ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 26, 2013

BARUA YANGU KWA NDUGU ZANGU WA BUSERESERE NA WATANZANIA WOTE- 2


Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Barua hii ni muendelezo wa iliyotoka toleo lililopita. Endelea kumalizia kuisoma:
Ni kweli hakuna kosa kwa mimi Mkristo kwa mujibu wa Biblia kuchinja mwenyewe na kula, lakini kuna tatizo gani iwapo nitatumia hekima ya kusema “Nanunua nyama hii kwa ajili ya kupika nyumbani kwangu, lakini binadamu tuna imani tofauti, wapo wanaoamini mpaka ng’ombe achinjwe na Muislam ndiyo inakuwa halali, tofauti ya hapo ni haramu, pengine naweza kupata mgeni wa imani hiyo na nisingependa kumkwaza acha ninunue iliyochinjwa na Muislam maana sijui nitatembelewa na nani…” kipi kitakuwa kimeharibika?
Meneja Mkuu wa Kampuni yetu Abdallah Mrisho ni Muislam, kwake ni haramu kula nyama ambayo haikuchinjwa na Muislam, lakini kuna kosa gani kama Mrisho akiwaona Wakristo wanachinja ng’ombe kwa imani yao na kuuziana wao kwa wao akiwa ametaarifiwa kabisa kwamba nyama ile, ng’ombe kachinjwa na Mkristo? Kwangu mimi sioni tatizo lolote atakachotakiwa kufanya yeye ni kuacha kwenda kununua nyama ile.
Kwa miaka yote nimeishi na Mrisho kama ndugu, yeye kwa imani yake nami na imani yangu, sijawahi kufikiria ipo siku nitakuja kuamka asubuhi namchukia ndugu yangu huyu kwa sababu ya Uislam wake, nimerithi kutoka kwa wazazi wangu kutowachukia watu kwa sababu ya tofauti zetu na hivyo ndivyo ilivyo kwa kila Mtanzania, sote tumerithi kupendana na kuheshimiana ingawa tunazo tofauti, ndiyo maana kwa miaka yote tangu kuwepo kwa dunia hatujawahi kuchinjana kwa sababu ya dini.
Swali ninalojiuliza baada ya tukio la Buseresere ni hili, hivi ni wapi nchi yangu inakoelekea? Na ni nani anayeipeleka huko? Kwa faida ya nani? Ndugu zangu nawasihi siku ya leo, kamwe tusifikirie kabisa kuiingiza nchi yetu nzuri kwenye machafuko ya kidini, tutakuja kujuta, bali tujifunze kuishi pamoja kama ndugu, katika namna ileile ambayo tumefanya siku zote. Kamwe tusiruhusu kugawanyika kwa sababu ya dini.
Ni lazima tuelewe kwamba majirani zetu wanatuonea wivu, watatucheka na kufurahia tukishapoteza amani yetu ambayo wengi wao hawana tena. Inawezekana wapo wachache wanaodhani vurugu zinaweza kutuletea suluhisho la matatizo tuliyonayo, si kweli, vurugu hazijawahi kuleta suluhisho mahali popote chini ya jua, bali kukaa chini na kuongea ili kutafuta majibu ya matatizo yetu ndiko kutakakotusaidia.
Kwa nini hatutaki kujifunza kwa wenzetu wa Misri? Walifanya vurugu, wakamwondoa Hosni Mubarak madarakani, nchi imetulia? Wana amani? Wana raha? La hasha! Nchi ndiyo imezidi kuharibika. Kwa nini hatujifunzi kutoka kwa wenzetu wa Libya? Walifanya vurugu wakamwondoa Muamar Gadafi madarakani, je nchi imetengemaa? La hasha! Imezidi kuharibika. Kama hivyo ndivyo, sisi tunataka vurugu za nini?
Mara zote nimesema naipenda nchi hii, kwa moyo wangu wote, si mimi peke yangu ninayeipenda Tanzania, tupo wengi, basi sisi tunaoipenda Tanzania na tusimame pamoja kuitetea, tukipinga kugawanywa kwa misingi ya dini na wachache wenye tamaa ya vita!
Sipendi kabisa itokee siku nijikute niko ukimbizini, nateseka na familia yangu, kwa sababu tu nilishindwa kuzuia machafuko kutokea kwa kuzungumza ukweli na kukemea uovu, hivi tunajua kwamba wakati mwingine kutokukemea uovu ni kuchagua kuwa sehemu ya uovu huo? Kama hivyo ndivyo basi tukataeni kutenganishwa kwa sababu ya tofauti ya dini, kabila au rangi zetu.
Imeanzia kwenye kuchinja ng’ombe, kama hatujaizuia itaendelea kwenye kuzikana ambako Wakristo watakuwa hawataki kuzika Waislam au kinyume chake,kutoka hapo litakwenda kwenye sherehe, Waislam watakataa kushirikiana na Wakristo kwenye harusi zao, itakwenda kwenye sehemu za kazi kama bosi ni Mkristo atakataa kuajiri Waislam, dhambi hii ya ubaguzi ikiendelea kwa muda mrefu itakuwa kansa ambayo itateketeza nchi yetu, lazima tuikatae kwa nguvu zote na tusisitize kuishi pamoja kama ndugu wa baba mmoja.
Naomba nimalize kwa kuwaomba Wananchi wa Buseresere, Nyehunge, Mwanza na Tanzania nzima kwa ujumla, tubadilike, huko tunakotaka kwenda tumepotea njia, ni vyema sasa tugeuke na kuanza kuelekea ambako tulitakiwa kwenda tangu mwanzo! Kwenye nchi ya ahadi ambayo wazazi wetu wa kwanza waliiota, mpaka wakaamua kumwondoa mkoloni; Tanzania yenye usawa kwa kila mmoja wetu, siku zote tupande pamoja na tushuke pamoja kama familia moja yenye upendo na amani.
Vijana wa Buseresere, hivi karibuni nitakuja ili tuongee juu ya umuhimu wa kuishi pamoja kama Watanzania. Tukatae ubaguzi wa aina yoyote uwe wa kidini, ukabila au wa itikadi za kisiasa, tukifanya hivyo tutakuwa tumemuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Ahsanteni kwa kunisoma.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu wabariki Watanzania.

No comments: