Rais Jakaya Kikwete
Kashfa inayohusu mradi wa maji uliotolewa mfano wa mafanikio kwa Rais Jakaya Kikwete alipotembelea wilaya ya Igunga mkoani Tabora, umezua mjadala huku ukidaiwa kujengwa kwa kiwango cha chini tofauti na inavyoaminika kwa walio wengi.Uharibifu mkubwa unaohusu mradi huo, unatajwa kuwepo katika eneo la Igogo ambapo katika ziara yake, Rais Kikwete aliambiwa kuwa utasaidia kutatua tatizo la maji wilayani humo kwa takribani asilimia 70.
Vyanzo tofauti vya ndani na nje ya IGUWASA vimedai kuwa miongoni mwa maeneo ‘yaliyoburuzwa’ katika ujenzi huo ni chujio la maji linalodaiwa kugharimu zaidi ya Shilingi bilioni 3.
Imeelezwa kuwa kutokana na ujenzi ulio chini ya kiwango, chujio hilo limekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya upotevu wa maji kutokana na udini wa viwango vilivyotumika katika ujenzi wake.
Hata hivyo, Meneja wa IGUWASA, Lema, alipoulizwa hivi karibuni kuhusu tuhuma hizo, hakukanusha wala kuthibitisha, badala yake alisema mwenye jukumu la kujibu tuhuma hizo ni Kingu.
Akiwa wilayani Igungda, Rais Kikwete alipata taarifa za miradi mbalimbali yenye matumaini ya kufikia matarajio ya umma, hivyo kuwepo kwa kashfa hiyo kunaweza kufifisha imani yake kwa uongozi wa wilaya hiyo.
Miongoni mwa miradi hai na inayokubalika kwa wananchi walio wengi ni uanzishwa mradi wa shamba kwa vijana wakiwemo waliohitimu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
Mwingine ni kutengwa eneo kwa ajili ya vijana wajasiriamali hasa wanaojishughulisha na ufundi wa magari.
Hata hivyo, baadhi ya shutuma zinaelekezwa kwa ‘kigogo’ mmoja wa IGUWASA (tunahifadhi jina lake kutokana na kutopatikana kuelezea tuhuma hizo), akihusishwa na ubadhirifu wa fedha na vifaa vya ujenzi.
Tayari baadhi ya watu wamepanga kuonana na Mkuu wa wilaya hiyo, Elibariki Kingu kumtaka afuatilie kashfa hiyo inayoweza kuwa doa kwa utawala wake unaotajwa kukubalika na kuwagusa walio wengi wilayani humo.
Hata hivyo, Kingu hakupatikana kulizungumzia suala hilo baada ya NIPASHE Jumamosi kuwasiliana naye kwa njia ya simu bila mafanikio.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, ‘kigogo’ IGUWASA anayetajwa kuhusika katika kashfa hiyo, anadaiwa kuwezeshwa kumiliki vitega uchumi na rasilimali kadhaa mkoani Tabora.
CHANZO: NIPASHE

No comments:
Post a Comment