ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 19, 2013

BARUA YANGU KWA NDUGU ZANGU WA BUSERESERE NA WATANZANIA WOTE


Majeruhi Sadick Yahaya akiwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Geita baada ya kujeruhiwa wakati wa vurugu za waislam na wakristu wachache zilizotokea katika kijiji cha Buseresere wilayani Chato mkoani Geita na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama.


TUMSIFU Yesu Kristo,
Asalam Aleiykum,
Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mungu, kwa nafasi ya kipekee ya kuwa hai tena katika nchi iliyopendelewa naye; Tanzania. Nikiishi na Watanzania, watu wenye sifa ya upole na uvumilivu tofauti na mabilioni ya watu wengine kutoka pande mbalimbali za dunia.
Ndugu zangu wa Buseresere na Watanzani wote, naandika barua hii ya leo moyo wangu ukiwa umepondeka, umejawa na huzuni nyingi mno pia hofu inayosababishwa na kutoelewa kitakachotupata mimi, familia yangu, nchi yangu nanyi Watanzania wenzangu, miaka michache ijayo kama mambo yataendelea kwenda kama yanavyokwenda.
Kila mmoja wetu anafahamu kwa miaka mingi pamoja na tofauti tulizonazo, ziwe za dini, rangi, kabila, hali ya uchumi, bado tumeishi pamoja kama ndugu, marafiki, wapendwa na tunaopendana kupita kiasi, tangu kuumbwa kwa dunia. Nchi yetu Tanzania haijawahi hata siku moja kushuhudia mambo ambayo yametokea huko Buseresere, Geita wiki moja iliyopita tangu kuwepo kwake.
Tukatae tukubali, damu imemwagika! Damu ya Watanzania ambao siku zote wameishi kama ndugu imemwagika, wamechinjana! Sababu ya tofauti zao, tena tofauti ya imani zao za dini. Hili ndilo jambo ambalo limenisikitisha kupita kiasi, kwani hata siku moja katika maisha yangu sikuwahi kuwaza kwamba nchi hii, ambayo wazazi wetu wa mwanzo walitengeneza misingi imara ya watu kupendana na kuishi kama ndugu, ingemwaga damu kwa sababu ya tofauti za dini.
Tanzania, nchi ya kidemokrasia, ambapo watu wana uhuru wa kuabudu watakavyo, bila kubughudhiwa au kubughudhi wengine, damu imemwagika! Tofauti za imani, zimefanya watu ambao ni ndugu wamechukua mapanga, wakakatana, kujeruhiana mpaka Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Mtumishi wa Mungu, Mathayo Kachila (48) akauawa kinyama. INASIKITISHA.
Hebu tuchukue dakika moja, kumfikiria mchungaji huyu, aliyeelekea eneo la machafuko lengo lake likiwa ni kutafuta suluhu, bila silaha yoyote mkononi mwake zaidi ya Biblia na kuuliza kulikuwa na nini kigumu kilichokuwa kimetokea mpaka watu wawe na mapanga mkononi? Badala ya kujibiwa alivamiwa na kuanza kukatwakatwa kwa mapanga, damu nyingi zikamvuja na akafa akiwa njiani kupelekwa hospitali!
Hili ni jambo la kusikitisha sana, moyoni mwangu naamini mtu huyu atakuwa upande wa kuume wa Mungu baba, kwa sababu hakufa akizini nje ya ndoa, akiiba au akitenda dhambi yoyote kinyume na matakwa ya Mungu, bali alikufa akimtumikia muumba wake.
Ndugu zake hawana sababu ya kulia sana, kazi yake imekamilika na Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi na awasamehe watu wote waliomkata kwa mapanga na kumuua.
Ndugu zangu;
Hii ndiyo Tanzania ya sasa, tumeanza kushuhudia chuki baina ya ndugu na ndugu ambapo huko nyuma hatukuwahi kuiona wala kudhani ingetokea! Hakika ni lazima tukubali kwamba sasa kama nchi tunalo tatizo, tusikae kimya, bali kwa haraka sana tuanze kulishughulikia kabla hatujatokomea mbali zaidi ambako mauaji yatakuwa makubwa na tutaiacha nchi yetu vipandevipande, tukiwa tumepoteza maisha ya watu wengi kwa sababu tu, hatukuambiana ukweli na kuonyana.
Kwa miaka yote tumeishi na amani, inawezekana tumeanza kukidharau kitu hiki cha thamani na kuona hakina maana, hivyo kutamani maisha mengine ya kutangatanga! Ndugu zangu, umuhimu wa kitu huonekana wakati hakipo, hakuna mtu anayejua umuhimu wa makalio mpaka siku moja akiambiwa “kalia kichwa.”
Yawezekana kuna watu wameanza kutamani vurugu, mauaji, wakidhani kwa kufanya hivyo watakuwa wanatafuta maisha bora zaidi, jambo ambalo si kweli. Mbele kuna majuto.
Ndugu zangu wa Buseresere,
Najua baadhi yenu mtakuwa mnanikumbuka vizuri kwani niliishi nanyi sana miaka ile nikiwa machimboni Mgusu, Lwamgasa, Nyakagwe na Nyarugusu! Mkimuuliza rafiki yangu aitwaye Lubambe, atawaeleza vizuri historia yangu na maeneo hayo. Hivi kweli ninyi ndugu zangu wapole na wakarimu, mmechagua kuwa watu wa kwanza katika nchi hii kuweka historia ya kuchinjana sababu ya tofauti za dini? Siamini.
Kwa nini nasema siamini? Nasema hivyo kwa sababu nawajua, ni watu wapole, wavumilivu na mna sifa zote za Kitanzania, iweje leo mchukue hatua hiyo ya kumuua Mtanzania mwenzenu sababu ya imani ya dini? Jambo hili limenisikitisha sana, nina kila sababu ya kuwaomba, msirudie tena kutenda kosa hilo siku nyingine, sababu kuua mtu ni dhambi.
Haya si maneno yangu, kwani hata vitabu vitakatifu vya Mungu vimekataza kuua na siku zote vimetusisitizia kutenda mema, hivyo ndivyo Quran inavyosema katika sura ya 60: 8; Mungu hawazuii (Waislam) kuonyesha wema na kuwatendea haki wale ambao hawajawapiga kwa sababu ya dini yenu, au kuwaondoa kwenye nyumba zenu. Mungu anawapenda watenda haki.
Maandiko haya ya Mungu yanawakumbusha Waislam kutenda mema kwa watu wote, hata wakati wa vita, Mtume Muhammad (S.A.W) aliwazuia askari kuua wanawake, watoto, wazee na watu wasio na hatia, hili ndilo jambo ambalo tunatakiwa kutendeana sisi kama wanadamu katika nchi tuliyopewa na Mungu tuishi pamoja ingawa tuna tofauti zetu, si za dini tu, bali za rangi, kabila, siasa, uwezo wa kiuchumi nk.
Wakristo pia katika kitabu cha Waebrania 12:14-15, wameandikiwa, naomba ninukuu; Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na utakatitu ambao bila kuwa nao, hakuna mtu atayemwona Bwana. Angalieni sana mtu yeyote asishindwe kupata neema ya Mungu, na muwe waangalifu pasizuke chuki ambayo kama mmea wenye sumu, inaweza kukua ikaleta matatizo na kuwachafua wengi.
Haya ndiyo maagizo ya Mungu ambaye sisi sote (Wakristo na Waislam) tunamwabudu. Hivi nani kati yetu asiyejua kwamba sisi sote asili yetu, shina letu ni kwa Adam na Hawa? Sasa kwa nini tuchinjane? Kwa nini tupigane? Wakati ni watoto wa familia moja? Hivi unapomuua mwenzako sababu ya imani ni pepo gani unayoitafuta?
Naambiwa chanzo cha mauaji haya ni bucha za nyama, Waislam wanaamini mnyama ni lazima achinjwe na Muislam ndiyo apate kuliwa, tofauti na hapo ni haramu! Wakristo nao wanasema si lazima mnyama achinjwe na Muislam, kwa sababu haijaagiza hivyo kwenye kitabu chao (Biblia) hivyo hawana sababu ya kusubiri mpaka Muislam achinje ndiyo wapate kula.
Hii ni moja kati ya tofauti zilizopo kati ya imani hizi mbili, bahati mbaya sana ni maagizo ambayo huwezi kuyabadilisha, ingekuwa ni katiba tungekaa chini na kutoa mapendekezo mapya, lakini maagizo haya ni ya Mungu kupitia kwa Mitume wake ambao leo hii wote hawapo pamoja nasi tena! Tuliachwa sisi kutekeleza maagizo haya na ni lazima sote tuyafuate kama ambavyo vitabu vya Mungu (Quran na Biblia) vinavyoagiza ili tupate sifa ya kuirithi mbingu.
Swali ninalojiuliza ni hili, kama tofauti hizi zimekuwepo kwa miaka yote, kwa nini tuchinjane mwaka 2013? Tena tukio hili baya litokee Buseresere? Tumeshindwa nini kuishi kama ambavyo mababu zetu, wazazi wetu waliishi na wakawa na amani ambayo waliturithisha sisi? Mungu mwenyewe aliyetuumba anajua tunazo tofauti na katika Quran sura ya 5: 48, amesema yeye ndiye aliyeumba mataifa tofauti na watu wenye imani tofauti ili kwamba wanadamu wapate kushindana katika kutenda mema na hatimaye waweze kumkaribia yeye.
Mungu hakuziweka tofauti hizi ili kwamba sisi tupate kuzitumia kuchinjana! Bali tuzitumie kumpendeza yeye, sasa swali ninalojiuliza ni kwa nini tunachinjana? Tunataka kumfurahisha nani? Ndugu zangu, yatupasa kujiuliza mara mbili kabla ya kuchukua panga na kumkata mwenzako.
Ndugu zangu Watanzania na wananchi wa Buseresere,
Mbuyu ulianza kama mchicha! Tusidanganyane kwamba mbegu hii ya chuki itakwisha hivihivi, inazidi kusambaa, ilitokea Buseresere, Geita, ikahamia Nyehunge wilayani Sengerema na sasa nasikia imeanza kunukia tena maeneo ya Kanyara, katika wilaya hiyohiyo ya Sengerema mkoani Mwanza. Hali hii inazidi kusambaa! Hatupaswi kukaa kimya au kuacha liishe lenyewe, lazima hatua zichukuliwe, nampongeza Waziri wa Mambo ya Ndani Dk Emmanuel Nchimbi kwa uamuzi wake wa kusafiri mpaka Buseresere kwenda kutafuta suluhisho.
Tusipochukua hatua, tutashtukia limeshaingia Kigoma, maana Waislam na Wakristo wapo kila mahali katika nchi yetu, ipo siku linaweza kuifunika kabisa nchi yetu ya Tanzania na kusababisha mauaji makubwa yanayosababishwa na chuki tu dhidi ya binadamu mwenzako.
Wakristo kwa Waislam nawasihi, niko chini ya miguu yenu, mikono yangu yote miwili nimekusanya mbele nikiwaomba tusiingize nchi yetu kwenye janga la aina hii ambalo ni vigumu sana kuliondoa likishatokea, bali jukumu letu ni kuchipusha upya moyo wa kupenda ndugu zetu bila kujali tofauti tulizonazo za kiimani, siku zote tufahamu sisi ni ndugu hata kama tunaabudu katika imani tofauti, Utanzania wetu uko pale pale.
Kamwe hatuhitaji kuivuruga nchi yetu, hakuna aliyefaidika na vurugu za aina hiyo, Nigeria mpaka leo bado wanasumbuka, maisha ya watu wengi yamekwishapotea sababu ya mapambano kati ya Wakristo na Waislam! Je, nasi tunataka kuelekea huko? Kipi kimetushinda? Hivi ni kweli tumeshindwa kutumia hekima ambazo Mungu alitupa na kuishi pamoja sababu ya suala ya kuchinja?

Barua hii ya Shigongo kwa wakazi wa Buseresere na Watanzania wote, itaendelea wiki ijayo.

2 comments:

Anonymous said...

Mr shigongo.
Kwanza kabisa waislamu na wakristo hawaabudu mungu mmoja,
Allah anakataa yesu hakufa msalabani
Allah anakataa utatu mtakatifu
Allah anakataa yesu si mwana wa mungu
Allah anachukia waisraeli
Kama tunaabudu mungu mmoja je tunaweza sema hivi. " hakuna mungu ila Jehova na Ezekiel ni mtume wake? kama hatuwezi kusema hivi, basi hatuabudu mungu mmoja na haiwezekani allah akawa Jehova kwa sababu allah anawachukia sana wana wa israeli wakati JEHOVA wana wa israeli ndo anawapenda saaaana na akawachagua kuwa taifa lake.

Anonymous said...

Wewe uliyemjibu Shigongo sidhani kama una uelewa mkubwa. Unavyosema kuwa wakristo na waislaam hawaabudu Mungu mmoja una maana gani? je umeshamuona huyo Mungu unayemuabudu wewe? unasema 'allah' lakini huelewi kuwa hilo ni neno la kiarabu ambalo tafsiri yake ina maana ya Mungu kwa kiswahili! Unasema allah anachukia waisraeli hivi una uhakika na unalosema au ni propaganda uliyoelezwa na sheikh wao wa msikiti ambaye alikimbia shule? Pili nani kakwambia kuwa waisraeli ni wakristo? ina maana umeshindwa kutofautisha uyahudi na ukristo? Nakueleza tu hivyo ni vitu viwili tofauti, uyahudi una tofauti sana na ukristo, una ukaribu sana na uislaam kwa sababu wote mnatumia vitabu vya kale na hata usalishaji wenu unafanana. Hata kama ninyi waislaam na wakristo mnatofautiana, siyo sababu ya kugombana na kuchoma makanisa, waacheni wakristo waendelee na utaratibu wao, kwani wakiwa makafiri ninyi inawadhuru vipi? Na ni vipi utafahamu kuwa dini yako ya uislaam ni ya kweli? Ndiyo...ukristo inaweza isiwe dini ya ukweli lakini kwanini mnawaingilia kwenye ustaarabu wao? Kwa nini msikae na ustaarabu wenu na msiwabughudhi wao na ustaarabu wao? Haya ndiyo hayo mambo yanayotokea huko Iraq, Syria, Lebanon, Libya na kwingineko ambako uislaam umeshagawanyika...kwa hiyo wewe hapo juu uliyesema wakristo na waislaam hawamwabudu Mungu mmoja, utasemaje kwenye hao washiite na wasunni? Je Washia na Wasunni mna miungu wenu tofauti? Kama sivyo mbona wanapigana? Jamani waislaam acheni udini na upuuzi mnaofanya wa kuchoma na kuua viongozi wa dini haina tija na haitawasaidia kufanya watu wahamie kwenye dini yenu. Mnaendelea kutufanya tuamini kuwa uislaam ni dini ya fujo.