MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imesitisha zoezi la utoaji wa vitambulisho kwa wananchi mpaka pale zoezi la kuhakiki taarifa zilizosajiliwa litakapokamilika.
Mamlaka hiyo inajipanga kutoa vitambulisho hivyo kwa watu wa kada mbalimbali ambavyo vitakuwa ni vya aina tatu ikiwa ni pamoja kwa raia, wakimbizi na wageni wakazi.
“Tulianza na viongozi wa Serikali kwa awamu ya kwanza na baada ya hapo tutafuata na watumishi wa serikali wa Dar es Salaam pamoja na Zanzibar. Tuliazimia kuwafikia watumishi wapatao 500,000 na mpaka sasa tumewaandikisha zaidi ya robo tatu na hao wachache waliobaki ni kutokana na kutokuwapo ofisini kwa sababu mbalimbali,” alisema William.
Kuhusu wananchi wa Dar es Salaam na Zanzibar ambao walitakiwa kujiandikisha kwa ajili ya vitambulisho hivyo mwishoni mwa mwaka jana, William alisema kuwa watafuata baada ya watumishi wa Serikali ambao taarifa zao zimekamilika.
“Tunaandaa mpango maalumu ili kuwezesha zoezi la uhakiki wa taarifa pamoja na kuchukua alama za vidole na saini za watu wote waliosajiliwa na kustahili kupata vitambulisho hivyo na hii tutaifanya mtaa kwa mtaa ili kupunguza msongamano wa watu kama ilivyotokea wakati wa kujisajili,” alieleza William.
Mamlaka hiyo inatarajia kukamilisha zoezi hilo kabla ya uchaguzi mkuu ujao na kuwa itafungua ofisi katika kila wilaya ili kuwezesha watu kurekebisha taarifa zao kila itakapobidi kwa kuwa vitambulisho hivyo vitakuwa vinakwisha muda wake kila baada ya miaka kumi.
“Tutakuwa tumetoa vitambulisho kwa watu zaidi ya 26 milioni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 wenye umri zaidi ya miaka 18” alifafanua William.
William aliwatoa wasiwasi Watanzania walio nje ya nchi kwa sababu mbalimbali kwa kusema kuwa watapata vitambulisho vyao kwa kufuata utaratibu kama watu wengine walivyofanya.
“Kwa wale walio nje ya nchi kwa sababu zozote iwe masomoni au kazi, watatakiwa kufuata utaratibu wa kawaida kwa kujaza fomu pindi warejeapo hapa nchini katika ofisi zetu zitakazokuwepo katika wilaya zote katika kila mkoa” alisema William.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment