Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mchana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratius Lyato alisema kuwa Wambura ameenguliwa kwakuwa hakukidhi matakwa ya katiba ya TFF na kanuni za uchaguzi za TFF ibara ya 9(7) kwa vile alifungua kesi ya madai namba 100 ya 2010 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam dhidi ya Mwenyekiti wa klabu ya Simba akiwa ni mwanachama wa klabu hiyo, kinyume na katiba ya Simba.
“Kwa kufanya hivyo, Michael Wambura alivunja katiba ya Simba, alikiuka katiba ya TFF na katiba ya FIFA,” alisema Lyato.
Mwenyekiti huyo aliendelea kueleza kuwa kamati yake inaheshimu maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Rufaa ya TFF kuhusu uchaguzi wa mwaka 2008 kwamba Michael Wambura hakukidhi matakwa ya ibara ya 29(7) ya katiba ya TFF na ibara ya tisa (9) ya kanuni za Uchaguzi za TFF na kwamba kwa mujibu wa katiba ya TFF na kanuni za uchaguzi za TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF haina mamlaka ya kubadilisha maamuzi yaliyofikiwa na kamati hiyo ya rufaa.
“Maamuzi hayo yanaweza tu kubadilishwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS),” alisema zaidi Lyato.
Alisema kuwa kamati yake imepitisha wagombea wawili, Wallace Karia na Ramdhani Nassib kuwania nafasi ya makamu wa rais wa TFF na kumuengua Wambura katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.
WAMBURA ANENA
Akizungumza na NIPASHE jana, Wambura alisema kuwa amezipokea kwa masikitiko taarifa za kuenguliwa kwake na kwamba anafikiria kupinga maamuzi hayo kwenye Kamati ya Rufani ya TFF.
“Nimepata taarifa kwamba nimeondolewa kuwania nafasi kwenye uchaguzi wa TFF. Kwa sasa (jana jioni) natafakari nichukue hatua gani lakini natarajia kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya TFF kwa sababu suala langu na Simba lilishapatiwa ufumbuzi,” alisema Wambura.
Aidha, Lyato alieleza kuwa Mussa Nkwaluro aliyekuwa ameomba kuwania nafasi ya rais wa TFF naye ametemwa kutokana na Ibara ya 9(7) ya kanuni za uchaguzi wa TFF kwa kutokuwa na ufahamu wa kuridhisha kuhusu majukumu na wajibu wa nafasi anayoomba na uwezo wa kutekeleza majukumu na malengo ya TFF.
Lyato alisema kuwa kamati yake imewapitisha wagombea Jamal Malinzi na Jumanne Nyamlani kuwania nafasi hiyo.
Upande wa bodi ya ligi, wagombea wote waliomba kuwania nafasi za uongozi wamepitishwa isipokuwa Christopher Lunkombe ambaye ameondolewa kwa kile kilichoelezwa na Lyato kuwa hakukidhi matakwa ya kanuni za uendeshaji za bodi ya TPL ibara ya 28(2) kwa kuwa cheti chake cha elimu ya sekondari kina utata.
Kwa mujibu wa Lyato, wagombea wafuatao na kanda wanazotoka kwenye mabano wameondolewa kuwania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF baada ya kutokidhi matakwa ya kanuni za uchaguzi wa TFF:-
Abdallah Hussein Musa (Kagera na Geita), Mbasha (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo (Arusha na Manyara), Ayubu Nyaulingo (Rukwa na Katavi), Nazarius Kilungeja (Rukwa na Katavi), Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya) na Farid Nahdi (Morogoro na Pwani)
Wengine ni Hassan Othuman (Morogoro na Pwani), Omary Isack (Dar es Salaam) na Shafii Dauda (Dar es Salaam).
Uchaguzi wa bodi ya TPL utafanyika Februari 22 na uchaguzi wa TFF utafanyika Februari 24 jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment