ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 4, 2013

UNAJUA UNAVYOMUUMIZA MWENZAKO?

TUMEKUTANA tena katika kona yetu kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku. Baada ya kumaliza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kusherehekea Sikukuu ya Idd El Fitr, nachukua nafasi hii kuwapa wapenzi wangu mkono wa Idd.

Nimepokea matatizo mengi katika uhusiano, kuhusiana na mtu kupenda na kugeuzwa mtumwa wa mapenzi na kupata mateso mazito.

Kama kawaida, kona hii inapopata matatizo huyafanyia kazi na kupata jawabu. Inaonekana watu wengi wamekuwa wakiumizwa na mapenzi kufikia hatua ya kujiona kama wametengwa na dunia. Wakila chakula kinakosa ladha, wakilala kupata usingizi inakuwa shida, wanapungua uzito kila kukicha kwa ajili ya mateso ndani ya mapenzi waliyomo.
Nilishawahi kusema ukimpata uliyempenda na kumkabidhi moyo wako naye akakupenda, basi utajiona upo katika pepo ya dunia, lakini ukimpenda mtu asiyekupenda na kumkabidhi moyo wako, basi mapenzi hugeuka moto, yakikutesa na kukupa maumivu ya moyo.

Naweza kuwa nimeanzia mbali kufikisha kile wa ninachotaka kukisema kama kichwa cha habari kinavyozungumza hapo juu. Katika falsafa ya mapenzi, upendo wa dhati ndiyo msingi imara unaolifanya penzi kuwa salama zaidi. Si wote wanaotambua thamani ya upendo wanapopendwa.

Siku zote wasiojua thamani ya upendo hawajui maumivu ya wenzao, mara nyingi watu wa aina hii hujiangalia wao wenyewe wakiamini kupendwa ni haki yao na si kupenda.

Hata matamshi yao huwa maumivu kwa wenzao bila kujali analolisema litamuathiri vipi mwenzake.

Upo na mpenzi wako lakini huna hata kitu cha kumfurahisha zaidi ya maneno ya kashfa au kufanya jambo lolote bila kumshilikisha kwa kuamini anakupenda na hana sehemu ya kwenda.

Lakini watu hao wanasahau hakuna mapenzi ya mmoja kucheka na mwingine kulia. Umekubali awe mpenzi wako, kwa nini unamuumiza?

Anakufanyia kila kitu kizuri ili kukuonyesha mapenzi lakini huoni, unamsubiri afanye makosa ili upate nafasi ya kumuumiza zaidi.

Hayo si mapenzi, huo ni ukatili, hebu tubadilike, tutambue kuwa maumivu ya moyo tunayosikia tunapofanyiwa kitu kibaya na wapenzi wetu, ndiyo wanayosikia na wao kama tukiwafanyia ubaya.

Kupitia makala haya, nawaombeni wote kurudisha furaha ndani ya nyumba au mapenzi yenu. Hukai na mpenzi wako mkacheka zaidi ya kukutana kitandani na pengine katika shughuli unajijali wewe, ukiwahi kufika basi humfikirii mwenzako.

Leo ukirudi kwako itazame nyumba yako halafu jiulize kama kuna furaha au majonzi.

Kama kuna majonzi na ikiwa hamsemeshani unatakiwa kujiuliza juu ya tatizo lililopo.

Kaa chini na mwenzako, zungumza naye kwa upole ujue nini tatizo, mkilifahamu, basi litatueni kwa busara ili kurudisha furaha ya ndani. Lazima uyajue maumivu ya mwenzako, hasa anapokupenda na kukuonyesha kweli anakupenda, hebu jione una deni la kumlipa upendo utakaomrudishia furaha.

Jione wewe ni sehemu ya furaha ya mpenzi wako, mhurumie, kwa nini ateseke, kwa nini aumie na wewe upo?

Hata kama mwenzako ana kosa, mna nafasi ya kukaa chini na kulimaliza kwa vile wanadamu upungufu ni maumbile yetu. Ukiyajua maumivu ya mwenzako, huwezi kumuumiza kamwe.

Leo inatosha tukutane wiki ijayo.

No comments: