ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 12, 2013

Wanasheria wa Uamsho wachachamaa Zanzibar


Mahakama Kuu ya Zanzibar, imeombwa kuondoa vizigiti kwa watu wanaokwenda mahakamni kufuatilia  kesi inayowakabili viongozi 10 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki).
 
Viongozi hao wamefunguliwa mashitaka ya kusababisha uharibifu wa mali za watu na serikali na kuhatarisha usalama wa taifa na wamekuwa wakifikishwa mahakamani wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto kuanzia Oktoba  21, mwaka jana.
 
Ombi hilo limewasilishwa na mawakili wanaotetea  washtakiwa Salim Towfiq na Abdallah Juma, ambapo walidai ndugu na jamaa wamekuwa wakikutana na vizigiti vya kuwanyima haki ya kusikiliza maendeleo ya kesi hiyo.
 
Wanasheria hao walidai kuwa tangu kufuguliwa kwa kesi hiyo wake za washitakiwa, ndugu, jamaa na marafiki  wamekuwa wakinyimwa haki ya kuingia katika chumba cha mahakama kusikiliza kesi na kufahamu maendeleo yake.
 
Towfiq alidai kuwa wanafamilia hao wamekuwa wakinyimwa haki ya kuingia katika chumba cha mahakama na vyombo vya dola, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na misingi ya haki za binadamu na utawala bora.
 
Alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 88 (1) cha Sheria ya Kuendesha Kesi za Jinai namba 7 ya mwaka 2004, kesi za jinai zinatakiwa kuendeshwa  katika mahakama ya wazi na kuhakikisha umma unapata nafasi ya kusikiliza uendeshaji wake.
 
Hata hivyo, alidai kuwa bahati mbaya kesi hiyo kila inapotajwa askari wa Jeshi la Polisi wakishirikiana na Vikosi vya SMZ, wamekuwa wakiweka vizuizi vya kungia mahakamani kwa ndugu na jamaa wakiwamo wake zao.
 
Alidai kwamba utaratibu huo hakubaliki kwa sababu unavunja sheria ya mwenendo wa usikilizaji wa kesi za jinai kwani ndugu na jamaa zao wana haki ya kufahamu kila kinachoendelea katika kesi kabla ya mahakama kutoa hukumu kwa washtakiwa hao. Hata hivyo, akijibu malalamiko hayo, Hakimu Yessaya Kayange,  alisema mahakama ni chombo huru na kazi zake zinatakiwa kufanyika katika mazingira ya uwazi na wananchi kupata nafasi ya kusikiliza kesi dhidi ya washtakiwa.
 
Viongozi wa Uamsho walioshtakiwa ni Masheikh  Farid Hadi Ahmed (41), Msellem Ali Msellem (52), Mussa Juma Issa (37), Azzan Khalid Hamdan (48) na Suleiman Juma Suleiman (66).
 
Wengine ni Khamis Ali Suleiman (59), Hassan Bakar Suleiman (39), Gharib Ahmad Omar (39), Abdallah Said Ali (48) na Fikirini Majaliwa Fikirini (48) wakazi wa mjini Zanzibar.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: