KWA wanandoa ni afadhali lakini wapenzi ambao hawajaoana athari yake huwa ni kubwa sana. Inawezekana akajitahidi kutoa lakini utoaji unaendana na uwezo. Akihisi ni mzigo ataona afadhali na mapenzi yafe. Zingatia, kutaka kupewa bila kujiuliza wewe unachangia nini ni mapenzi ya kizamani. Tafadhali sana, usiwe wa kizamani.
Wakati unajiongeza kwamba unashindwa kubadilika kutokana na wakati, tambua kuwa mtindo wako wa kimaisha unakufanya uonekane mzigo mzito kwa mwenzio. Tambua kuwa mzigo huwa haukumbatiwi, kwa kawaida aliyeubeba hutamani kuutua. Akifanikiwa kuutua, hupumua.
Kwa mantiki hiyo, tabia zako zinaweza kumfanya mpenzi wako ajisikie amani siku akiachana na wewe. Na kwa kukuongezea ni kwamba hakuna kitu kibaya kama mwenzi wako aone nafuu ya kuwa bila wewe, hapo ni lazima ujue kuna matatizo ambayo yapo ndani yako.NI ASILI MBAYA
Mtu ambaye anataka apewe zaidi, mara nyingi anakuwa na kasoro za kimaumbile. Huyo anakuwa ni mbinafsi kwa sababu chake kinakuwa ni cha kwake peke yake lakini cha mwenzake anataka kukiwekea sauti. Mara nyingi wanakuwa hatari kwa sababu husumbuliwa na nongwa.
Atataka apewe hata kikiwa hakipo. Anapokosa huhisi kanyimwa. Mtu wa aina hiyo siyo tu kwamba hafai kwenye mapenzi bali hata kwenye maisha ya kawaida kijamii. Hachangii wenzake wanapokuwa wanahitaji michango lakini yeye asipochangiwa ni nongwa.
Mapenzi ni jinsi ambavyo moyo unaridhika, inapotokea mtu anaanza kujiuliza maswali mengi kuhusu mpenzi wake, maana yake anakuwa anamtilia wasiwasi. Pale wasiwasi unapoendelea ndivyo na kiwango cha mapenzi hupungua. Hali hiyo inapozidi, mapenzi hufa kabisa.
Hujawahi kuona watu wanaishi, kila mtu anajua ni wapenzi lakini ndani yao ni kama hakuna kupendana. Yaani wanaishi kwa mazoea tu! Moja ya sababu za wapenzi kufikia hatua hiyo ni mmoja kumuona mwenzake ni mzigo mzito kuubeba.
Tabia hiyo ni sumu hatari kwa maana wapo walioshindwa kupata wenzi wa maisha yao, kwani kila mmoja alimkimbia. Maisha magumu lakini wewe hutaki kutambua hilo, badala yake unataka mahitaji lukuki. Unapaswa kujiuliza wewe umefanya nini?
Angalau basi, kama wewe ni wa kupewa, ufanye juu chini kuhakikisha unapunguza matumizi. Ila wewe ndiye mkali wa kuongeza mahitaji. Ni rahisi kuachwa kwa sababu mtoaji atakapoanza kujiuliza, mwisho wa maswali yake atapata jibu kuwa wewe ni mnyonyaji.
CHUKUA MUONGOZO HUU
Hebu ishi kwa mtindo wa kula na kipofu. Yeye anakupa, sasa kazi kwako kuhakikisha unampa faraja na amani. Ana fedha, wewe huna, kwa hiyo mahitaji yako yanamtegemea yeye, jitahidi kujikomboa ili nawe uwe unaingiza kipato cha kukutosheleza na wakati unapigania hilo, hakikisha unakuwa faraja yake.
Inakuwaje uombe vocha ya simu lakini akikupa, simu unawapigia wengine. Akupigie yeye tu. Nani kakudanganya kwamba yeye ni zezeta wa kiwango hicho? Atakuacha katika kipindi ambacho wewe umetunga kiburi kwenye kichwa chako kuwa hawezi kufurukuta mbele yako.
Ni utani kuamini kuwa hana ujanja mbele yako. Asilimia kubwa walioweka kiburi cha namna hiyo, mwisho walipata shida baada ya kuachwa. Mapenzi hujengwa na vimelea vyake ambavyo ni upendo, heshima na utu. Kama kimoja kati ya hivyo hakuna, hayatafika popote. Yatakufa!
Atakupenda kama nawe unampenda. Anapokuwa anaonesha upendo wa hali ya juu kwako lakini yeye humpi, itafika kipindi atakuona hufai. Ataanza kupunguza, mwisho atachoka kabisa. Hii ndiyo sababu ya kukwambia ‘unapopewa, jiulize nawe unatoa nini’. Zingatia kuwa mapenzi ya upande mmoja ni ya kizamani.
Usitarajie heshima kutoka kwa mwenzi wako ikiwa wewe humheshimu. Namna unavyo mtendea ndivyo unavyokaribisha uhusika wake kwako.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments:
Post a Comment