Hofu ya kushambuliwa na wananchi wanaopinga ujenzi wa bomba la gesi imesababisha baadhi ya polisi waliokuwa wanafanyakazi mjini Mtwara kutimka na kutelekeza vituo vya kazi.
Hatua ya kukimbia na kusitisha huduma katika vituo hivyo imesababisha wakazi wa maeneo ya Vigaeni na kituo kikuu cha mabasi cha mkoa wa Mtwara kukosa msaada wa polisi.
Wakizungumza na NIPASHE baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walisema kituo cha Vigaeni na kile cha Stendi ya Mkoa vilishambuliwa wakati wa vurugu zilizotokea mwezi uliopita.
Walidai vituo hivyo vilivyokuwa vinahudumia watu wengi vilipigwa mawe, samani zake kuharibiwa na polisi walikimbia kunusuru maisha yao.
Ilielezwa kuwa tangu wakati huo wananchi wanaoishi maeneo hayo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu wengi wakiwa na kipato kidogo hawana huduma za polisi hivyo kukosa usalama wa kutosha.
Kuwapo kwa hali hiyo kumesababisha mji wa Mtwara kugawanyika sehemu mbili, moja ikiwa na ulinzi wa polisi wanaotoa huduma zote na sehemu nyingine zikikosa huduma hizo.
Maeneo yaliyosalama ni Mkoani, Shangani na katikati ya mji wakati sehemu zilizoathirika ni pamoja na Majengo, Likonde na Mdenga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki, akizungumzia suala hilo alieleza kuwa polisi walilazimika kuhama baada ya waandamanaji kuvishambulia vituo vyao vya kazi.
Aliongeza kuwa polisi hawatarudi maeneo hayo mpaka ofisi hizi zitakapofanyiwa ukarabati kwani vitu vyote vimeharibiwa kwa kupigwa mawe na samani zake kuchukuliwa.
Wakazi wa Vigaeni, Omari Dadi na Mohamed Davalu waliliambia gazeti hili kuwa tangu polisi walipoondoka sehemu hiyo wananchi wanajiongoza wenyewe na hakuna kuzingatia sheria wakitaja za barabarani.
Walieleza hofu nyingine ni kuwa hakuna mjadala mwingine unaozungumzwa na wakazi zaidi ya kupinga ujenzi wa bomba la gesi.
“Polisi wakionekana sehemu hii wanazomewa na kulazimika kukimbia,” alisema Davalu.
HALI HALISI
Sehemu iliyotelekezwa na polisi imegeuka kuwa ‘kisiwa’ kutokana na wakazi wake kuzingatia hoja ya gesi katika mazungumzo ya kila wakati wakisisitiza gesi yao haitoki.
Hata kwenye salamu wanaamkiana ‘gesi kwanza vyama baadaye’ haitoki inatoka?
Katika salamu hiyo, anayejibu salama anasema ‘haitoki’
Maongezi hayo yanasikika kwenye migahawa, wanakocheza bao, stendi za daladala na ndani ya mabasi, sokoni na kwenye nyumba za kulala wageni.
WAPIGWA MARUFUKU
Wananchi hao wanasisitiza kuwa hawataki kusikia baadhi ya majina ya viongozi wa mkoa huo na wilaya zake lakini wakisisitiza kumuunga mkono mbunge wao Hasnaien Murji –Mtwara Mjini (CCM).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment