Zapigwa 200, sms 400
Chanzo kilichopo karibu na Spika kimesema kuwa tangu chama hicho kilipotangaza namba hizo za simu, jumla ya simu 200 za kumtukana Spika zilipigwa.
Hali kadhalika, katika kipindi hicho jumla ya ujumbe 400 mfupi wa simu za mkononi (sms), uliokuwa ukimtukana ulipokelewa katika simu zake.
“Simu hizo walikuwa wameshika wasaidizi wake, kila aliyepiga simu kwa lengo la kutukana, amekuwa akiachwa kutukana hadi anapomaliza na kisha kuambiwa sawa,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake liandikwe gazetini.
Hata hivyo, NIPASHE ilimtafuta Spika Makinda jana kuzungumzia suala hilo bila mafanikio na kuelezwa kuwa ofisi ya Bunge itafanya mkutano na waandishi kati ya leo ama kesho kulizungumzia sakata hilo.
KAULI YA SITTA
Alipoulizwa kuhusiana na kutukanwa kwa Spika Makinda, Spika Mstaafu, Samuel Sitta, alisema kumtukana mtu mzima si maadili mema na kwamba hata kama kuna mambo ambayo mbunge hakubaliani nayo, nchi zote zimeweka taratibu za kushughulikia mambo kama hayo.
“Wanatakiwa kuwa wavumilivu…wafuate taratibu ambazo zimewekwa katika kushughulikia mambo hayo,” alisema.
Alisema amesikia kuwa wabunge wa Chadema wakirejea bungeni wameandaa mpango wa kusimama na kupiga kelele wakati kikao cha Bunge kikiendelea.
“Najiuliza ni mpango gani kama kupiga kelele, nimesikishwa sana mimi kama mtu mzima na mambo haya,” alisema Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema mambo yanayofanywa na Chadema ni dalili za kufilisika kisiasa.
“Bunge limeweka taratibu za kushughulika na rufaa na mambo ambayo upande mmoja unapinga, wao Chadema ndiyo kambi rasmi bungeni wanatakiwa kama kuna kitu wanakipinga kufuata taratibu zinazokubalika,” alisema.
Aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Tisa kupitia Jimbo la Iramba Magharibi (CCM), Juma Kilimbah, alisema siyo vibaya kutolewa kwa namba ya simu ya kiongozi, lakini kama kukiwa na dhamira nzuri.
“Nawatahadharisha waliopewa wasije wakachuuzwa wakamtukana Spika, maana hii inaweza kuwasababishia kuwa na kosa la jinai kwa kuwatukana watu,” alisema Kilimbah, ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM.
Kwa mujibu wa viongozi wa Chadema, lengo la kugawa namba hizo za simu ni kuwataka wananchi ambao waliwaita kuwa ni ‘mahakama ya umma’ wawatumie ujumbe mfupi wa simu za mkononi wa kuwataka Makinda na Ndugai wajiuzulu kutokana na kushindwa kuliendesha Bunge kwa kupendelea CCM na kuuonea upinzani.
Chadema wanadai kuwa kiti cha spika kimekalia rufani za miongozo mingi bila kuitolea majibu tangu mwaka 2011.
Miongoni mwa ushahidi wa miongozo na rufaa zilizowasilishwa katika ofisi ya Spika ni ya kiti kwa kukataa kuliwezesha Bunge kujadili hali ya huduma katika hospitali za umma na jaribio la kutaka kuuawa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka uliotolewa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Nyingine ni kutoridhishwa na uamuzi wa Naibu Spika wa kukataa mgomo wa walimu na yatokanayo na mgomo huo kujadiliwa bungeni, malalamiko dhidi ya uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Muhagama, kwa kudai kuwa Mnyika anao ushahidi kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Lameck Mwigulu Nchemba (CCM), ni mmoja wa watuhumiwa wa kesi za Epa na kumtaka kuwasilisha ushahidi.
Uamuzi kuhusiana na uthibitisho kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), juu ya kauli ya uwongo unaodaiwa kutolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bungeni wakati akijibu maswali Februari 10, mwaka 2011.
Maamuzi mengine yanayodaiwa kutotolewa uamuzi na Spika, ni kauli ya Mbunge wa Meatu (Chadema), Meshack Opulukwa, ambaye alisema bungeni kuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Abihudi Saideya, alihongwa gari ili ampatie mwekezaji kitalu cha uwindaji kwenye pori la akiba ili wananchi waondolewe eneo hilo.
Uamuzi mwingine ambao haujatolewa ni wa Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya (CUF), ambaye alitakiwa kuwasilisha uthibitisho wa kauli yake kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo, aliingia katika zizi la mfugaji na kutoa mbuzi kisha kumchinja bila ridhaa ya mmiliki.
Uamuzi mwingine ni mwongozo wa kuhusu kauli ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye alisema kuwa majaji wengi wanateuliwa bila kuwa na sifa.
Mwongozo mwingine ambao haujatolewa maamuzi licha ya kuwasilishwa kwa ushahidi, ni Baraza la Mawaziri kushawishi Shirika Hodhi la Mashirika ya umma (CHC) lisiongezewe mkataba.
Viongozi wa Chadema waligawa namba za viongozi hao wa juu wa Bunge Jumapili iliyopita katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Temeke Mwisho, jijini Dar es Salaam.
NDUGAI AWAJIBU CHADEMA
Kufuatia shinikizo hilo, Ndugai amesema kuwa Chadema wanapaswa kufuata kanuni na sheria zilizomo katika katiba za kuwaondoa madarakani viongozi kuliko kutumia njia ya maandamano.
Akuzungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kuhusiana na alivyopokea wito wa Chadema wa kumtaka aachie ngazi, Ndugai alisema kuna sheria na taratibu zilizowekwa katika kuiongoza nchi, hivyo kila mtu anapaswa kuzifuata.
Alisema endapo Mbunge akimtaka rais, waziri, spika au kiongozi yeyote aliyeko serikalini kujiuzulu, inampasa kufuata utaratibu uliowekwa na siyo kutumia njia ya maandamano.
Ndugai alisema mbunge pia anaweza kuandika barua au kuwasilisha hoja bungeni ya kumtaka spika au naibu spika ajiuzulu na hoja hiyo itajadiliwa na wabunge.
“Wanapaswa kuwasilisha hoja bungeni, hoja itapokelewa lakini, siyo kwa njia ya maandamano, ile ni ofisi ya umma siyo yangu, kila mtu ana haki ya kuliongoza Bunge,” alisema Ndugai, ambaye alilalamikiwa na upinzani kwa hatua yake ya kukubali Bunge liondoe hoja ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) kuhusu kasoro katika mtaala wakati wa Mkutano wa 10 uliomalizika wiki iliyopita.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment