Advertisements

Sunday, January 20, 2013

Makamanda wa JWTZ walazwa hospitali ya Lugalo

Makamanda na viongozi wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jenerali David Musuguri pamoja na Meja Jenerali Makame Rashid ni wagonjwa na wamelazwa katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam.

Jenerali Musuguri ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama mstaafu aliyetumikia JWTZ wakati wa kipindi cha serikali ya awamu ya kwanza , wakati Meja Jenerali Makame Rashid alikuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati wa awamu ya pili.

Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe alizungumza na NIPASHE Jumapili, juu ya afya za viongozi hao wa jeshi na kueleza kuwa wamelazwa Lugalo.

Alisema awali wakuu hao walikuwa wanafika hospitali na kutibiwa lakini sasa hali zao zinahitaji uangalizi zaidi na wamelazwa hospitalini hapo ingawa hakufafanua kama walilazwa kuanzia lini.

Hata hivyo hakuwa tayari kutaja matatizo yanayowasumbua bali kusisitiza kuwa ni wagonjwa .

Jenerali Musuguri baada ya kustaafu alirejea kijijini nyumbani kwake Butiama, mkoani Mara akijishughulisha na kilimo na ufugaji.

Kwa upande wake Meja Jenerali Makame Rashid alikuwa akijishughulisha na kuhamasisha maendeleo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment:

Anonymous said...

poleni sana makamanda wetu.Mungu atajalia hali itarudia ya kawaida.