ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 19, 2013

UVCCM wamtosa Lowassa, Nagu

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Baraza Kuu la Umoja wa Vijana la Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) limewaondoa makada wake maarufu katika Baraza la Wadhamini la umoja huo akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wake, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
 
Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji) na Mbunge wa Hanang, Dk. Mary Nagu, ambaye walishikilia nafasi hizo kwa miaka 10.
 
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela, alisema jana kuwa Baraza Kuu lililoketi kwa siku mbili limemteua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa mwenyekiti wa baraza hilo.
 
Wengine walioteuliwa kuwa wajumbe ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) na Mjumbe wa Kamati Kuu, William Lukuvi; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Anna Tibaijuka.
 
Wengine ni Naibu Waziri wa Fedha, na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), Janeth Mbene;  Mbunge wa Kikwajuni ambaye pia ni mjumbe wa Nec, Hamad Yusuf Masaun na  Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi,  Mohamed Aboud ambaye pia ni mjumbe wa Nec. Abood pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.
 
Baraza la zamani la wadhamini mbali na Lowassa na Dk. Nagu,  wajumbe wengine walikuwa ni Lukuvi; aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi; Hemed Yusuf Ahamed na Said Amour.
 
Shigela alisema baraza hilo ndilo litakuwa wasimamizi wa mali zote za umoja huo. “Tumeona kuwa tuingize damu ya vijana katika dhana nzima ya kujitegemea kama jumuiya,” alisema Shigela.
 
Shigela pia alisema kuwa wajumbe wengine wameteuliwa kwa lengo la kuisaidia jumuiya hiyo kutokana na utaalamu wao.
 
Lowassa ameondolewa katika jumuiya hiyo yenye ushawishi mkubwa ndani ya chama tawala wakati baadhi ya makada ndani ya CCM wakianza kujipanga kwa ajili ya mbio za kuwania uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
 
Kuwa na ushawishi ndani ya UVCCM kuna umuhimu mkubwa kwa anayewania uteuzi wa urais kutokana na nguvu na ushawishi wa vijana katika kampeni za uteuzi ndani ya chama.
 
Lowassa ni miongoni mwa makada ambao wanatajwa kujipanga kwa ajili ya kuwania uteuzi wa CCM kwa nafasi ya urais baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kwa mujibu wa katika mwaka 2015.
 
 
“MRADI WA GESI MTWARA
Shigela alisema Baraza Kuu la Umoja huo lilitaka kuadhibiwa kwa watu ambao walihusika katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mradi wa gesi Mtwara na hawakufanya hivyo.
 
“Wasiadhibiwe wale waliohusika na matukio ya kuchoma moto majengo na mali nyingine, bali hata wale ambao walitakiwa kutoa elimu hiyo, lakini hawakufanya hivyo.
AJIRA KWA VIJANA
 
Katibu huyo aliitaka serikali kuweka utaratibu wa kuwafanya wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwamo waendesha bodaboda kutobughudhiwa na vyombo vya dola.
 
Aidha, waliitaka serikali kuweka utaratibu ambao unawezesha wafanyabiashara hao kuondokana na kodi.
 
“Kama wafanyabiashara wakubwa wanaweza kusahamehewa kodi, kwa nini wasifanye hivyo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kuwaondolea bughudha?” alihoji
 
Aidha, waliitaka serikali kuongeza silabasi vyuoni hususani ya somo la ujasiriamali ili pindi wanahitimu wawe na elimu ya ujasiriamali.
 
Halikadhalika, Shigela alisema kikao hicho ambacho ni cha kwanza tangu uchaguzi ufanyike ndani ya chama, kiliwachagua wajumbe wa kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja huo.
 
Waliochaguliwa kwa upande wa Bara ni Daud Njalu, Reuben Sixtus, Seki Kasuga, Amini Mkalipa na Mariam Chaurembo.
 
Kwa upande wa Visiwani  ni Shaka Shaka, Bakari Vuai, Nadra Mohamed, Viwe Khamis na Ally Nassoro.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: