ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 23, 2013

Waziri Maghembe aapa kuwatimua makandarasi

Pr. Maghembe
WAZIRI wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe amewataka makandarasi wanaosimamia ujenzi wa miradi ya maji Pwani,kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kabla hajawachukulia hatua kali ikiwamo kuwafukuza.

Pia Profesa Maghembe amewataka wananchi kuruhusu waendesha miradi ya maji kupitisha mabomba ya maji pasipokulipwa fidia.

Profesa Maghembe aliyasema hayo juzi wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya maji ya awamu ya pili mkoani humo.

Alisema miradi hiyo imekuwa ikitekelezwa polepole,ambapo amewataka kufanya kazi kwa juhudi ili kuhakikisha ifikapo Mei 30 mwaka huu unakamilika na wananchi wanapata huduma hiyo ambayo ni adha kwa mkoa huo.“Ninataka miradi hii ya maji ikamilike ifikapo Mei 30 mwaka huu na kwa mkandarasi ambaye atakuwa hajamaliza kazi yake hatutasita kumchukulia hatua kali ikiwamo kuwafukuza,” alisema Profesa Maghembe.Alisema kitendo cha wananchi kudai fidia pale wakandarasi wanapotaka kupitisha mabommba ya maji hakitakubalika.

“Wananchi wanatakiwa kujitoa na kuchangia huduma za maji ikiwa ni pamoja na kuruhusu mabomba kupita katika maeneo yao, ili kuhakikisha huduma inawafikia karibu,” alisema

Naye Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza alisema makandarasi hao wanaotekeleza miradi hiyo amewataka kujitahidi kumaliza kazi kwa wakati.

Alisema hakuna maendeleo bila maji,hivyo kitendo cha huduma hiyo kukatika mara kwa mara kinatakiwa kutafutia ufumbuzi na kumaliza. Mahiza alisema wananchi wanatakiwa kujitolea kusimamia miundombinu hiyo, ambayo bila hivyo hakutakuwa na maana yeyote ya kujengwa mkoani humo.

Kwa upande wake,Meneja wa mradi huo, Christer Mchoma alisema mradi huo unakwenda vizuri na unatarajiwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Mchoma ameiomba wizara ya maji kusaidia kupatikana kwa wataalamu wa kusimamia mitambo ya maji

“Hivi sasa kuna upungufu wa wataalamu wa kuendesha mitambo ambapo inatubidi kutumia wataalamu ambao wamebobea katika usimamizi hivyo tunaomba wizara itusaidia kwa hili,” alisema.
 Chanzo:Mwananchi

No comments: