Mpenzi msomaji, karibu tena kwenye safu yetu ya Maisha Ndivyo Yalivyo.
Bila shaka bado unafuatilia kwa makini mada zangu na unaelimika vya kutosha. Wiki ijayo nitajumuisha maoni ya mada tatu zilizopita lakini leo ngoja nikumegee kituko cha baadhi ya ya kinamama wanaothamini starehe kuliko malezi ya watoto wao.
Wiki hii nikiwa maeneo ya Uru mjini Moshi, nilisimuliwa kisa cha mtoto mmoja mdogo mwenye umri wa miaka mitatu hivi wa kiume ambaye aligongwa na gari na hivi sasa amelezwa katika hospitali ya KCMC Moshi chumba cha wagonjwa mahututi.
Majirani wa pale nilikofikia kwa binamu yangu wakawa wanasema kuwa mtoto huyo ni mara nyingi tu amekuwa akikoswakoswa na magari kwenye barabara hiyo itokayo mjini kwenye Uru kupitia Rau Madukani.
Hitoria niliyoipata kuhusu mtoto huyo ni kwamba mama na baba yake ambao ni wanandoa mara nyingi wamekuwa wakizozana na hivyo mwanamke kuondoka na kwenda kujibanza kwa mashoga zake wa kike.
Wanandoa hao wana watoto wanne na huyo aliyegongwa ndio mdogo.
Inaelezwa kuwa mwanamama huyo amekuwa hajishughulishi na watoto wake na hata wanapokorofishana na mumewe huwaacha watoto wake na kuishia.
Lakini cha ajabu, pale anapokwenda kupata hifadhi siyo mbali sana na makazi ya mumewe na ndio maana mtoto huyo mdogo anapojisikia kumuona mamake hutoroka na kuvuka barabara kumfuata aliko.
Jambo lingine ambalo nilisikia likizungumzwa kuhusu mwanamama huyo ni kwamba amekuwa ni mpenda madisco na siyo ajabu ndio sababu kubwa inayomfanya azushe jambo na mumewe ili apate mwanya wa kwenda kujirusha na mashoga zake.
Mpenzi msomaji, hivi kama mama huyu angetulizana balaa lililompata mwanae lingetokea? Hivi sasa kiranga kimemuisha kwani anashinda pale KCMC kumtunza mwanae ambaye hadi sasa hajitambui.
Kinamama, kwanini hatutulizani tulee watoto wetu? Tatizo kubwa nilionalo kwa mama huyu ni kwamba bado hajatulia kwani starehe ameziweka mbele kuliko malezi ya watoto wake.
Hivi sasa kinamama wa eneo lile la Rau Madukani wamefanya kuwa gumzo suala hilo na kusema kuwa kinamama wengi hasa wenye umri wa kati wamekuwa wakipuuzia sana malezi ya watoto na badala yake kujielekeza kwenye biashara zaidi.
Wengine ndio kama hao wanajitosa kwenye ndoa au wanazaa watoto lakini hawakai chini kuwajengea misingi mizuri ya malezi. Hili ni tatizo ambalo jamii na serikali yafaa ilifanyie kazi katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu.
Mpenzi msomaji, watoto wengi wamekuwa wakirandaranda hovyo mitaani ambako hujifunza tabia mbaya kinyume na maadili ya Taifa letu.
Serikali yafaa ilitizame suala hili kwa macho mawili na kuliwekea msimamo. Sheria ya mtoto ilishaundwa na Sera ya Malezi ya watoto yafaa iwepo kwa ajili ya kudhibiti tabia hizi za wazazi kuacha watoto wakizurura ovyo na kupata ajali zinazoweza kuzuilika.
Taifa haliwezi kusonga mbele kama rika hili(watoto) hawatajengewa misingi imara ya maelezi. Tusipozinduka mapema, tutajikuta tunaelea taifa la manunda yaani watoto magoigoi, watukukutu, mazezeta, mambumbumbu yasiyoweza kufanya lolote.
Tukumbuke tayari vijana wengi wamejiingiza katika maisha hatari ya madawa ya kulevya, wezi na wengine wamekewa mazuzu/ mateja kiasi kwamba hawawezi kutegemewa tena.
Yafaa iwepo mifumo inayotekelezeka katika kuokoa makundi haya muhimu (watoto/vijana) kwa mwendelezo wa taifa hili. Wazazi, walezi, walimu, asasi za kijamii na wengineo ikiwemo serikali waweke nguvu ya pamoja katika kushughulikia uhai wa makundi haya. Maisha Ndivyo Yalivyo.
Mpenzi msomaji, kwa leo nilitaka kukumegea tatizo hilo la watoto kuachwa wakizurura na matokeo yake kupata ajali na kuambulia vilema vya kudumu au kupoteza maisha. Tukutane tena wiki ijayo ambako nitakuletea maoni mbalimbali ya wasomaji wetu kuhusiana na mada tatu zilizopita.
Kama unayo maoni au ushauri tuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi
Namba 0715268581(Usipige) au e-mail fwingia@gmail.com.
1 comment:
Enyi dada zetu na wake zetu mkiisha kuwa mama waoneeni huruma hao viumbe wa Mungu. Hizo starehe na mengineyo yapo kila siku ila maisha ya watoto wenu msiyaweke rehani.
Post a Comment