ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 12, 2013

MAUAJI YA KUCHINJA WANAWAKE:Polisi wanasa mtandao wa wauaji Butiama

Kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na raia wema, wamefanikiwa kuunasa mtandao wa watu wanaojihusisha na uchinjaji wanawake, na kutumia damu na baadhi ya viungo vya miili yao kwa mambo ya kishirikiana.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE Jumamosi na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angeline Mabula, umebaini kuwa miongoni mwa watu muhimu katika mtandao huo, wamejulikana, kukamatwa na kuhojiwa na polisi.

Washukiwa hao wanadaiwa kushirikiana na watu mbalimbali kufanikisha mauaji hayo, ingawa mengine yanayofanyika hayana dalili za kishirikina.

“Wapo waliokamatwa kwa kuhusika moja kwa moja na mauaji hayo na wamekiri baada ya mahojiano tulivu na polisi, sasa wanaisaidia (polisi) kuutambua mtandao mzima uliopo ndani na nje ya wilaya ya Butiama,” kilieleza chanzo chetu.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mabula akizungumza na waandishi wa habari wa The Guardian Limited ofisini kwake mjini hapa juzi, alithibitisha kukamatwa kwa watu kadhaa.
Mabula anasema, “zipo taarifa nyingi zilizopatikana kuhusu mtandao huo, lakini kuzi-reveal (kuzitangaza zijulikane) kwa sasa kunaweza kuathiri mwenendo wa upepelezi.”
Mabula anasema tangu kuwepo kwa taarifa za kuuawa watu kwa imani za kishirikina, kiasi cha watu watano wameripotiwa kupoteza maisha.

“Zipo taarifa zilizotolewa zikihusisha idadi kubwa ya watu waliouawa, lakini ripoti rasmi tulizonazo ni watu watano,” alisema.

Wakati Mabula akitoa idadi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome, aliiambia NIPASHE Jumamosi mapema wiki hii ofisini kwake, kwamba watu wanane waliuawa, ingawa kwa matukio yasiyohusishwa na  ushirikiana.

Kwa hali hiyo, idadi rasmi inayotolewa na viongozi hao wa serikali wilaya za Musoma na Butiama inafikia watu tisa, lakini taarifa zilizokariri vyanzo tofauti zilitaja idadi hiyo kufikia 17.

WALIOUAWA BUTIAMA WATAJWA
Mabula alisema waliouawa kwa vipindi tofauti katika mauaji yanayohusishwa na ushirikina ni watoto Wegesa Mwikwabe (6) na Tatu Mwikwabe (4) wa kata ya Buswahili, waliouawa Agosti, mwaka jana.

Wengine na miezi waliouawa kwenye mabano ni Norbert Mshumbuzi (58) wa kata ya Nyegina (Septemba mwaka jana), Mkwaya Busiya (47) wa kata ya Mkirira aliyechomwa kisu tumboni na kukatwa kiganja cha mkono.

Mabula alimtaja mwingine kuwa ni Blandina Peru (28) wa Etaro, aliyechinjwa na wauaji kuondoka na damu huku Sabina Mkireri (44) wa Nyakatende akichinjwa njiani na (wauaji) walichukua kichwa chake.

Pia yupo mkazi wa kata ya Mugango, Tabu Marubira, aliyechinjwa baada ya wauaji kumvamia usiku akiwa amelala.

Kichwa chake (Tabu) kiliokotwa baada ya kutupwa na watu waliomchinja, walipofukuzwa na watoto wa marehemu wakishirikiana na wananchi kufuatia yowe iliyopigwa.

MAKACHERO WAJICHIMBIA KUSAKA WAHALIFU
Wakuu wa wilaya za Musoma na Butiama, Msome na Mabula, wamethibitisha kuwepo ushirikiano wa makachero wa upelelezi waliotumwa mahususi kufanikisha kupatikana kwa mtandao na wafadhili wa mauaji hayo.

“Kwa hatua tuliyofikia sasa, niseme tumepata njia nzuri ya kufikia kuubaini mtandao wote, kwa maana waliokamatwa wanatoa msaada mzuri kwa vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema.

Makachero hao wakiwemo kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam, wanasemekana kusambazwa maeneo tofauti hususani vijijini, wakitafuta taarifa sahihi na kufanikisha kukamatwa kwa wahusika.

NIPASHE Jumamosi ilibaini kuwepo watu sita waliotoa taarifa zenye kuisadia polisi wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Sabina.

Pia watu watatu wenye taarifa kama hizo wameshakamatwa na kuhojiwa kuhusiana na mauaji ya Blandina, huku watu wengine zaidi wakiendelea kusakwa.

“Tutafika mahali tatizo hilo litashughulikiwa na kupata suluhu huku wahusika wakichukuliwa hatua, kwa maana polisi wetu wanatumia utaalamu mkubwa,” alisema Mabula, Mkuu wa wilaya ya Butiama.

DIWANI WA CCM, BABA YAKE WAKAMATWA
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Diwani wa kata ya Mugango (CCM), Wandwi Maguru amekamatwa na polisi kuhusiana na mauaji ya Tabu Marubira.

Diwani ambaye taarifa za awali za kukamatwa kwake zilimhusisha pia baba yake mzazi, anaendelea kushirikiliwa na polisi kwa mahojiano.
CHANZO: NIPASHE

No comments: