Sunday, February 3, 2013

UWT `warubuni` wanawake

Mwenyekiti wa Taifa wa UWT, Sophia Simba
  Yawaingiza CCM kwa kigezo cha kupewa mikopo nafuu
  Sophia Simba asema `wasiguswe`
Mkakati wa kuongeza idadi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaonekana kutumia nguvu kubwa wakati nchi ikieleke katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka ujao na Uchaguzi Mkuu 2015.
Tayari Jumuiya ya Wanawake (UWT), inatumia mikopo isiyokuwa na masharti magumu kama ‘ndoana’ ya kuwanasa wanawake na kuwaingiza katika chama hicho.
Wanawake na vijana ni makundi yanayotajwa na kulengwa na vyama vingi vya siasa nyakati za uchaguzi, wakiaminika kuongoza miongoni mwa wapiga kura.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE Jumapili kwa takribani mwezi mmoja sasa, umebaini kuwa UWT kupitia viongozi wake wa ngazi ya taifa, imekutana na wanawake katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, na kuwashawishi kujiunga CCM.
Jitihada hizi zinafanywa, kuwakutanisha wanawake kwa ahadi ya kupewa mikopo ya kati ya Shilingi 500,000 na 1,000,000. Taarifa za awali zinaelezwa kwa wanawake kwamba mikopo hiyo inatolewa na UWT na haina riba.
Mbali na kutokuwa na riba, mikopo inaelezwa kutolewa pasipo dhamana kwa mkopaji, hali iliyoibua hisia tofauti kwa baadhi ya wanawake.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa NIPASHE Jumapili, idadi kubwa ya wanawake hasa wenye kipato cha chini na wasiokuwa na uhakika wa mitaji, wameshajitokeza na kujiunga CCM kupitia UWT.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, wanawake wanapokutanishwa kwenye maeneo yao, wanataarifa kuhusu kuwepo mpango wa UWT kuwapa mikopo isiyokuwa na riba.
Hata hivyo, sharti wanalopewa wanawake hao ni kujiunga katika UWT ambapo wanakabidhiwa kadi za uanachama bure.
“Tulipoitwa tukapewa kadi za UWT (kwa wale ambao hatukuwa nazo), kesho yake wakatupeleka kupata semina kuhusu mikopo,” kilieleza moja ya vyanzo vyetu.
Mafunzo kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, inaelezwa kutolewa na wawakilishi waliojitambulisha kutoka benki ya ABC.
Imebainika kuwa, wanapokuatana kwa mara ya kwanza, wanawake hao wanapewa ahadi ya kukopeshwa na UWT, baadaye jukumu hilo linabadilika kuwa la benki hiyo.
Maofisa wa benki hiyo wanapokutana na wanawake hao, wamekuwa wakiwajulisha kuwa pamoja na kufungua akaunti kwa kianzio cha Shilingi 10,000,, wanatakiwa kuweka na kuchukua fedha kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu.
“Walituambia tutakopeshwa kwa riba ya asilimia 1.6 na kuanzia Shilingi 500,000 hadi 1,000,000 na mkopaji anatakiwa alipe deni lake ndani ya miezi sita,” kilieleza chanzo kingine.
Aliongeza kuwa maelezo waliyopewa awali na UWT yalikuwa tofauti ya waliyoyapata kutoka kwa maofisa wa benki.
“UWT walituambia tukishafungua akaunti tu, tunapata mikopo, lakini watu wa benki wakasema mpaka tuweke na kuchukua fedha kwa miezi hadi mitatu, wajiridhishe na mwenedo wa fedha zetu.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi wa UWT, waliwataka wanawake hao kufungua akaunti NMB, kwa maelezo kwamba mikopo yao itapitishwa huko.
“Lakini ABC walipokuja, walituambia tufungue akaunti na tuweke fedha kwenye benki yao ndipo watatupatia mkopo kulingana akiba zetu,” alisema mmoja wa wanawake, mkazi wa kata ya Kimara.
Aliongeza, “sisi hatukuwa na shida ya kujiunga na benki wala UWT, tungekuwa na shida tungeenda maofisini kwao, lakini lengo lilikuwa tupewe mikopo vinginevyo walitupotezea muda wetuy.”
HISIA ZA ‘KUTAPELIWA’
Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, mpango huo umetafsiriwa kama ulilenga ‘kuwatapeli’ wanawake ili wajiunge kwa wingi katika CCM kupitia UWT.
Aidha, wapo wanaoamini kwamba huenda mpango huo uliratibiwa kwa maslahi binafsi yenye lengo la kuifanya benki hiyo iongeze wateja wake kwa kasi.
“Hata kama mtu hafuatilii kisiasa, atajua tu kuwa mambo haya yana malengo ya kisiasa kwa njia za ulaghai hasa kwa sisi tusio na vipato vya kutosha,” kilieleza chanzo kingine.
SOPHIA SIMBA ANENA
NIPASHE Jumapili ilipowasiliana na Mwenyekiti wa Taifa wa UWT, Sophia Simba, huo ni moja ya mikakati yenye kukidhi ushindani wa kisiasa.
Kisha, Simba ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alihoji kama mwandishi wa habari hii ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akiwa amepigiwa saa 6:17 ambapo aliikata kwa madai yupo mkutanoni, saa 8:28 alipigiwa ndipo akasema, ““hukunielewa mara ya kwanza nilivyokueleza kuwa nina kikao, mbona msumbufu hivyo.”
Alipohojiwa zaidi, Simba alisema, “hayo mambo ni ya ushindani wa kisiasa, hayakuhusu wewe mwandishi wa habari.”
“Huu ni mkakati wetu wa chama, hautakiwi kuufahamu zaidi, nitajuaje kama wewe ni Chadema,” alihoji na kukata simu.
Hata hivyo, NIPASHE Jumapili ilimpigia tena simu Simba, ambapo alisema UWT hawana benki, bali wameanzisha Saccos zinazotumika kwa ajili ya kuwakopesha wanachama wao.
Alipulizwa namna wanavyowakopesha wanawake na asilimia za riba wanazowatoza na kama mkakati wa kuwakopesha umeshaanza, alikata simu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, alipoulizwa kuhusu mpango huo, alijibu, “suala lenyewe umeshasema mpango, sasa hatuwezi kuuzungumza kwenye simu,” alisema
ABC WAKANA `KUEGEMEA’ UWT
Kiongozi mmoja wa benki ya ABC, akizungumza kwa sharti la kutotaka kutajwa jina lake , alisema hawana mpango wa `kuviegemea’ vyama vya siasa ikiwemo CCM, ili kupata wateja wao.
Badala yake alisema benki hiyo inakopesha watu tofauti kupitia dhamana zinazohusisha ofisi za serikali za mitaa na ngazi ya kata.
“Hilo la kutumiwa na UWT silifahamu zaidi, ninachikifahamu ni hicho nilichokueleza,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: