Harusi ya Consaliva Kudaga (33), imegeuka kilio na simanzi baada ya mtarajiwa huyo kupata ajali na kufariki dunia eneo la Ngiloli, Gairo mkoani Morogoro, siku moja kabla ya harusi.
Consaliva alikufa peke yake katika ajali hiyo, iliyohusisha pia wapambe wake wakati wakisafiri kuja Dar es Salaam kutoka Mwanza kusherehekea harusi yake ilikuwa ifungwe jana mchana.
Wakiwa ndani ya gari aina Coaster yenye namba T 146 CDG iliyokuwa inaendeshwa na Ahmed Rashid waligongana na lori aina ya Isuzu lenye namba B 3839 ikiendeshwa na raia wa Burundi Juma Galungu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo kwenye barabara kuu ya Morogoro-Dodoma.
Alisema ilitokea juzi jioni baada ya isuzu hiyo mali ya Nduwaye Erick raia wa Burundi lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Burundi, kugongana uso kwa uso.
Marehemu Consaliva wakati wa uhai wake alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Kanilo iliyopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Baadhi ya mashuhuda walisema biharusi huyo alikuwa kwenye gari hiyo ya kukodi alikuwa ameambatana na walimu wenzake, ndugu na marafiki kwa ajili ya ndoa yake iliyotarajiwa kufungwa jana jijini.
Aidha NIPASHE Jumapili ilitaarifiwa kuwa gari la bibi harusi lilikuwa na abiria 29 walikuwa wakimsindikiza.
Akizungumzia zaidi mkasa huo Shilogile alisema katika ajali hiyo mbali ya kifo hicho abiria wengine 21walijeruhiwa wakiwamo madereva wa magari hayo. Mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Serikali ya Dodoma.
Alisema dereva Galungu ambaye gari yake ndiyo lilikuwa chanzo cha ajali hiyo kutokana na kuwa kwenye mwendo wa kasi hali yake ni mbaya na kwamba alikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Dodoma wakati mwenzake amevunjika miguu.
Kamanda Shilogile alisema kati ya majeruhi hao, 11 walitibiwa na kuruhusiwa wakati wengine wanatibiwa katika hospitali za: Taifa ya Muhimbili, Berega Misheni na ya Mkoa wa Morogoro.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment