ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 12, 2013

Mwakyembe avamia reli Moro

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe 


WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema kuwa atasitisha mikataba yote ya magari yanayohusika kubeba mafuta na kusambaza katika Shirika la Reli Tanzania (TRL) kutokana na hasara inayopatikana badala yake kutumia usafiri wa shirika hilo.

Mwakyembe alisema hayo mjini Morogoro alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye stesheni ya reli iliyopo mjini Morogoro na kudai kuwa hatakuwa tayari kuendelea kufumbia macho suala hili la usafirishaji wa mafuta kwa magari wakati shirika hilo lina uwezo wa kusafirisha mafuta kwa kutumia usafiri wao.

Alisema endapo shirika litatumia mabehewa yake kusafirishia mafuta shirika halitapata hasara kama inayoendelea kupata kutokana na kutumia magari binafsi kusambaza mafuta kwenye stesheni zote nchini. Kwa upande wa wafanyakazi wa shirika hilo Kituo cha Morogoro, Taferi Dimisheni na Ramadhani Dalueshi, walisema kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu licha ya kuwa taifa linategemea pato kupitia shirika hilo.

Walisema kumekuwa na tatizo la mabehewa ya mizigo kukaa muda mrefu kituoni hapo kutokana na kukosekana kwa mafuta katika kituo hicho.

“Inafikia wakati mafundi injini wanashindwa kutengeneza injini za treni kutokana na kukosekana kwa mafuta na kusababisha msongamano wa mabehewa ambayo yana mizigo ya wateja wao,” alisema Taferi

Kwa upande wake, dereva wa treni inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Morogoro, Rango Mboma alisema kuwa madereva wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu hali inayowasababisha kuwa na madeni mengi kutokana na kutegemewa na familia zao.

Alisema kuwa kipato wanachopata wao hata dereva wa boda oda wanawazidi kwa kipato hivyo Serikali inatakiwa kuwaboreshea masilahi wafanyakazi wa kituo hicho.

Akitoa ufafanuzi wa madai hayo Meneja wa Karakana ya Morogoro, Mhandisi Nejo Ngosomwile alikiri kuwapo kwa matatizo hayo likiwamo la mafuta.

hivyo kusababisha mabehewa ya mizigo kukaa kwa muda mrefu.
Hivyo aliiomba Serikali kuboresha masilahi ya wafanyakazi wakiwamo madereva kwani wao ndiyo wanaotegemewa katika kusafirisha abiria.
Mwananchi

No comments: