ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 26, 2013

SISTA ALIYEFUMANIWA ASABABISHA KIZAAZAA

Sista Yasinta Sindani,
SASA MKEWE ADAI TALAKA
Na Juddy Ngonyani, Sumbawanga
WAKATI Mahakama ya Mwanzo mjini Sumbawanga ikiwa imemtia hatiani aliyekuwa mtawa wa Shirika la Kitawa la Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga, Sista Yasinta Sindani, kwa kufumaniwa na mume wa mtu na kuamriwa kumlipa fidia ya Sh 700,000 mlalamikaji, ameleta kizaazaa kwa mwanaume kwa kumdai talaka.
Mke wa Martin Msangawale , Asteria Mgabo akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni alisema hukumu iliyotolewa ameridhika nayo pia anadhamiria kufungua shauri mahakamani hapo la kudai talaka.
“Baada ya hukumu kutolewa, nitaanza mchakato wa kufungua shauri mahakamani hapa kudai talaka kwani siko tayari tena kuendela kuishi na Martin,” alisema Asteria.
Wakati Asteria akisema hayo, habari zaidi zinasema mumewe Martin Msangawale, alikamatwa siku ya hukumu ya kesi hiyo wakati anajiandaa kuingia ndani ya mahakama kwa madai ya kujifanya afisa ardhi.
Akithibitisha habari hizo kwa mwandishi wa habari hizi, Mwanasheria wa Manispaa ya Sumbawanga, Tulalemwa Mwenda alisema ni kweli Martin amekamatwa.
“Martin alikamatwa akituhumiwa kujifanya ofisa ardhi wa manispaa hii na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na upelelezi juu ya tuhuma hizo unafanywa na polisi,” alisema mwanasheria Mwenda.
Afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji alikiri kukamatwa kwa Martin na upelelezi juu ya madai kuwa alijifanya afisa ardhi na kujipatia fedha, unaendelea.
Martin hivi karibuni ilithibitishwa mahakamani mbele ya hakimu wa mahakama hiyo , Jaffar Mkinga kuwa alifumaniwa na Sista Yasinta katika nyumba moja ya kulala wageni iitwayo Chipa mjini hapa ambapo mwanamke huyo alitozwa faini ya shilingi 700,000.

Global Publishers

No comments: