ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 19, 2013

Mauaji wa Padri yameitia doa Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitoa kauli nzito ya Serikali kuhusiana na mauwaji ya Padre Evarist Mushi wa kanisa katoliki Zanzibar, wakati akifungua semina ya madiwani wa CUF kisiwani Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amelaani vikali kitendo kwa kupigwa risasi na kuuliwa kwa Padre Evarist Mushi wa kanisa katoliki Zanzibar. Amesema kitendo hicho kimevuruga sifa njema ya Zanzibar ya kuwa kisiwa cha amani.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF ametoa kauli hiyo kisiwani Pemba wakati akifungua semina ya madiwani wa CUF inayofanyika ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi. Amesema kwa niaba yake binafsi, chama chake na Serikali analaani vikali kitendo hicho cha kinyama ambacho kimeitia doa kubwa Zanzibar.
Amesema kitendo hicho ambacho hakikubaliki ni cha kusikitisha kwa vile Wazanzibari wamekuwa wakiishi kwa kuvuliana kwa kipindi kirefu bila ya kutoa vitendo hivyo. Amesema ni wajibu wa Wazanzibari kuendeleza sifa njema ya Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuishi kwa kuvuliana na kuwapa matumaini wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kwa shughuli mbali mbali ikiwemo ya utalii.
Ameviomba vyombo vya dola kufanya kazi ya ziada kuwatafuta waliohusika na tukio hilo na kuchukuliwa hatua za kisheria. Hata hivyo amesema wakati uchunguzi huo ukiendelea kufanyika, ni vyema kwa vyombo vya dola kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuepuka kuwahusisha watu wasiohusika na tukio hilo.
Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea kusikitishwa kwake na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa kitendo hicho ni cha kigaidi. Amekiri kuwa kitendo hicho ni kikubwa na kibaya, lakini hakijafikia hatua ya kuitangaza Zanzibar kuwa nchi ya kigaidi, na kwamba kufanya hivyo ni kuijengea sifa mbaya Zanzibar.
“Kauli kama hizi ukweli hazisaidii zaidi ya kutuvuruga, ni kweli ni kitendo kibaya na kikubwa, lakini ugaidi ni mkubwa zaidi na sisi hatujafikia na wala hatutofikia hatua hiyo”, alionya Maalim Seif. Amesema ni vyema kwa viongozi wanaotokea upande wa pili wa Muungano kufanya mashauriano na viongozi wa Zanzibar kabla ya kutoa kauli ambazo zinaijengea sifa mbaya na kuitia doa Zanzibar.
Wakati huo huo Maalim Seif amesema ni lazima maamuzi ya madiwani yaheshimiwe na watendaji wengine katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao. Amesema madiwani ndio wafanya maamuzi katika Serikali ya mitaa,hivyo maamuzi yao yaheshimiwe na watendaji ili kujenga mustakbali mwema katika kuwatumikia wananchi.
Amefahamisha kuwa tatizo lililopo sasa ni kuwa mfumo uliopo unatoa mamlaka makubwa kwa watendaji, hasa makatibu wa Halmashauri na  Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa. Amesema wakati Serikali imo katika mchakato wa kuleta mageuzi  katika Serikali za Mitaa Zanzibar, ni vyema mageuzi hayo yakarekebisha hali isiyoridhisha iliyopo sasa.
Ametoa wito kwa Madiwani  kuchapa kazi kwa bidii, na kuhakikisha wanayafahamu, kuyasimamia na kuyatekeleza ipasavyo majukumu waliyokabidhiwa.
Aidha Maalim Seif amewasihi Madiwani wa CUF kutokubali kuburuzwa na watendaji, na kuhakikisha kuwa maamuzi yao katika Mabaraza na Halmashauri yanaheshimiwa na kutekelezwa kwa ukamilifu.
“Lazima mujue matumizi ya kila senti moja. Lazima muhakikishe kuwa hakuna upendeleo katika ugawaji wa rasilimali kwa Shehia zilizomo katika Halmashauri au Baraza”, alisema Maalim Seif na kuongeza,
“Endapo Katibu au Mtendaji hafuati maagizo ya Madiwani na anafanya atakavyo, lazima mumuarifu Waziri anayehusika, na kama Waziri atapuuza wasilisheni ripoti kwa Makamu wa Pili wa Rais”,
Amefahamisha kuwa ili malengo ya utekelezaji yaweze kufikiwa ni vyema kwa madiwani kufanya kazi bega kwa bega na watendaji wengine wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Masheha, kwa vile kazi na maeneo yao ya kazi yanalingana.
Jumla ya madiwani 83 wa CUF kutoka Pemba na Unguja wanashiriki semina hiyo ya siku 6 ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji madiwani, inayofadhiliwa na Taasisi ya Friedrich Naumann Foundation (FNF) ya Ujerumani.

No comments: