Leo tunaendelea kuanzia pale tulipokuwa tumeishia lakini kabla sijaenda mbali, niwashukuru marafiki mlionitumia SMS na kutoa maoni yenu juu ya mada yetu. Michango yote mliyoitoa nimeipokea na nawasihi muendelee kuwa nami mpaka mwisho•
KUWA MSIKILIZAJI BADALA YA MZUNGUMZAJI
Kunapotokea mfarakano ndani ya uhusiano wa kimapenzi, jifunze kuwa msikilizaji badala ya mzungumzaji. Wengi hujikuta wanashindwa kupata suluhu hata kwa mambo madogo kwa sababu huwa hawawapi wenzi wao nafasi ya kueleza dukuduku walilonalo ndani ya mioyo yao. Muoneshe kwamba unamjali kwa kumsikiliza kwa makini hata kama anachokizungumza unaona hakina maana. Epuka kuchezea simu wakati mwenzako anazungumza kwani atahisi unamdharau.
JIFUNZE KUZUNGUMZA MAMBO YA MAANA
Ni ukweli ulio wazi kuwa watu wengi huwa hawajui nini cha kuzungumza na wapenzi wao wanapokuwa peke yao, hasa kunapotokea mfarakano. Badala ya kuzungumza kwa namna ambayo itamfanya mpenzi wako aone kwamba umejutia makosa yako, unakuwa mkali, unazungumza kwa amri na kufoka. Hiyo haisaidii chochote bali unaongeza matatizo.
ACHANA NA TABIA ZAKO MBAYA
Kama kilichosababisha umuudhi mpenzi wako ni tabia au mazoea yako mabaya, ni vizuri kuachana nayo kabisa na kumhakikishia kuwa hutarudia. Kama ulimkosea kwa sababu ulikuwa umelewa, basi jidhibiti ili starehe zako zisiwe kero kwa wengine. Kama ulimuudhi mwenzako kwa sababu ya mazoea yako ya kuchelewa kurudi nyumbani, jirekebishe.
USIHAMISHIE HASIRA ZA KAZINI NYUMBANI
Huenda unafanya kazi katika mazingira ambayo yanakufanya ukasirike mara kwa mara kiasi kwamba hata muda wa kurudi nyumbani ukiwadia, unakuwa na kisirani ndani ya moyo wako. Matokeo yake ukifika, unakuwa mkali bila sababu na mwisho unaishia kukwaruzana na mwenzio. Mambo ya kazini yaache kazini na mambo ya nyumbani yaache nyumbani.
MPE ZAWADI MPENZI WAKO
Inashauriwa kuwa endapo umemkosea mpenzi wako, mtafutie zawadi nzuri na kumpa. Haina maana kuwa zawadi hiyo itakuwa ndiyo fidia bali kwa kiasi fulani itamfanya ajue kwamba umetambua kosa lako na unalijutia. Muoneshe kwamba unamjali na hutarudia tena kumuudhi kwa kumpa zawadi mbalimbali kama maua, kadi za ‘Im Sorry’ na vitu vingine vinavyomfurahisha.
MTIMIZIE HAJA ZAKE KIKAMILIFU
Wataalam wa uhusiano wa kimapenzi, wanaeleza kuwa tendo la ndoa lililofanywa kikamilifu ni dawa kubwa inayoweza kuwaunganisha upya wapenzi waliogombana. Jitahidi kumbembeleza akubali kukupa nafasi ya kuwa naye faragha na ukipata nafasi hiyo, mtimizie haja zake kwa kadiri ya uwezo wako wote. Tendo hilo lichochee miili yenu kuzalisha homoni ambazo zitamaliza hasira, chuki na stress ndani ya miili yenu.
WASHIRIKISHENI WATU WALIOWAZIDI
Endapo mbinu zote zilizoelezwa hapo juu zitashindwa kuleta suluhu, siyo vibaya kama mtatafuta ushauri kwa watu wenye busara. Inaweza kuwa ni wazazi wa pande zote mbili (kama mmeoana) au watu wazima waliowazidi umri na wenye busara. Inashauriwa kuwa mbinu hii itumike pale tu inapoonekana suluhu haipatikani kwa urahisi lakini vinginevyo siyo vyema kutoa siri za uhusiano wenu nje.
Ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment