ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 9, 2013

Waganga feki wanavyochota mamilioni

BAADHI ya waganga wa kienyeji nchini sasa wamegeuza matatizo ya Watanzania kuwa mitaji yao ya kujipatia mamilioni ya fedha kwa madai kwamba wanawapatia tiba.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumamosi umebaini kuwa wengi wa waganga hao wanaojipatia fedha kwa njia ya kuwadaganya wananchi ni wale ambao hawajasajiliwa na Serikali. Moja ya uthibitisho wa kwamba huduma hiyo haramu huwapatia fedha nyingi waganga hao ni kuenea kwa mabango mengi yanayotangaza kuwepo kwa waganga hao.

Katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam na miji migine mikubwa nchini huwezi kutembea mwendo mrefu bila kukutana na kibao kinamtangaza mganga wa kienyeji kutoka ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa waganga hao, wapo wanaojitangaza kutibu watu walio na matatizo ya nguvu za kiume, wanaotaka kupata utajiri wa haraka, kutibu mwanafunzi ambaye hana akili darasani, kuolewa au kuoa haraka, kumvuta mpenzi aliye mbali, kunenepesha makalio na kurefusha maumbile ya sehemu za siri kwa wanaume na mengineyo.

Wingi wa matangazo hayo unaashiria pia kuwapo kwa watu wengi wenye matatizo na wanaotumia huduma hizo, ambao huwasiliana na waganga hao kwa njia ya simu zilizoandikwa kwenye matangazo yao ya kuvutia wateja. Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi Jumamosi umebaini kuwa waganga hao wengi ni feki, ambao hawana tiba hiyo, badala yake wanajipatia mamilioni kutoka kwa wananchi hao wakiwaachia madhara, pengine kusababisha vifo.

Baadhi ya waganga hao, ambao wanaweka mabango yao jijini Dar es Salaam kutangaza tiba yao ni lile linalosomeka Dk .. wa Nigeria anatibu matatizo akili darasani, mafanikio siku tatu, kukuza uume, kung’arisha nyota, makalio na magonjwa mengine.
Tangazo jingine la mganga wa kienyeji linalosomeka : “Dk … anatibu, ugumba, nguvu za kiume, mvuto wa mapenzi, kumwita mpenzi aliye mbali na utajiri wa haraka.”

Yapo matangazo mengine ambayo yanaonyesha kuwa wanatoa huduma mbalimbali ikiwamo kurejesha fedha ambazo mtu alidhulumiwa, kulipiza kisasi kwa mtu aliyekukosea, kupata nguvu za ajabu katika kufanya mapenzi, kutibu Ukimwi, saratani, mabusha, magonjwa wa zinaa na kupata utajiri kwa siku mbili.
Katika uchunguzi wake Mwananchi Jumamosi liliwasiliana na waganga wawili mmoja akijitaja kuwa ametoka Nigeria akiwa na ofisi zake Mbezi Makonde jijini Dar es Salaam na kuzungumza naye kwa simu ya mkononi kujua namna anavyotoa tiba yake na mazungumzo yalikuwa hivi

Mwananchi Jumamosi: Halo Dk Abuja, nimechukua namba yako katika tangazo la biashara zako, mimi nina shida!
Dk Abuja: Shida gani sema?

Mwananchi Jumamosi: Nina mtoto wa dada yangu anasoma kidato cha pili, lakini ana matatizo ya kutoelewa darasani, gharama yake itakuwaje?
Dk Abuja: Inawezekana kabisa, gharama ni Sh 50,000, lakini naomba unitumie kwanza jina la mtoto huyo na unirushie Sh21,000 kwa njia ya simu sasa hivi, ili ni mwangalie kwanza huku.

Mwananchi Jumamosi: Sasa baada ya kumfanyia matibabu hayo anatakiwa kusubiri kwa muda gani?

Dk Abuja: Nakupa wiki moja tu, tena utashangaa mno, yaani atakuwa na uwezo wa kuwafundisha wanafunzi wa kidato cha nne.

No comments: