ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 28, 2012

Watahiniwa 1,818 NBAA wafeli

Watahiniwa 1,818 kati ya 3,856 waliofanya mitihani ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) Novemba, mwaka huu, wamefeli mitihani hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, Pius Maneno, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana alisema watahiniwa 703, ambao sawa na asilimia 18.2 ndio waliofaulu mitihani hiyo na 1,332 sawa na asilimia 34.6 watalazimika kurudia masomo waliyofeli mwakani.

Alisema katika ngazi ya mwisho (Final Stage Module F), watahiniwa 173 sawa na asilimia 15.6 ya watahiniwa 1,110 waliofanya mtihani huo wamefaulu, 502 watarudia somo moja na 435 hawakufaulu.

Maneno alisema katika mtihani wa taaluma ngazi ya Module ‘E’, watahiniwa 304 kati ya 2,033 wamefaulu mtihani, 521 watarudia somo moja na 1,208 wamefeli.

Alisema watahiniwa 188 waliofanya mtihani wa Shahada ya Juu ya Uhasibu nchi I-CPA (T), wamefaulu na kwamba, idadi hiyo inafanya jumla ya waliofaulu mitihani ya CPA kufikia 4,323 tangu mitihani hiyo ianze mwaka 1975.

Katika ngazi ya Module “D”, watahiniwa 63 kati ya 131 waliofanya mtihani huo wamefaulu na 53 sawa na asilimia 40.5 watarudia somo moja na watahiniwa 15 wamefeli.

Alisema watahiniwa 25 waliofanya mtihani wa ngazi ya Module “C”, wamefaulu mtihani huo, 70 watarudia somo moja na 61 sawa na asilimia 39.1 hawakufaulu.

Katika ngazi ya Module “B”, watahiniwa 47 kati ya 109 waliofanya mtihani huo wamefaulu, 54 watarudia somo moja na wanane wamefeli, wakati ngazi ya Module “A” 24 wamefaulu, 33 watarudia mtihani na wanane wamefeli.

Alisema katika ngazi ya Uandishi na Utunzaji wa Hesabu (ATEC II), watahiniwa 23 kati ya 117 wamefaulu mitihani na 56 hawakufaulu wakati katika ngazi ya awali ya mitihani ya Uandishi na Utunzaji wa Hesabu (ATEC I), watahiniwa 44 wamefaulu, 61 watarudia somo moja na 27 wamefeli.

Maneno alisema watahiniwa, ambao wamefeli mitihani hiyo, watarudia Mei 7-10, mwakani.

CHANZO: NIPASHE


No comments: