuu,” alisema Frank.
Kwa upande wake, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra katika Kanda ya Mashariki, Konrad Shio, alisema wameimarisha ukaguzi na kuwataka wananchi kuonyesha ushirikiano pale wanapopandishiwa nauli.

Shio alikiri kuwapo kwa baadhi ya magari yanayopandisha nauli, lakini akalaumu baadhi ya wananchi kwa kutoonyesha ushirikiano.

Chanzo: Mwananchi

No comments: