ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 23, 2013

Sitta ajitosa vurugu za kidini

Mh. Samwel Sitta
*Awanyooshea 'kidole' wakuu wa mikoa, wilaya

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amejitosa sakata la vurugu na mauaji ya viongozi wa kidini, akiwaelekezea ‘kidole’ wakuu wa mikoa na wilaya kuchukua hatua za awali za kudhibiti.

Kwa mujibu wa taratibu za utendaji kazi wao, wakuu wa mikoa na wilaya ambao ni wawakilishi wa Rais kiutawala, wanaziongoza kamati za ulinzi na usalama katika ngazi husika.

Sitta amesema wapo baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya walio waoga kiasi cha kushindwa kuchukua hatua za haraka katika kutatua migogoro ikiwamo inayohusishwa na masuala ya udini.
Sitta aliyasema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) uliofanyika mjini hapa.

Alisema kuwa woga wa viongozi katika ngazi za mikoa na wilaya umekuwa miongoni mwa vyanzo vya kukua kwa vurugu mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo mengi nchini.
kwa mujibu wa Sitta, viongozi hao wanatakiwa kuwa wepesi katika kuyatatua masuala mbalimbali yakiwemo yanayotishia amani na utulivu uliopo.

“Viongozi wa ngazi za mikoa na wilaya wawe wepesi katika kuchukua hatua za haraka kwa masuala ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo yao, kwa kuwa uwezo wa kufanya hivyo wanao siyo mpaka wamsubiri Waziri Mkuu aje kutatua migogoro,” alisema.

Akifungua mkutano wa TLS, Sitta alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), imeweka mkazo katika kuwawezesha wanasheria kufanya kazi kwenye nchi wanachama pasipo vikwazo.

Alisema kuwa kumekuwapo na mkazo wa kuangalia ni namna gani masomo ya sheria na lugha vinaweza kufanana, ili kuwasaidia wanasheria kufanya kazi katika nchi mbambali za Jumuiya hiyo.

Sitta alisema, pamoja na mkazo huo, bado kuna changamoto mbalimbali ikiwamo suala la lugha na mfumo wa sheria zinazotumika kwa hivi sasa, kuwa tofauti kwa baadhi ya nchi.
Alisema kuwa nchi kama Kenya na Tanzania zimekuwa zikitumia kiingereza tofauti na Rwanda na Burundi ambazo zinatumia kifaransa.

“Pamoja na kuwa baadhi ya wenzetu kutumia kifaransa, lakini hata mfumo wa kisheria pia umekuwa na utofauti, hivyo kama mwanasheria atatoka hapa kwenda huko anaweza kushindwa kufanya kazi yake ya kisheria” alisema.

Naye Rais wa TLS, Francis Stolla, alisema kuwa gharama za wanasheria zinazotolewa kwa wanachi ni kubwa kiasi cha kuwanyima walio wengi fursa za kupata haki zao.

Aidha alitoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kuona ni jinsi gani wanaweza kusaidia katika kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma za kisheria kwa gharama nafuu.


CHANZO: NIPASHE

No comments: