ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 7, 2013

Arsenal kuwabomoa Swansea


Joe Allen and Ashley Williams of Swansea defend against Mikel Arteta of Arsenal (Photo credit: Wikipedia)
*Watenga £ mil. 8 kumchukua beki Williams
*Wapanga safari Vietnam kujiimarisha Julai
 

Arsenal wameanza kuangalia ‘maisha baada ya msimu huu mbaya’, kwa kutaka kumsajili nahodha wa Swansea, Ashley Williams na kwenda Vietnam.
Baada ya msimu unaowaendea vibaya ambapo si ajabu wakakosa nafasi kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arsene Wenger sasa amekiri hana beki.

Katika hilo, ametenga pauni milioni nane kwa ajili ya kumng’oa nahodha na mkoba wa Swansea, Ashley Williams.

Ama kwa safari na mechi kabla ya msimu ujao, Arsenal wametenga siku tatu za kukaa Vietnam, na watakuwa timu ya kwanza ya Ligi Kuu England kwenda huko kwa ‘vichaa’ wa soka.

Vietnam ina watu milioni 90 na ni taifa la wapenda soka, hivyo Arsenal wanaona ni eneo muhimu kuongeza mashabiki wake.

Arsenal wanao pia mashabiki wengi kutoka bara la Afrika na Asia na wamekuwa na utamaduni wa kuwa na wachezaji mchanganyiko wa rangi kwenye kikosi chao.

Wakiwa mji mkuu wa Vietnam, Hanoi, Arsenal wamepanga kuchezesha kikosi kamili dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo ya kikomunisti kati ya Julai 15 na 17 kwenye Uwanja wa Taifa wa My Dinh.

Kwa miaka kadhaa, Arsenal wamekuwa wakisaidia miradi ya soka ya Vietnam kwa ajili ya kukuza wachezaji chipukizi kupitia Hoang Anh Gia Lai-Arsenal JMG Academy.

Tayari wametangaza mechi nyingine jijini Jakarta, Indonesia na nyingine katika nchi ambayo haijatajwa barani Asia.

Imekuwa kawaida Arsenal kwenda Austria kabla ya msimu kuanza, lakini shinikizo za kibiashara zimewasukumia Asia miaka ya karibuni.

Liverpool, Manchester United, Chelsea na Manchester City nao pia wanatarajiwa kukwea pia hadi Asia kwa ajili ya mechi za maandalizi ya msimu ujao.

Baada ya ulinzi dhaifu mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Tottenham Hotspurs ambapo Arsenal walilala kwa mabao 2-1, imedhihirika wameanza kupoteza imani na walinzi wake wa kati, nahodha Thomas Vermaelen na Per Mertesacker.

Mabao yote mawili ya Spurs yaliyofungwa na Gareth Bale na Aaron Lennon yalikuwa laini na yanayozuilika na wadau wameinyooshea kidole beki.

Williams anakadiriwa kugharimu pauni milioni nane, lakini Arsenal wanaweza kulazimika kuongeza dau, kwani Brendan Rodgers wa Liverpool naye anamwangalia kijana huyo huyo mwenye umri wa miaka 28.

Williams ni nahodha wa Timu ya Taifa ya Wales na Wenger anaamini ni mtu mwenye tunu za kiuongozi anayeweza kupanga na kudhibiti mfumo wa ulinzi wa Arsenal.

Anataka kuurejesha ukuta huo enzi zile za mafanikio, ukiwa chini ya watu kama Tony Adams, Martin Keown au Steve Bould ambaye sasa ni kocha msaidizi wa Arsenal na mtaalamu wa kunoa mabeki.

Williams ana mkataba hadi 2015, ndiyo maana gharama yake inatarajiwa kwenda hadi £8m. amekuwa nguzo ya mafanikio ya Swansea tangu alipojiunga akitoka Stockport County enzi za kocha Roberto Martínez.

Tanzania Sports

No comments: