Wazazi wa aliyekuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM)marehemu Benson Mollel,Suzana na Peter Mollel wakiweka shada la maua katika kaburi la marehemu mtoto wao jana nyumbani kwao Lemara jijini Arusha.Picha na Moses Mashallah
Wafuasi wa Chadema, wameibua tafrani ya aina yake wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), marehemu Benson Mollel baada ya kung’oa bendera za chama hicho na kuamsha hasira za waombolezaji wafuasi wa chama tawala.
Mollel alikutwa amefariki mwanzoni mwa wiki, katika Hoteli ya Lush Garden Business, Mtaa wa Jacaranda Arusha huku mwili wake ukiwa mtupu.Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana na baadhi ya makada wa CCM walionekana wakiwasaka wafuasi hao wa Chadema.
Mashuhuda walisema tukio hilo lilitokea saa 8:30 usiku na baadhi ya wafuasi wanaosadikika kutoka Chadema walichukizwa na kuwapo kwa bendera hizo msibani na hivyo kuanza kuzing’oa.
Hata hivyo, mara baada ya tukio hilo, makada wa CCM waliamua kuzirudisha bendera hizo katika eneo la msiba, safari hiyo ya pili wakiamua kuweka vijana wa kuzilinda.
Mamia wajitokeza kumzika Mollel
Mbali na rabsha hizo, jana mamia ya waombolezaji walijitokeza kumzika kada huyo wa CCM.
Waombolezaji hao waliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigella, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na wakazi mbalimbali wa Arusha na mikoa mingine.
Mwili wa marehemu uliwasili nyumbani kwake saa 2:00 asubuhi ukitokea Hospitali ya Mt. Meru huku jeneza lake likiwa limefunikwa kwa bendera ya CCM na kufuatiwa na shughuli za kutoa heshima za mwisho.
Askofu Mkuu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomon Masangya aliendesha ibada maalumu ya mazishi.
Katika salamu zake, Shigella alisema marehemu atakumbukwa kwa mchango mkubwa wa kuwaunganisha vijana ndani ya CCM na kuwataka wengine kufuata nyayo za marehemu.
Alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo alikuwa akiyasimamia wakati wa uhai wake ilikuwa ni amani, haki na mshikamano ndani ya chama na kuwataka wana UVCCM kuenzi mambo hayo.
Kwa upande wake, Mulongo alisema kutokana na utata wa kifo hicho, uchunguzi wa kina unaendelea na kuwataka wananchi kuwa na subira.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment