Advertisements

Tuesday, February 19, 2013

Asilimia 60 chali matokeo ya kidato cha nne

Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa 

MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yametangazwa. Watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.

Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa alisema watahiniwa walikuwa 456,137, wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea wakiwa 68,806.
“Matokeo ya mwaka huu yamekuwa mabaya sana, Serikali tunasikitika kutokana na hali hii lakini tuna mipango mbalimbali ya kuhakikisha tunaweza kutatua hili tatizo,” alisema Dk Kawambwa.

Dk Kawambwa alisema watahiniwa wote kwa ujumla waliosajiliwa walikuwa 480,036 kati yao wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67 lakini waliofanya mtihani huo ni 456,137 sawa na asilimia 95.44, wengine 21,820 (asilimia 4.55) hawakufanya mtihani.

Alisema watahiniwa wa shule (school candidates) walikuwa 397,136 sawa na asilimia 96.57, miongoni mwao, 14,090 sawa na asilimia 3.43 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo utoro, ugonjwa na vifo.

Ufaulu kwa madaraja
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.

Waliopata daraja la tatu ni 15,426, wavulana 10,813 na wasichana 4,613, waliopata wa daraja la nne 103,327, wavulana 64,344 na wasichana 38,983 huku waliopata sifuri wakiwa 240,903, wavulana 120,664 na wasichana 120,239.

Shule 20 bora
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wizara ilitaja shule 20 zilizofanya vizuri badala ya 10 kama ilivyozoeleka, kati yake 18 zilikuwa za watu binafsi na mashirika ya dini na mbili za Serikali.

Shule hizo ni pamoja na St.Francis Girls ya Mbeya, Marian Boys ya Pwani, Feza Boys ya Dar es Salaam, Marian Girls ya Pwani, Rosmini ya Tanga, Canossa ya Dar es Salaam, Jude Moshono ya Arusha, St. Mar’s Mazinde Juu ya Tanga, Anwarite Girls ya Kilimanjaro na Kifungilo Girls ya Tanga.

Nyingine ni Feza Girls ya Dar es Salaam, Kandoro Sayansi Girls ya Kilimanjaro, Don Bosco Seminary ya Iringa, St. Joseph Millenium ya Dar es Salaam, St. Iterambogo ya Kigoma, St. James Seminary ya Kilimanjaro, Mzumbe ya Morogoro, Kibaha ya Pwani, Nyegezi Seminary ya Mwanza na Tengeru Boys ya Arusha.

Shule 10 za Mwisho
Kwa upande wa shule 10 za mwisho, iliyofanya vibaya zaidi ni Mibuyuni ya Lindi, Ndame ya Unguja, Namndimkongo ya Pwani, Chitekete ya Mtwara, Maendeleo ya Dar es Salaam, Kwamndolwa Tanga, Ungulu Morogoro, Kikale ya Pwani, Mkumba na Tongoni za Tanga.

Matokeo yaliyofutwa
Jumla ya watahiniwa 789 wamefutiwa matokeo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na udanganyifu na kuandika matusi.

Baadhi ya udanganyifu huo ni karatasi za majibu kuwa na mfanano usio wa kawaida, kukamatwa na simu za mkononi kwenye chumba cha mtihani, kukutwa na karatasi au madaftari pamoja na kubadilishana karatasi za majibu.

Dk Kawambwa alisema matokeo ya watahiniwa 28,582 yamezuiwa kwa sababu ya kutolipa ada ya mtihani na wanatakiwa kulipa fedha hizo ndani ya mwaka mmoja.

Matokeo ya QT
Dk Kawambwa alisema waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Maarifa (QT) walikuwa 21,310, wasichana 13,134 na wavulana 8,176 na waliofanya ni 17,137 sawa na asilimia 80.42... “Watahiniwa 5,984 kati ya 17,132 waliofanya mtihani huo wamefaulu.”
Waziri akwepa
Kabla ya kutangaza matokeo hayo, Waziri Kawambwa alitumia muda mwingi kuzungumza sababu za yeye mwenyewe kuamua kutangaza matokeo hayo badala ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Mirihani la Taifa (Necta), Dk Joyce Ndalichako kama ilivyozoeleka.

“Najua kila mtu ana shauku ya kusikia matokeo leo, naona mkimwangalia Katibu (Dk Ndalichako) hapa, lakini mimi kwa kujua jambo hili, nimeona kwa nini nimbebeshe jukumu hilo zito wakati waziri mwenyewe mwenye dhamana hiyo nipo! Ndiyo nimekuja niwape matokeo haya,” alisema Dk Kawambwa.

Baadaye Dk Kawambwa aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa na haraka hivyo asingekuwa na muda wa kujibu maswali, huku akitumia muda mwingi kuzungumza mambo yaliyokuwa nje ya matokeo aliyotarajiwa kuyasoma.

Pia alikwepa kujibu maswali ya msingi likiwamo kutaja majina ya wanafunzi bora pamoja na majina ya shule 10 bora zenye wanafunzi chini ya 40 akisema anajua umuhimu wa kueleza mambo hayo, lakini wataalamu wake wamekwepa kuandika kila kitu katika taarifa hiyo kwa kile alichoeleza kukwepa kuwa na taarifa ndefu. Taarifa iliyosomwa na waziri kwa waandishi ilikuwa na karatasi nne.

Ufaulu mwaka 2011
Kwa mujibu wa matokeo ya mwaka 2011, ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule ulionyesha kuwa watahiniwa 33,577 sawa na asilimia 9.98 walifaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu. Wasichana waliofaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 10,313 sawa na asilimia 7.13 na wavulana 23,267, sawa na asilimia 12.13.

Waliopata daraja la nne mwaka huo walikuwa 146,639 sawa na asilimia 43.60. Wavulana 87,039 sawa na asilimia 45.40 na wasichana 59,600, sawa na asilimia 41.22 huku waliofeli wakiwa 156,089 sawa na asilimia 46.41, kati yao wavulana wakiwa 81,418 sawa na asilimia 42.47 na wasichana 74,667, sawa na asilimia 51.64.
Mwananchi

5 comments:

Anonymous said...

MATOKEO YA MITIHANI KIDATO CHA NNE YANADHIHIRISHA JINSI HALI YA NCHI INAVYOZIDI KUWA MBAYA. HIYO ASILIMIA 60 WALIOPATA DIVISION 0 SIYO SUALA LA BAHATI MBAYA AU KUWA WALIMU NA UONGOZI MZIMA WA WIZARA HAWAKUFAHAMU KUWA MATOKEO YATAKUWA HIVYO. KWA SAS NCHI INAKWENDA KANA KWAMBA HAKUNA UONGOZI NA NDIYO MAANA TUNAFIKIA HAPA.HALI ZA WATANZANIA ZINAZIDI KUWA MBAYA SIKU HADI SIKU NA VIONGOZI WETU WANADIRIKI KUSEMA WATANZANIA WANA HALI NZURI KWA KUWAANGALIA TABAKA LA WA WACHACHE.ANGALIA UGOMVI WA KIDINI HADI KUFIKIA MAUAJI HUKO MUSOMA NA ZANZIBAR. VIONGOZI WANAFANYA LIPI LA MAANA KUZUIA MACHAFUKO HAYO. TANZANIA IMEKUWA SUALA NI "SURVIVAL OF THE FITTEST" UKIPATA WADHIFA JINUFAISHE NA WATU WAKIHOJI INASEMEKANA WANA WIVU. TUMKUMBUKE BABA WA TAIFA HADI ANATOKA MADARAKANI HAKUWA NA MALI WALA UTAJIRI. SASA ANGALA VIONGOZI WETU JINSI WALIVYOJINEEMESHA. NANI ATAMLINDA MTANZANIA WA KAWAIDA? NANI ATAJALI SUALA ZIMA LA ELIMU KWA KIZAZI HIKI NA KIJACHO???ANGALIA HATA TAARIFA YA WAZIRI KUHUSU MATOKEO JINSI ILIVYOANDALIWA NA MAPUNGUFU ETI KWA "KUFUPISHA TAARIFA" NA UHARAKA ALIOKUWA NAO WAZIRI AKIKWEPA MASWALI YA WAANDISHI. JE HILI HALIKUWA NA UMUHIMU SANA KWA SASA? KWA NCHI ZA WENZETU ALIPASWA KUJIUZURU MAANA HII NI AIBU KWA WAZIRI NA TAIFA KWA UJUMLA.... EEH MUNGU ITAZAME KWA JICHO LA HURUMA NCHI YETU TANZANIA

Anonymous said...


I fully agree with the above comments. Ni lini wapiga kura wa TZ watafanya uamuzi wa kuleta mabadiliko. Uongozi wa chama tawala umeshindwa. It's time for change!

Anonymous said...

Hivi huyu waziri haoni kama anajizalilisha maana yote yanaanzia kwake inabidi atoke ofisini atembelee mashule kufuatilia nini hasa kitendeke kusadia wanafunzi kuwa katika kiwango kizuri ili waweze kukabiliana na mitihani maana hii ni aibu

Anonymous said...

I visited an elementary school in a village in Tanzania early last month. The first grade teacher had 73 children (plus 3 missing on that day). The kids were sitting 4-5 at a desk. The teacher was so overwhelmed, she resorted to chalk and talk teaching method- no interaction with the children. Mind you, these children attended kindergarten the previous year but none of them could even write his/her name. If you begin formal schooling in this mode, very likely you will end up on the FAIL list.

Anonymous said...

NDUGU WAZIRI,KUFELI KWA WANAFUNZI AMBAKO KUMEVUNJA REKODI KTK TAIFA LETU NI KUSHINDWA KWA UONGOZI NDANI YA WIZARA YAKO. SASA BAATHI YA WANAFUNZI WAMEAMUA KUJINYONGA, UNAHITAJI MALAIKA GANI AJE AKUAMBIE UJIUZULU??? WAKATI NI HUU CHUKUA UAMUZI WA BUSARA MH. KAWAMBWA.
I was just saying!!!!