Friday, February 22, 2013

UHUSIANO WA DINI, KABILA, MILA KWENYE NDOA! – 3

NGUVU za Mungu ni za ajabu na haziwezi kufananishwa na yeyote. Ni yeye ndiye anayenipigania na kunifanyia njia mahali pasipo na njia. Ahsante kwa kila kitu Mungu wangu.
Mara ya mwisho nilizungumza kuhusu wasomaji waliowasiliana nami na kunipa shuhuda zao; walikuwa ni Dk. Milangwa na mama mtu mzima mwenye umri wa miaka 45 ambaye anaishi maisha ya mateso kutokana na kubadilisha dini ili aolewe.

MSIKIE MWENYEWE
“Mwanangu nimefurahishwa sana na mada yako. Vijana wa sasa wana bahati, wanapata mafundisho kama haya kwa uwazi kabisa. Sisi wakati tunakua kulikuwa hakuna majarida wala magazeti yanayotoa elimu kama hivi.
“Nimeolewa miaka 28 iliyopita, kwanza niliishi na mume wangu mwaka mzima bila ndoa, maana tulikuwa tunavutana kuhusu suala la dini (naomba kuficha imani zao). Mume wangu alinisisitiza nimfuate kwenye dini yake ili aweze kunioa, nikakubali.
“Mwanzoni ndoa ilikuwa tamu sana lakini baadaye mambo yakabadilika. Mume wangu amekuwa mkorofi na ana wanawake wengine nje. Amani niliyoifuata kwenye ndoa yangu kwa kuamua kubadili dini siipati tena.
“Mbaya zaidi mume wangu hanifundishi namna ya kuabudu kwa utaratibu mpya wa imani yake, imefikia mahali nimeona najitesa tu nafsi yangu, siku hizi kwa kujiiba huwa nakwenda kwenye imani yangu ya zamani na ninaabudu huko.
“Lingine linaloniumiza ni watoto wetu. Tumejaaliwa watatu, wawili wanasoma chuo (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na IFM) wa mwisho anasoma Moshi, yuko form three (kidato cha tatu). Hawa wawili wamejikuta wanapenda kufuata dini yangu na wanakwenda kuabudu kwangu, huyu wa mwisho yeye ameamua kumfuata baba yake.
“Hofu yangu kubwa ni mume wangu kugundua kwamba mimi nimesharudi kwenye imani yangu na watoto wetu wawili wapo katika imani yangu. Kifupi nakumbana na changamoto nyingi sana lakini sina namna maana tayari mimi ni mtu mzima sina cha kufanya, najitahidi kuwafundisha wanangu wasiingie kwenye mtego kama wangu.”

UMEPATA KITU?
Wakati mwingine ukweli unaweza kuwa unauma lakini ni vizuri kuuchukua kama changamoto. Haraka ya ndoa na kufanya uamuzi wa haraka wa kubadili imani au ndoa ya mseto, kunaweza kukusababishia matatizo.
Uamuzi wa nani awe mke/mume wa ndoa unatakiwa kuchukua kwa umakini mkubwa sana. Ukikosea kuchagua mwenzi sahihi wa maisha ni dhahiri kwamba huko mbele maisha yako yanaweza kubadilika na kuwa machungu. Jifunze kupitia kwa wengine.
Wengi wanadhani ndoa ni bahati, si kweli. Kila kitu hufanyika kwa wakati wake na mpango wa Mungu.

LINAZUNGUMZIKA
Ili uwe salama na usiingie kwenye mtego huu ni vyema mkalizungumza jambo hili mapema sana. Unapokutana na mwenzako na ukahisi kuna dalili za kufika mbali katika uhusiano wenu ni vyema mkazungumzia kuhusu imani zenu.
Usisubiri tatizo likue, lazima ujue mwenzako ni imani gani ili baadaye mkifikia kwenye suala la ndoa isiwe tatizo kwako.

KABILA/MILA

Wazee wanajua zaidi kuhusu hili ndiyo maana kijana akipata mchumba swali la kwanza kuuliza ni juu ya dini na kabila, kuna makabila yana mila potofu; sasa huwezi kusubiri mpaka mtakapofikia kwenye mipango ya ndoa ndiyo unaanza kuchunguza.
Unaingia kwenye ndoa unakutana na tabia za ovyo, kumbe ni kosa lako hukuchunguza. Mada imeisha. Wiki ijayo nitakuja na nyingine nzuri zaidi, tafadhali sana USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: