Saturday, February 2, 2013

ARVs zatishia maisha ya wenye Ukimwi

Baadhi ya waathirika wa virusi vya Ukimwi (VVU), wamelalamika kuwa licha ya kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi (ARV), zimeendelea kuwaongezea matatizo ya magonjwa nyemelezi.

Wametaja magonjwa nyemelezi yanayowakabili kuwa ni pamoja na kuharibika figo, mfumo wa uzazi, kuwa na unene lakini miili hubakia na uzito hafifu pia kuharibika mapafu pamoja na kutokwa na usaha au uchafu mwingi sehemu za siri.

Wakizungumza kwa sharti la kutokutajwa majina yao waliiomba serikali kuzichunguza dawa hizo kwa makini ili kuepusha kuwaongezea madhara yanayowakabili.

Katika mahojiano yao na NIPASHE yaliyofanyika jijini Dar es Salaam waathirika hao walisema wengi wao wanajikuta wakiendelea kutumia ARVs wakati wanaendelea kukabiliwa na magonjwa nyemelezi zaidi. Walisema licha ya kunufaika na huduma ya dawa hizo wengi wao wanakabiliwa na magonjwa lukuki.

“Mtu anatembea lakini afya yake haiko sawa, mfano mwili kujaa nyama wakati uzito wake ni hafifu hilo ni tatizo, jambo la kushangaza pindi tunapokwenda katika vituo vyetu vya afya unaweza kubadilishiwa dawa na daktari au mshauri kulingana na tatizo lenyewe.

“Lakini muda mfupi ukiwa katika tiba, tatizo jingine linajitokeza, tena kubwa zaidi kutokana na hili tunaiomba serikali itusaidie” alisema mwathirika.

Mkuu wa Kitengo cha Ushauri wa Upimaji VVU cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Salama Lembariti alilitaka kundi hilo kufuata ushauri wa daktari hususani katika vituo wanavyopatiwa huduma za ARVs kwa ajili ya uchunguzi na kubadilishiwa tiba.

CHANZO: NIPASHE

No comments: