Wednesday, February 6, 2013

Daladala zaenguliwa D'Salaam


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Ahmad Kilima
Mpango wa kuziondoa daladala jijini Dar es Salaam ‘umeiva’, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kueleza kuwa kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, wasafirishaji wa magari hayo katika barabara za Kilwa na Ali Hassan Mwinyi, hawataruhusiwa kutoa huduma hiyo kama watakuwa hawajajiunga na kuanzisha kampuni au ushirika wa kusimamia usafiri huo.


Sumatra imesema kujiunga na kuanzisha kampuni au ushirika kwa wasafarishaji hao kutawawezesha kupewa leseni za kutoa huduma katika njia husika kuanzia tarehe hiyo.

Hata hivyo, Sumatra imesisitiza kuwa vigezo na masharti ya leseni za usafirishaji vitazingatiwa katika utoaji wa leseni hizo mpya; ambavyo ni pamoja na kampuni kuwa na mabasi yasiyopungua 100 na yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 70.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Sumatra kusitisha utoaji wa leseni mpya kwa mmiliki mmoja mmoja wa magari hayo ya abiria yanayopita katika njia hizo, kuanzia Mbagala kwenda maeneo ya jiji kati na maeneo mengine, na kuanzia Mwenge kwenda maeneo ya jiji kati.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabarani wa Sumatra, Leo Ngowi, alisema jana kuwa mwisho kwa wasafirishaji hao kuanzisha kampuni au ushirika huo, ni Juni 30, mwaka huu.

Ngowi alisema hayo wakati akiwasilisha mada ya hatua ya kuboresha huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam kwa kupitia kampuni za usafiri, katika mkutano wa wadau kuhusu uanzishwaji wa utoaji leseni kwa kampuni za usafirishaji abiria, ulioandaliwa na Sumatra jijini humo jana.

Ili kuonyesha kuwa Sumatra iko makini juu ya utaratibu huo mpya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Ahmad Kilima, aliwaeleza wadau kuwa fursa za kutoa huduma ya usafiri wa magari hayo Dar es Salaam, bado zipo, hivyo akawataka wasafirishaji wasioweza kuungana na kuanzisha kampuni waende wakaendelee kutoa huduma hiyo nje ya jiji, ikiwamo Mabwepande. 

Ngowi alisema hatua hiyo imechukuliwa na Sumatra kama njia mojawapo ya kuboresha mfumo wa utoaji huduma katika jiji hilo, ikiwa ni pamoja na wamiliki wa vyombo vya usafiri kujiandaa kushiriki katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (Darts) na kuwa na kampuni chache zenye uwezo wa kutoa huduma bora na mabasi yenye viwango.

Ngowi alisema Sumatra ilisitisha utoaji wa leseni mpya kwa mmiliki mmoja mmoja kwa magari yanayopita katika njia hizo, kuanzia Desemba Mosi, mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuanzia Juni 30, mwaka huu, Sumatra itasitisha uendelezaji wa leseni kwa mmiliki mmoja mmoja anayetoa huduma katika njia hizo.

Alisema kwa wale, ambao leseni zao zinaisha kabla ya Juni 30, Sumatra itaziendeleza kwa kuwapa leseni za muda mfupi zitakazoishia tarehe hiyo.

“Katika kipindi cha kuanzia tarehe 01/12/2012 hadi tarehe 30/06/2013 wasafirishaji wanaotoa huduma katika njia hizo wanashauriwa kujiunga na kuanzisha kampuni au ushirika ili waweze kupewa leseni za kutoa huduma katika njia husika kuanzia tarehe 01/07/2013,” alisema Ngowi.

Alivitaja vigezo vingine vya kampuni ya usafirishaji kuwa ni iliyosajiliwa Tanzania, iwe na ofisi yenye anuani na mahali, muundo wa kampuni, mpango kazi wa kampuni, eneo la mkuhifadhi na kufanyia matengenezo, mmahesabu ya mapato na matumizi, mpango wa ukaguzi na usimamizi wa magari.

Vigezo vingine ni mfumo wa kutoa tiketi, mfumo wa udhibiti wa mapato na kuzuia matumizi ya wapigadebe, mpango wa upangaji na ufuatiliaji wa ruti, utaratibu wa ajira kwa madereva na makondakta na kadiri maelekezo yatakayokuwa yanatolewa na mdhibiti.

Awali, Ngowi alisema hali ya utoaji huduma ya usafirishaji abiria katika jiji la Dar es Salaam haikidhi viwango vya ubora na kwamba, inakabiliwa na changamoto kadhaa; ikiwamo miundombinu isiyotosheleza mahitaji.

Changamoto nyingine alizitaja kuwa ni uduni wa vyombo vya uchukuzi; ikiwamo mabasi kuwa chakavu, uwezo mdogo wa mabasi, weledi usiotosha katika kuendesha biashara ya usafirishaji na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji zinazochangiwa na bei ya mafuta na vipuri.

Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni watoa huduma wenye mitaji midogo, matengenezo hafifu na yasiyokidhi viwango vya usalama na ubora, usimamizi duni katika uendeshaji wa biashara ya usafirishaji na kutofanyia matengenezo magari.

Changamoto nyingine ni kutokuwa na utamaduni wa kutii sheria kwa baadhi ya wamiliki, madereva na makondakta na malengo makubwa ya fedha kwa siku wanayowwawekea madereva.

Ngowi alisema katika Jiji la Dar es Salaam ni kampuni chache ndizo zinazomiliki vyombo vya usafiri; kama vile Uda na Cordial Transport, ambazo kila moja umiliki wake uko kwa mtu binafsi, wakati leseni hutolewa kwa chombo cha usafiri.

Hata hivyo, alisema muundo wa kampuni una manufaa makubwa kwa kuwa mmiliki wake anakuwa na wakaguzi, ambao pamoja na kudhibniti matumizi mabaya ya magari yao, hudhibiti pia uvujaji wa mapato ya kampuni, pia kampuni zitakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora na mabasi yenye viwango.

Alisema pia wamiliki wa kampuni kufanya biashara ya usafirishaji kwa weledi na ufanisi zaidi, uwezekano wa kupata menejimenti ya kisasa na yenye taaluma katika mambo ya usafirishaji na pia kuweza kuandaa taarifa za kihasibu na kuwa na utaratibu wa kuweka pesa benki.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, aliwataka wamiliki wa magari kutokuwa waoga kuupokea mfumo huo mpya wa kutoa huduma ya usafiri wa magari hayo jijini humo.

Kutokana na hali hiyo, aliwaeleza wamiliki wenzake wa magari hayo kuwa hawana budi zaidi ya kuungana na kuanzisha kampuni zao ili kuingia kama wanataka kuendelea kutoa huduma jijini humo.


Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Kilima alisema sekta ya usafirishaji abiria nchini inazidi kukua kwa kiwango cha kuridhisha na kwamba, sasa Watanzania wanashuhudia wamiliki hususan wa mabasi ya masafa marefu wakiwekeza katika mabasi mapya na yenye viwango vya juu.


Baadhi ya wadau katika kuchangia utaratibu huo mpya, walionyesha wasiwasi wao kuhusu kuungana wakisema ni vigumu katika kipindi kifupi cha miezi minne na wengine kushauri ufanyike utafiti kubaini mambo yaliyosababisha baadhi ya mashirika ya zamani kufeli katika suala hilo.

Hata hivyo, wengi walikubaliana na utaratibu huo mpya baada ya kuanza kujiorodhesha kwenye daftari maalum lililowekwa na uongozi wa Sumatra katika mkutano huo.

Mmoja wa wadau hao, Azim Dewji, licha ya kusaini daftari hilo, pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo, aliitaka Sumatra kueleza wapi mabasi hayo 100, ambayo kampuni imetakiwa kuwa nayo, yatakapokuwa yakilazwa.

Naye Mratibu wa Taifa wa Chama cha Wamiliki wa Magari ya Abiria nchini Kenya, maarufu kama “Matatu”, Albert Karakacha, aliwaondoa hofu wasafirishaji wa Kitanzania, akisema utaratibu huo hauna tatizo, badala yake una faida nyingi iwapo wataungana na kuwa wa wazi.

Alisema kwa kutekeleza utaratibu huo, mwaka 2008 walianza na basi moja, lakini hivi sasa wameweza kumiliki mabasi 150 na kwamba, unawasaidia kutoa ajira kwa watoto wao pindi wanapomaliza shule.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: