Friday, February 22, 2013

Kim ampa kisogo Tegete

NDOTO ya mshambuliaji wa Yanga, Jerryson Tegete kuitwa kikosi cha Taifa Stars, imezidi kufifia baada ya Kocha Kim Poulsen kusema hana sababu ya kuita wachezaji wapya.
Stars inajiandaa kupambana na Morocco katika mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, Brazil.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Machi 22, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tangu kuanza kwa mwaka huu, Tegete amekuwa kwenye kiwango kizuri katika klabu yake ya Yanga, akifunga karibu kila mchezo.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts amemfanya kuwa mshambuliaji tegemezi kwenye michuano ya Ligi Kuu kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga aliouonyesha.
Tegete alikuwa miongoni mwa washambuliaji nyota wa Kocha Marcio Maximo alipokuwa akiifundisha Stars miaka minne iliyopita.
Msimu huu hasa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, ameonyesha kurejesha kiwango kizuri jambo lililowafanya wengi kudhani anaweza kuitwa Stars.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kim alisema hafikirii kumwita Tegete kwa sababu ya muda mchache wa kukaa kambini kabla ya kucheza na Morocco.
“Sifikiri kuongeza wachezaji wapya kwenye mchezo dhidi ya Morocco, muda wa maandalizi ni mdogo hivyo ni heri kubaki na wachezaji waliopo,” alisema Kim.
“Ligi inaendelea wachezaji wanazitumikia klabu zao hii ina maana pengine nitatumia siku nne au tano kukaa kambini na wachezaji kabla ya kucheza na Morocco.”
Kim alisema ana imani na wachezaji aliowatumia kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cameroon.
“Haimaanishi kwamba hakuna wachezaji wazuri, lakini lazima niwe wazi kwamba, programu yangu kwa sasa hairuhusu mchezaji mpya,” alisema Poulsen.

Mwananchi

No comments: