ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 12, 2013

Maadhimisho mema ya Mapinduzi, tuzingatie umoja, mshikamano

Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh Dk Ali Mohamed Shein 

SIKU kama ya leo miaka 49 iliyopita, vijana jasiri wa Kiafrika waliupindua utawala uliokuwapo katika Visiwa vya Unguja na Pemba kwa madhumuni ya kujipatia utawala wa kizalendo ama kwa maneno mengine kujiongoza wenyewe.

Ni miaka 49 ya changamoto nyingi, pia ni miaka ya mafanikio katika nyanja anuai. Kwa mantiki hiyo, tunachukua nafasi hii kuwapongeza Wazanzibari kwa kuadhimisha Miaka 49 ya Mapinduzi.

Walipotoka ni mbali, lakini angalau waendako huko mwanga wanauona kwa sababu wamejitambua. Dhamira zilizokusudiwa nyingi zilitekelezwa kama vile kutoa haki sawa, kutoa elimu bila malipo, kutoa huduma za afya, maji, elimu na barabara hadi vijijini.
Siyo kama hakuna matatizo, lakini ni makosa kusema hakuna kilichofanywa kwani Zanzibar ya mwaka 1963 siyo Zanzibar ya leo.

Maendeleo yaliyokuwapo mwaka 1963 siyo maendeleo ya leo, bila shaka pamoja na changamoto zote zilizopo, yapo mambo yamefanyika kwa vizuri, yapo maendeleo yaliyopatikana. La muhimu zaidi ni kule kuvunja umwinyi na ukabaila, hivi sasa Wazanzibari ni wamoja, hakuna bwana zaidi ya mwingine.

Hata hivyo, Wazanzibari wanasherehekea miaka 49 ya Mapinduzi wakiwa na changamoto nyengine kubwa, nayo ni ile ya kutoka sauti za kutaka mabadiliko ya mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hawa wanataka Zanzibar iwe huru zaidi na kuwa na mamlaka yake kamili na hata kama Muungano utakuwapo, basi Muungano huo uwe wa mkataba, siyo huu tulionao, ambao wanauita kuwa ni wa Katiba.

Mkataba kwa maana ya kuwa Watanganyika na Wazanzibari waamue ni mambo gani yawemo kwenye Muungano na yapi yasiwemo na kisha wawekeane makubaliano ya kukutana tena baada ya muda fulani kuangalia mambo ambayo wangependa kuendelea nayo.
Hivyo, kimsingi wanataka ziwepo Serikali tatu; ya Tanganyika, ya Zanzibar na ya Muungano ambayo itasimamia mambo machache tu.

Madai haya yameibuka kwa nguvu wakati huu ambapo Watanzania tupo katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Haya ni madai ambayo ingawa yanapaswa kufanyiwa kazi, lakini yatulazimu kuchukua hatua za ziada kuhakikisha kwamba Muungano wetu hauvunjiki.
Kinachoweza kufanyika kwa masilahi ya Watanzania ni kuuboresha Muungano uliopo na madai hayo yachukuliwe kama chachu ya kushughulikia kero za Muungano kwa nguvu zaidi, tusiigeuze desturi kuwa kila mwaka tunahadithia kero hizo hizo, wakati jitihada za kuzitatua hazionekani.
Kwa kuwa huu ni wakati wa kujitathmini, mawazo mbadala tusiyachukulie kuwa ni potofu, bali tuyafanyie kazi na kubadilisha yale yanayotukwaza kama taifa, huku tukitilia maanani masilahi ya Tanzania.

Tunawawatakia Watanzania maadhimisho mema ya Mapinduzi, huku tukizingatia umoja na mshikamano. Ni umoja wetu ndiyo unaotufanya tutambulike kuwa ni Watanzania na tuheshimiwe kwa hilo.

Tunaamini kuwa muungano wetu ni tunu ambayo watu wengi duniani wanaitamani kuwa nayo.

Kama walivyosema unaweza kuwa na kitu kizuri, ukakiona hakina thamani sana , lakini siku kikitoka ndipo utaiona thamani yake.

Ni vyema sasa wakati Wazanzibar wakisherehekea mapinduzi, kuelewa pia kwamba wanatakiwa kuuenzi muungano.
Mwananchi


No comments: