Dr.Emmanuel Nchimbi
NA RICHARD MAKORE
Jumla ya silaha 310 zimesalimishwa kwa vyombo vya dola, ofisi za serikali na taasisi za dini kufuatia agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Dk. Nchimbi alimtaka mtu yeyote ama kikundi cha watu kinachomiliki kinyume cha sheria kuzisalimisha ndani ya siku 30 kuanzia Desemba 4, mwaka jana.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Issac Nantanga, aliliambia NIPASHE juzi kuwa baada ya agizo la Dk. Nchimbi, watu kadhaa waliokuwa wanamiliki silaha kinyume cha sheria walianza kuzisalimisha kwa vyombo vya dola.
“Tangu agizo la Waziri kutolewa, tumekuwa tukipokea silaha nyingi kutoka kwa watu mbalimbali na hakuna hatua zozote walizochukuliwa wahusika kwa kuwa wamezileta wenyewe,” alisema Nantanga.
Katika agizo hilo, Dk. Nchimbi alieleza kwamba silaha hizo zisalimishwe katika vituo vya polisi, wenyeviti wa vitongoji, vijiji, watendaji wa kata, taasisi za kidini wakuu wa wilaya na mikoa.
Hatua hiyo inafuatia kuwapo kwa tatizo la kuzagaa na matumizi holela ya silaha hizo, ambazo zimekuwa chimbuko la uhalifu, unaohusisha matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha ambao hujitokeza sehemu mbalimbali nchini.
Akitangaza agizo hilo Desemba 4, mwaka jana, Dk. Nchimbi alisema kumbukumbu zilizopo na taarifa za operesheni zilizofanyika maeneo mbalimbali nchini kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka juzi, zinaonyesha kuwapo kwa matukio 876 ya uhalifu, ukiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha.
Waziri Nchimbi alisema kuwa katika kipindi hicho, silaha 62 ziliibwa ama kunyang’anywa kutoka kwa wamiliki wake halali na jumla ya silaha 304 zilikamatwa katika matukio mbalimbali ya uhalifu.
Pia Waziri Nchimbi alisema kuwa katika kipindi hicho, matukio ya ujambazi yalikuwa 876, ambayo yalisababisha vifo 138 vya raia na sita vya askari.
Vile vile, alisema katika kipindi hicho, jumla ya mali zenye thamani zaidi ya Sh. bilioni 4.5 ziliibwa kwa kutumia silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria, zikiwamo zinazomilikiwa kisheria, lakini zinatumika isivyo halali.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha kwamba miongoni mwa jamii, kuna baadhi ya watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na isivyo halali.
“Kufuatia hali hiyo, natoa wito kwa mtu yeyote ama kikundi chochote kinachomiliki silaha kinyume cha sheria na isivyo halali hapa nchini kusalimisha silaha hizo katika vituo vya polisi, wenyeviti wa vitongoji, vijiji, watendaji wa kata, taasisi za kidini, wakuu wa wilaya na mikoa,” alisema Dk. Nchimbi.
Alisema hakutakuwa na hatua zozote za kisheria dhidi ya yeyote atakayesalimisha silaha kwa hiari na kwamba, msalimishaji wa silaha hiyo hatabughudhiwa kwa namna yoyote ile.
Hata hivyo, alisema baada ya muda huo kumalizika, operesheni kali itafanyika nchini kote na kwamba yeyote atakayebainika akimiliki silaha isivyo halali, atakamatwa na sheria itachukua mkondo wake.
Akizungumza na NIPSHE ofisini kwake juzi kuhusiana na usalimishaji wa silaha unavyoendelea, Dk. Nchimbi alisema baada ya kesho kutwa ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kuzisalimisha silaha hizo kwa hiari, atatoa taarifa kamili kuhusu agizo lake alilolitoa mwishoni mwa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment