ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 10, 2013

Polisi mbaroni kwa kusindikiza mihadarati


Askari wawili wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Bunda mkoani Mara, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.

Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi, alisema kuwa watuhumiwa hao walitiwa mbaroni juzi saa 7:30 mchana katika kizuizi cha jeshi hilo kilichopo katika eneo la Wilaya ya Busega, karibu na mji mdogo wa Lamadi, kwenye barabara kuu ya Mwanza-Musoma.


Msangi alisema watuhumiwa hao, askari mwenye namba E. 4640 Koplo Daniel na E. 6224 Koplo Mwinyihaji  walikamatwa wakiwa na mirungi yenye uzito wa kilo 72 iliyokuwa imewekwa kwenye mabegi mawili.

Alisema kuwa askari hao walikuwa na gari binafsi aina ya Toyota Noah, na kwamba walikuwa na wanawake wawili, Achien Aoko (30) na Penina Samson (20),  wakazi wa wilayani Tarime.

Alisema kuwa baada ya askari hao ambao walikuwa wamevaa kiraia kufika katika kizuizi hicho, gari lao lilipekuliwa na askari wenzao, na ndipo ilipogundulika kuwa kulikuwa na mabegi mawili ya mirungi.
Alisema kuwa askari hao wamefunguliwa mashitaka ya kijeshi.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, wanawake waliokuwa na askari hao jana walifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi kwa sasa inatumika kama Mahakama ya Mkoa wa Simiyu.

Alisema kuwa upelelezi kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea na kuongeza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa askari hao waliokuwa na silaha, pia walivuka mkoa mwingine bila ya kufuata taratibu za jeshi hilo.

“Lakini hata kama wakisema walikuwa kazini, upelelezi wetu wa awali unaonyesha kwamba hawakufuata utaratibu, kwani unapovuka wilaya au mkoa mwingine, lazima ufuate taratibu za serikali,” alisema   Msangi.

Vyanzo vya habari ndani ya Jeshi Polisi vinaeleza kuwa askari hao walikuwa wakisindikiza mirungi hiyo ambayo ilikuwa ni mali ya baadhi ya watu.

“Kwani ni leo tu mbona tabia hiyo wanaifanya kila siku, lakini za mwizi ni arobaini na leo wamepatikana,” kilieleza chanzo kimoja.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya kutokea tukio jingine mkoani Mara, ambako  polisi wawili kutoka mkoani Kagera walikamatwa wakituhumiwa kuwa na nyara za serikali.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Absalom Mwakyoma, alisema kuwa hata kama askari hao wakijitetea kwamba walikuwa kazini, lakini kazi ina taratibu zake.
Mwakyoma alisema kuwa miongoni mwa taratibu hizo ni matumizi mazuri ya muda.

“Siku zote na kwa saa zote askari lakini lazima ufuate taratibu na kutokutumia saa ya kazi vibaya, pia lazima taratibu zifuatwe,” alisema Kamanda Mwakyoma.

Alisema hata kama askari akiwa kazini, lazima aheshimu sheria za nchi kwa kutokufanya uhalifu wa aina yoyote kwa sababu yeye kama mlinzi wa raia na mali zao, ndiye anayetakiwa kuwa mfano mzuri ndani ya jamii.
CHANZO: NIPASHE

No comments: