ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 15, 2013

Makamu wa Pili wa Rais akipokea ujumbe wa NSSF

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kitope Bibi Halima Bushir Abeid mchango wa Shilingi 100,000/- kwa ajili ya ulipaji huduma ya umeme ya kituo hicho hapo mbaleni katika Jimboni humo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijaza Fomu Maalum ya kuomba uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii { NSSF } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijaza Fomu Maalum ya kuomba uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii { NSSF } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kitope Bibi Halima Bushir Abeid mchango wa Shilingi 100,000/- kwa ajili ya ulipaji huduma ya umeme ya kituo hicho hapo mbaleni katika Jimboni humo.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewaomba mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) kufanya utaratibu wa kushawishi mifuko mengine ya Jamii kuanzisha miradi ya Jamii ili kuongeza pato la wanachama pamoja na Maendeleo ya Taifa nchini.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akipokea ujumbe wa NSSF waliofika ofisini kwake kumjazisha fomu maalum ya kuomba uanachama wa mfuko huo Ofisini kwake jana Vuga Mjini Zanzibar.Balozi Seif alisema Mfuko huo umesaidia jamii kwa kiasi kikubwa na ni matumaini kwa wanachama wake hasa kutokana na miradi mingi iliyoianzisha ambayo kwa Asilimia kubwa inalenga kuwanufaisha wanachama wake hasa wale wenye kipato cha chini.

“Ni wazi kabisa na hilo halina ubishi kwamba NSSF mnastahiki pongezi za kweli kutokana na juhudi zenu mnazozitekeleza na nashangaa mfumo kama huu siuoni katika mifuko mengine. Nahisi mnawajibu wa kuisaidia kimaarifa Mifuko hii ili ifuate nyayo zenu za kusaidia jamii yetu lakini hata nchi”.Alisema Balozi.Balozi Seif ambaye baada ya kujaza fomu hiyo ya uanachama alisema NSSF ni chombo cha wananchi kwa vile kinajihusisha moja kwa moja katika kutoa huduma za jamii na amevutika sana na miradi ambayo imeanzishwa na mfuko huo.

Baada ya kukamilisha taratibu za uanachama Balozi Seif aliuahidi ujumbe huo wa NSSF kwamba atakuwa akichangia kila baada ya kipindi cha miezi mitatu kama ni mchango wake kwa mfuko huo na kuwataka uongozi wa mfuko huo kuendelea kuwahamasisha watu mbali mbali na mashirika kujiunga ili kusaidia mfuko huo.

Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Dodoma ambao ndio uliopewa jukumu la kuhudumia Viongozi wa ngazi ya Juu, Bibi Maryma Ahmed alisema zaidi ya Wabunge 165 wamekubali kujiunga kwa hiari kuwa wanachama wa Mfuko huo na wanaendelea kuchangia kama kawaida.

Maryam alisema kwamba wabunge hao hupatiwa mafao yao mara tu wanapomaliza utumishi wao wa Bunge sambamba na huduma za matibabu wakati wa kipindi chote cha kazi zao ambapo alisema ni fursa muhimu sana kwa watu kujiunga ili kupata huduma za kijamii.

Meneja huyo wa NSSF Kanda ya Dodoma alieleza kuwa wapo Wabunge wastaafu waliomaliza wadhifa wao lakini bado wanaendelea kuchangia mfuko huo kwa vile bado wana fursa iliyo wazi ya kufanya hivyo.

Balozi Seif amesajiliwa kuwa mwanachama wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii baada ya kukamilisha taratibu zote za kujaza fomu ya usajili mbele ya Timu ya Maafisa wa mfuko huo ikiwemo pia kupigwa picha kwa ajili ya kupatiwa kitambulisho rasmi cha uwanachama kamili wa mfuko huo.

wakati huo huo Waziri wa nchi ofisi ya Makamo wa pili wa rais Mohamme Aboud Mohammed amesema wananchi wa Zanzibar bado hawajapata mwamko mzuri wa kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF na kuwataka uongozi wa mfuko huo kuendelea kuelimisha jamii.

Aboud amesema binfasi amevutiwa sana na miradi na huduma zinazotolewa na NSSF na hivyo kujiunga kwa wanachama wengi kutasaidia serikali kwa kuwa huduma nyengine serikali haiwezi kuzibeba peke yake bila ya kupata msaada wa taasisi za kijamii na mashirika.


Alisema iwapo elimu hiyo itafika kwa wananchi wa kawaida baadhi yao watavutika na watahitaji kujiunga kwani mifuko ya kijamii ina faida kubwa hasa kwa wananchi wa mashambani ambao wana miradi mbali mbali ya kujisaidia.

Waziri huyo ambaye naye amejiunga na mfuko huo kwa kujaza fomu aliwaahidi uongozi wa NSSF kwamba atawashawishi wakulima wa karafuu, wavuvi, na wajasiri amali wadogo wadogo ili waweze kujiunga na mfuko huo ili kuweza kuweka akiba ya fedha zao lakini pia kunufaika na mfuko huo ikiwemo huduma za afya.

Naye kwa mara nyengine Meneja wa NSSF Bi Maryam alisema wajasiri amali wadogo wadogo na sekta zisizo rasmi watafaidika endapo watajiunga na mfuko huo wa hiari ambao utasaidia maisha yao ya baadae.

Alisema wafanyikazi wa sekta zisizo rasmi kabla haujanzishwa mfuko huo wa hiari walikuwa hawachukuliwi na sekta nyengine yeyote isipokuwa yule aliyeajiriwa katika sekta binafsi tu.

Alisema faida za kujiunga na mfuko huo ni nyingi ikiwemo kupata mafao yao baada ya kustaafu, huduma za matibabu, huduma za uzazi, kuumia kazini na huduma za mazishi.

Bi Maryam alisema mafao mengine yatakuwa ni baada ya muda miaka mitatu kuchangia mfuko huo ni mafao ya pensheni ya ulemavu , pensheni urithi na pensheni ya uzee .

“Kina mama waja wazito watafaidika na mafao ya mfuko wa hiari endapo watajiunga na mfuko huo, tunaendelea kuwahamasisha wana jamii wajiunge”alisema Bi Maryam .

Meneja huyo alisema NSSF wana mkataba wa mashirikiano na ZSSF ya Zanzibar na hivyo wanachama wao NSSF waliopo Zanzibar wanapeleka fedha zao ZSSF kama ambavyo ZSSF waliopo Bara wanapeleka katika mfuko wa NSSF kila mwezi.

“Sisi tuna mkataba wa mashirikiano na ZSSF kwa hivyo wanachama wetu fedha zao zinakusanywa na ZSSF na sisi kule bara wanachama wa ZSSF fedha zao wanaleta kwetu NSSF kwa hivyo huwa tunasaidia kukusanyiana fedha na kila baada ya muda huwa tunakuja kuchukua fedha zetu” alisema Bi Maryam.

No comments: