NA Flora Wingia.
Mpenzi msomaji, bila shaka u bukheri wa afya. Wiki iliyopita niliahidi kuwaletea maoni ya makala tatu hivi zilizotangulia. Makala hizo zilikuwa na vichwa vya habari vyenye maneno yafuatayo;“Eti ni kweli ndoa nyingi zinavunjika kisa kinamama wamejiunga Saccos, Vikoba?”, “Mwanaume anafanya kazi lakini mkewe kutwa anaranda mitaani au kwa waganga!”, na “Fundi nguo amenizimia nilipotaka anishonee nguo zangu, nifanyeje?”
Kati ya mada hizo ambazo tayari zilishachapishwa gazetini, hiyo ya fundi nguo ndiyo iliyopata wachangiaji wengi kama ambavyo itaonekana hapa chini.
Nyingine ambayo nitaifanyia muendelezo ni hiyo ya kinamama kujiunga na saccos au vicoba na tafrani zake kama ambavyo nilisimuliwa mikasa wakati nikiwa likizo kijijini kwangu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro hivi karibuni.
Katika mada hii, niwamegee ujumbe mmoja wa simu unaosomeka ifuatavyo; “Kuna familia zingine hazihitaji mikopo lakini utaona mwanamke analazimisha kujiunga na Vicoba. Mume akikataa mwanamke anajiunga kwa nguvu.
Hii inapelekea kwenda kinyume na maagizo ya Muumba wetu kwamba mwanamke anapaswa kuwa mtii kwa mumewe. Matokeo yake nyumba inakwa kwenye turmoil(vurugu). Kuna mke wa rafiki yangu alikopa Vicoba kwa siri akaweka rehani samani zote za nyumbani akawekeza kwenye mradi wa mitumba.
Aliposhindwa kurejesha Vicoba wakataka kupiga mnada samani ndipo mume akashtuka. Ilibidi mke asepe kusikojulikana. Ilibidi mwanaume aingie mkataba na Vikoba akalipa deni kwa miezi mitatu ndipo mama akarejea! (Mosoi)
Mpenzi msomaji, hebu sasa nikukumbushe ujumbe wa bibie kuhusu fundi nguo kama ulivyotumwa na bibie kupita simu ya mkononi, halafu usikie maoni yaliyotolewa na wasomaji wengine kuhusu suala hilo
Ujumbe ulisomeka hivi;“Shikamoo, mimi kuna fundi mmoja nilimpelekea nguo zangu, basi akaomba namba yangu ya simu. Lakini nilivyomuona ananipenda sababu ananirushia hela, ananipa hela.
Chaajabu pia ananipigia kila siku lakini bado hajaniambia kitu ila naona anashindwa kuongea sababu mimi na yeye nilimjua baada ya kupeleka nguo zangu. Naomba nishauri.”
Naam. Huo ndio ujumbe wenyewe. Sikia ushauri wa wasomaji mbalimbali:
…Dadangu, huyo mchizi fundi nguo kwanza nasema asipoangalia atajikuta anaharibu kazi yake kwani siyo wateja wake wote wa kike watakaoenda hapo watafurahia tabia yake. Pia nampa huyo bibie big up(nampongeza) kwa kuomba ushauri. Mchizi yawezekana ni tabia yake kwa hiyo kama vipi mwambie biashara yake naye ni nguo na siyo kingine akupoteze((Thadeus a.k.a Phide Boy).
Mwingine anamshauri hiyi; “Binti nampa mfano mmoja ulio wazi. Fundi huyo wa nguo au fundi cherehani ni kama basi la abiria ambapo hupenda kila abiria apande lakini ikifika wakati huachwa kila abiria na kutafuta wengine. Binti huyo amwone binti huyo kama chui mwenye madoa mazuri akimchekea tu atamharibu sura na kumwachia majuto”(Msomaji).
…Hapo Anti Flora kuna mawili; huenda huyo fundi ni laghai au ana upendo wa kweli. Yapo mengi ya kumtambua aliye mkweli au laghai.
1. Achunguze je, huyo bwana ana mke au rafiki wa kike? 2. Je, ni mcha Mungu, 3. Je, yuko tayari kuwaona wazazi au hata ndugu wa binti, 4. Je, suala la ukimwi yuko tayari kupima, 5. Je, binti anataka kuolewa?
Akipata majibu hayo machache, majibu anayo mwenyewe. Ila hela asichukue kwanza mpaka ajue anachukua hela hiyo kama nani. (Mama Lulu, Kitunda)
Mwingine anasema…Hapo huyo fundi hana mapenzi ya kweli kwani anatumia hela kama kishawishi. Kuhusu huyo dada yeye anatumiwa hela hatujajua huwa anazikataa au huwa anazipokea. Na kama anazipokea hapo kafanya makosa. Cha msingi amwambie ukweli kwamba yeye ni mwanamke anayejiheshimu na hataki kutumiwa na amwambie huyo fundi ina maana ameniona mimi kahaba au au umenichukuliaje.
Mtu unamwambia ukweli tu kwani anayetumia hela huwa ni hatari. Jiulize keshawatumia hela wangapi. Ila inawezekana na huyo dada kashaanza kumpenda ila kama ulivyomshauri huyo siyo mwanamume mwenye msimamo kwani hataki kuweka wazi kwamba amempenda.
Isitoshe, anataka siku akija kumwambia huyo dada kampenda naye akikataa huyo fundi ataanza kumkumbushia umekula hela zangu unakataa nini. Mwanamke anapewa hela kwa makubaliano sasa wewe unampa tu, je, ukijajua ana mtu mwingine ni itakuwa kazi kubwa? (Elia Kaovela, Iringa)
….Msomaji mwingine anasema; “Kwani fundi mshona nguo kabakia mmoja huyo huyo? Kama binti anajiheshimu na anaheshimu mahusiano anayoweza kuwa nayo, namshauri achukue vitambaa vyake avipeleke kwa fundi mwingine. Vinginevyo binti huyo anatutega (baba Kevin, Mbezi Beach Dar)”.
Mwingine anasema; kwanza lazima bibie ajiulize ni wangapi tangu aanza ufundi wake. Asikubali huyo fundi ni kazi yake kila amuonaye anampa namba ya simu na inawezekana hiyo simu yake imejaa namba za wateja kama yeye( Haji Mzigo wa Tanga Mabawa).
…Mwingine anasema:Fundi cherehani kuwadi tu. Binti afanye utafiti kabla ya kumkatalia. Nimesema afanye utafiti ili asimkose rafiki au mchumba. Kama fundi anataka mapenzi amkatalie na amwelekeze kwa wazazi. Nahisi binti ni mdogo (Msomaji , China).
Naitwa Muharami Katapila ningependa kuchangia mada hiyo kwamba dada huyo kupewa hela siyo tatizo kwani ni sawa na zawadi. Namshauri huyo dada apokee hizo pesa za fundi lakini mwisho wa siku huyo fundi akimtamkia kumtaka kimapenzi amwambie kuwa yeyehamtaki na kumpa pesa isiwe sababu kumtaka kimapenzi. Asante.
…Ninavyoelewa huyo jamaa inawezekana amempenda huyo binti ila anashindwa kumtobolea ukweli na ndio maana anatumia njia hiyo ya kumrushia vijisenti. Ninachomshauri aondoe aibu. Wanaume tulishajaliwa na Mungu kipaji na ndiyo maana wanawake wapo chini yetu katika maandishi ya kibiblia. Basi ajifunze ujasiri atalizwa. Ni mimi Pascal MTASIWA NIPO Makambako mkoa mpya wa Njombe.
Mambo ni mambo. Msomaji wangu hayo ndiyo niliahidi kukuletea leo. Tuonane tena wiki ijayo kwa mjadala mwingine. Kama unacho kituko ungependa tujadili kwa pamoja usisite kunitumia.
Hebu nikuache na swali moja; Ndoano ya pesa kumkamatisha mpenzi ni udhaifu au ulimbukeni? Ukipata majibu kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com
Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.
No comments:
Post a Comment