Saturday, February 2, 2013

Morocco, Ivory Coast zamtisha Poulsen

KOCHA wa timu ya Taifa, Kim Poulsen, amesema anajukumu zito, kuhakikisha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inafanya vizuri, pindi itakapocheza na timu ya Morroco na Ivory Coast katika mechi za mchujo wa Kombe la Dunia.

Kauli hiyo ya Poulsen imekuja baada ya Kocha huyo kurejea, akitokea Afrika Kusini ambako alikwenda kuziangalia, ni wazi kocha huyo anazihofia.

Akizungumza jijini jana, kocha huyo ambaye alirejea nchini juzi akitokea Afrika Kusini, alisema ameweza kufuatilia mechi tatu ambazo timu ya Morocco ilizicheza, na kuona jinsi gani timu hiyo ilivyo na kiwango cha hali ya juu.Poulsen alisema wachezaji wa Morroco wameonyesha nidhamu ya hali ya juu ya mchezo, jambo ambalo amejifunza na inamlazimu kuhakikisha Taifa Stars inafuata nyayo hizo.

“Nimeweza kuona mechi tatu ambazo timu ya Morroco ilicheza, upande wa Ivory Coast nimeangalia mchezo wao mmoja tu, lakini kati ya timu hizi mbili Morroco wanakiwango cha juu zaidi,” alisema Poulsen.

Katika hatua nyingine kocha huyo alisema, anatarajia kuendesha kambi ya muda mfupi, kwa wachezaji ambao hawachezi Ligi Kuu, ili kuhakikisha anapata hazina ya wachezaji.

Kocha huyo alisema kambi hiyo amepanga ifanyike Aprili, kwani itamsaidia kutengeneza wachezaji wazuri ambao Taifa litawategemea katika mechi mbalimbali, kwani tayari wachezaji waliopo katika timu hiyo anawafahamu vizuri.

Ivory Coast imefuzu katika hatua ya robo fainali za Afrika, huku Morocco imeaga mashindano hayo.

No comments: