Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Duwani Nyanda akizungumza na viongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki ambapo polisi walizuia ibada kufanyika jana katika Kanisa la Moravian Ushirika wa Tabata jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa ingehatarisha amani kwa waumini hao. Picha na Pamela Chilongola
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini, la kutaka kufunguliwa makufuli yaliyofungwa katika Kanisa la Usharika wa Tabata, ili waweze kumsimika mchungaji mpya, ambaye ni Lawi Mwankuga.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Mathew Mwaimu,baada ya bodi hiyo ya wadhami wa Kanisa la Moravian Kusini chini ya Mchungaji Clement Mwaitebele, kupitia wakili wao, Henry Chaula wa Kampuni ya Uwakili ya C&M, kufungua kesi namba 12 ya mwaka 2013 na kuomba isikilizwe chini ya hati ya dharura.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Mchungaji Gervas Mwakafwila, Mchungaji Silas Mwakibinga, Tukuswiga Mwakabur, Atuganile Mbombo, Isakwisa Ernest na Sekela Mukisele ambao wanatetewa na Wakili Benjamin Mwakaganda wa Kampuni ya uwakili ya BM, wanadaiwa kufunga makufuli kwenye Kanisa la Usharika wa Tabata, ili kuzuia bodi hiyo kumsimika mchungaji mpya.
Akitoa uamuzi, Jaji Mwaimu alikataa ombi la bodi hiyo ya wadhamini la kutaka kufunguliwa kwa makufuli yaliyokuwa yamefungwa kwenye kanisa hilo, ili kupisha kumsimika mchungaji mpya.
Pia jaji huyo aliruhusu shughuli za kawaida za kanisani hapo kuendelea na kusisitiza kwamba kilichozuiwa ni usimikaji wa mchungaji ili kuondoa uvunjifu wa amani.
Pia jaji huyo aliruhusu shughuli za kawaida za kanisani hapo kuendelea na kusisitiza kwamba kilichozuiwa ni usimikaji wa mchungaji ili kuondoa uvunjifu wa amani.
Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Mwaimu aliwataka wadaiwa kupeleka kiapo pinzani mnamo au kabla ya Februari 5, mwaka huu ambapo kesi hiyo imepangwa kusikilizwa.
Bodi hiyo ya wadhamini wa Kanisa la Moravian Jimbo la Rungwe ni wadaiwa namba 4 katika kesi namba 222 iliyofunguliwa mwaka 2012 katika Mahakama Kuu, ambayo inaendelea kusikilizwa Februari 6, mwaka huu mbele ya Jaji Augustini Mwarija.
Katika kesi hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Jimbo la Mashariki na Pwani ya Kanisa la Moravian Tanzania, Clement Fumbo na wenzake saba wanapinga kuondolewa madarakani na kusimamishwa kazi.
Katika kesi hiyo, Fumbo na wenzake hao saba wanaiomba Mahakama iamuru walipwe Sh500 milioni kama fidia na gharama ya kesi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment